DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com
Fax: 255-22-2113425 |
PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA
MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KUFUATIA AJALI
YA KUZAMA KWA MELI YA MV SKAGIT ILIYOTOKEA TAREHE 18 JULAI, 2012,
CHUMBE, ZANZIBAR
Jana tarehe 18 Julai,
2012, majira ya alasiri kumetokea ajali ya kuzama kwa meli ya MV SKAGIT
katika eneo la Chumbe, Zanzibar. Meli hiyo iliyokuwa ikitokea Dar es
Salaam kueleka Zanzibar ilikuwa imebeba watu 290. Kati yao watu wazima
250, watoto 31 na wafanyakazi wa meli 9.
Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete aliagiza vyombo vya ulinzi na usalama vya Serikali ya
Muungano yaani JWTZ na Polisi waanze kazi ya uokoaji mara moja.
Kazi hiyo imefanywa kwa
kushirikiana na vyombo vya usalama vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na
meli za makampuni binafsi. Mpaka giza lilipokuwa limeingia na hivyo
kazi ya uokoaji kusitishwa mpaka kutakapokucha tarehe 19 Julai, 2012,
watu 136 walikuwa wameokolewa na maiti 31 zilikuwa zimepatikana. Aidha,
mali zilizokuwa kwenye meli hiyo hazikuweza kuokolewa.
Kufuatia ajali hiyo, Rais
wa Jamhuri ya Muungano alizungumza na Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Alimpa pole kwa ajali iliyotokea hasa kwa vifo na majeraha waliyopata
Watanzania wenzetu na watu wasiokuwa raia wa Tanzania. Alimuomba
afikishe salamu za rambirambi kwa ndugu zetu waliopotelewa na jamaa zao
na kuwapa pole waliopata majeraha na maumivu maungoni mwao. Rais wa
Jamhuri ya Muungano alisema kuwa huu ni msiba wetu sote na kwamba
majonzi yao ni majonzi yake na ya Watanzania wote. Kwa ndugu zetu
waliojeruhiwa tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape ahueni na wapone
haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za kujiletea maendeleo na
kulijenga taifa letu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein na viongozi wote wa ngazi mbalimbali
kwa uongozi wao thabiti tangu taarifa ya kutokea kwa ajali mpaka sasa.
Aidha, amewapongeza maafisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama na
wafanyakazi wa meli binafsi, kwa juhudi kubwa walizozifanya za uokoaji
wa ndugu zetu waliopatwa na maafa haya makubwa na ya aina yake.
Amewataka waendeleze juhudi hizo leo na siku zijazo.
Rais amewataka wananchi
wawe na moyo wa subira na uvumilivu wakati kazi ya uokoaji inaendelea.
Kama ilivyofanyika katika ajali ya MV Spice Islander miezi 10 iliyopita,
uchunguzi wa kina utafanyika kubaini chanzo cha ajali.
Kutokana na ajali hiyo na
msiba huu mkubwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ametangaza maombolezo ya taifa ya siku tatu
ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia leo, tarehe 19 Julai,
2012.
Asanteni sana.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
19 Julai, 2012
No comments:
Post a Comment