JESHI
la Polisi mkoani Kilimanjaro, limekamata shehena ya meno ya tembo
iliyokuwa ikisafirishwa kutoka mji wa Tarakea mpakani na Kenya kwenda
mjini Moshi.
Shehena
hiyo ilikuwa ikisafrishwa ndani ya gari aina ya Toyota Noah lenye namba
za usajili T 557 BST linalodaiwa kumilikiwa na askari polisi wa kituo
cha Tarakea, Koplo Phabian.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alikiri jana kukamatwa
kwa shehena hiyo na kwamba watu wawili wanashikiliwa kwa kosa la kukutwa
na nyara za serikali.
Kamanda
Boaz alisema gari hilo baada ya kupekuliwa lilikutwa likiwa na vipande
sita vya meno ya tembo, ingawa hakuweza kufafanua zaidi meno hayo
yalikuwa yasafrishwe kwenda nchi gani.
Waliokamatwa
kwa mujibu wa Kamanda Boaz ni Sharifa Athuman (35) ambaye ni Mtanzania
anayeishi eneo la Kimana nchini Kenya na Raphael Emmanuel (25) mkazi wa
Magamba mkoani Tanga.
Kwa
mujibu wa kamanda, gari hilo lilikamatwa jana saa 2 asubuhi na askari
polisi waliokuwa kwenye kizuizi cha barabara katika mji mdogo wa Himo
Wilaya ya Moshi Vijijini.
Kukamatwa
kwa meno hayo ya tembo kunakuja siku chache baada ya Waziri wa
Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki, kukiri kuwapo na mtandao
mkubwa wa majangili wanaojihusisha na biashara ya meno ya tembo na pembe
za ndovu.
Kagasheki
alikiri kuwapo kwa mtandao huo wenye nguvu kifedha wakati akipokea
faru watatu weusi kutoka nchini Uingereza, ambao walipelekwa katika
Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi. NA TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment