KATIBU
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ), Dk. Willibrod
Slaa, amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinachukiwa na wananchi
kutokana na kuendelea kujitetea kwa kutumia sababu zilizotumiwa na
wapigania uhuru wa Tanganyika kujikomboa katika mikono ya wakoloni.
Akizungumza katika
mikutano ya hadhara kwenye vijiji mbalimbali vya kata za Ngerengere na
Makambarai, Dk. Slaa alisema serikali ya CCM imeshindwa kutengeneza
fursa ya wananchi kujiletea maendeleo yao licha ya kuwa katika nchi
yenye rasilimali nyingi.
“Mwalimu
Nyerere pamoja na wapigania uhuru wengine wa Tanganyika hawakumkataa
mkoloni kwa sababu ya rangi, dini wala hali zao isipokuwa waliwakataa
kwa vile walishindwa kuwaondolea watu umaskini, ujinga na maradhi ambayo
yanaendelea kutuandama kila wakati,” alisema.
Alisema
kuwa hayati Mwalimu Nyerere alifikia malengo kwa kuonesha njia ya
kupita, hivyo waliomfuatia walikuwa na wajibu wa kuhakikisha njia hiyo
inapitika lakini serikali ya CCM imeamua kuziba njia hiyo.
Huku
akisoma takwimu za maendeleo katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki,
linaloongozwa na Dk. Lucy Nkya (CCM), Dk. Slaa alisema kuwa hakuna
sababu ya kuendelea kukivumilia chama hicho kwa sababu ya kufanana kwa
rangi na badala yake wananchi wanapaswa kuchukua hatua ya kukipumzisha.
“Kila
mmoja hapa amesikia takwimu nilizosoma, tena zinatokana na vitabu vya
serikali yenu hii mliyoichagua na kuiweka madarakani, mlichagua rais wa
CCM, mbunge wa CCM, Diwani wa CCM, mwenyekiti wa kijiji na serikali ya
kijiji ya CCM, sasa nawasomea hapa ufisadi unaofaywa mnaanza
kusikitika,” alisema.
Alisema
ni aibu miaka 50 baada ya Uhuru kusikia Watanzania wakizungumzia
upungufu wa madawati wakati nchi nyingine zikiwa zinashindana kwenda
kuangalia uwezekano wa kufanya utafiti utakaozisaidia nchi zao.
na tanzania daima
No comments:
Post a Comment