ALIYEKUWA
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Frederick Mwakalebela
anatakiwa ajisalimishe Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) badala ya kusubiri kukamatwa baada ya vipengele alivyotumia
kukata rufaa dhidi ya kesi yake ya rushwa wakati wa uchaguzi kutupiliwa
mbali baada ya kuonekana havina nguvu mbele ya Mahakama Kuu Kanda ya
Iringa.
Agosti
mwaka 2010, Takukuru ilimfikisha mahakamani Mwakalebela kwa tuhuma za
kujihusisha na utoaji wa rushwa wakati wa kampeni za kura za maoni za
ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo la Iringa Mjini.
Katika
kura hizo, Mwakalebela alimshinda kwa mbali aliyekuwa Mbunge wa Jimbo
la Iringa Mjini Monica Mbega, hata hivyo alienguliwa kuwania ubunge
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo baada ya Takukuru kumfikisha
mahakamani kwa tuhuma hizo.
Katika kesi hiyo, Mwakalebela na
mkewe Selina, kwa pamoja walikuwa wakituhumiwa kutoa hongo ya shilingi
100,000 kinyume cha sheria namba 15 (1) , (b) cha sheria ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), ambayo inasomwa kwa pamoja na kifungu
cha 21 (1) , ( a) na 24 (8) ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka
2010.
Mwezi Mei mwaka jana, Mahakama ya
Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, ilitupilia mbali kesi hiyo baada ya
kusikiliza mapingamizi yaliyokuwa yamewekwa na Wakili wa mshitakiwa,
Basil Mkwata na kuamuru upande wa jamuhuri kuifanyia mabadiliko hati
hiyo kama wanataka kumfikisha tena mtuhumiwa huyo mahakamani.
Takukuru ikiwa katika mchakato wa
kuifanyia mabadiliko hati ya mashitaka, wakili wa mshatkiwa alikata
rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa akiomba mahakama hiyo itolee uamuzi
mapingamizi mengine ya kisheria ambayo Mahakama ya Hakimu Mkazi
haikuyatolea uamuzi na mengine ikiyatolea uamuzi kimakosa.
Hoja ya kwanza ya wakili wa
mshitakiwa iliyosikilizwa na Jaji aliyeendesha kesi hiyo jana, Rehema
Mkuye ilidai, hati ya mashitaka iliyokuwa imaendaliwa na Jamuhuri
haitengenezi kosa la jinai kisheria kwa kuwa makosa yote kama
yalivyokuwa yametajwa kwenye hati hiyo yalikuwa yanakosa maneno.
Katika hoja hiyo, Jaji Mkuye alisema
mahakama imepitia hoja za pande zote mbili na kuona hoja hiyo ingekuwa
na nguvu kisheria kama mashahidi wangeitwa na kisha kutoa ushahidi wao.
“Kwa kuwa hilo bado halijafanyika Mahakama Kuu inatupilia mbali kigezo hicho cha rufaa,” alisema Jaji huyo.
Hoja ya pili ya rufaa hiyo ilieleza
kwamba Kifungu cha 21 (1) (a) na Kifungu cha 24 (8) cha Sheria ya
Gharama za Uchaguzi Sheria No 6 ya mwaka 2010 ambacho mshitakiwa alikuwa
ameshitakiwa nacho, hakikutengeneza kosa la jinai kisheria.
Baada ya kusikiliza hoja za pande
zote mbili, Mahakama iliona hoja zote zina nguvu kisheria lakini Jaji
Mkuye alisema kulingana na kifungu cha 359 (2) cha sheria hiyo hiyo,
hoja hiyo haikuwa imetolewa uamuzi wowote na Mahakama ya Hakimu Mkazi
Mkoa hivyo haikutakiwa kukatiwa rufaa kwasababu hakukuwa na amri yoyote
ya mahakama ya awali.
“Hivyo kwa kuwa rufaa iliyokuwa
imekatwa na Wakili wa Mwakalebela ilikuwa na hoja mbili ambazo zote
mahakama imezitupilia mbali, hivyo mahakama inatupilia mbali rufaa yote
na amri ya mahakama ya Hakimu Mkazi ya kuifanyia marekebisho hati ya
mashtaka na kumfikishe tena mtuhumiwa Mahakamani sasa itatekelezwa,”
alisema jaji Mkuye.
Kaimu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa
Iringa Stephen Mafipa alisema baadaye kwamba kikosi chake hakihitaji
kumtafuta mtuhumiwa, bali atumie busara kujisalimisha ili afikishwe
mahakamani.
Wakili wa mtuhumiwa alipofuatwa na
vyombo vya habari ili atoe msimamo kwa niaba ya mteja wake ikiwa ni
pamoja na kama watakata rufaa katika Mahakama Kuu ya Rufani kupinga
maamuzi ya Mahakama kuu, hakupatikana ofisini kwake
No comments:
Post a Comment