Tarehe
10 Septemba 2012 majaribio ya usafiri wa treni katika jiji la Dar es
salaam yalifanywa kuanzia Stesheni mpaka Ubungo Maziwa. Kufuatia
majaribio hayo kauli kuhusu changamoto zilizopo ilitolewa na Naibu
Waziri Dkt Charles Tizeba na maoni mbalimbali yametolewa na wadau
wengine kwenye vyombo vya habari tarehe 11 na 12 Septemba 2012.
Kwa
nafasi yangu ya Mbunge wa Ubungo katika Jiji la Dar es salaam natambua
kuwa majaribio hayo ni hatua muhimu katika suala ambalo tangu mwaka 2010
kwa nyakati mbalimbali nimeihoji Serikali kutaka utekelezaji wa haraka
kwa kuzingatia kuwa suala hilo lilikuwa kwenye mipango zaidi ya miaka 10
iliyopita hata hivyo hatua zaidi na za haraka zinahitajika kwa huduma
ya usafiri wa reli kuanza tarehe 1 Oktoba 2012 na kuweka mazingira bora
ya usafiri huo kupunguza msongamano.
Natoa
mwito kwa Waziri na Naibu Waziri wa Uchukuzi kuzingatia mchango wangu
nilioutoa bungeni mwezi Agosti 2012 ili kuhakikisha kwamba TRL na RAHCO
zinashirikiana kwa karibu na Halmashauri za Jiji la Dar es salaam
kushughulikia changamoto zinazohusu uvamizi wa maeneo ya hifadhi za njia
za reli na ufinyu wa eneo la kugeuzia vichwa vya treni sehemu ya Ubungo
Maziwa.
Aidha,
Wizara ya Uchukuzi iharakishe mchakato wa kushirikiana na sekta binafsi
kuhusu uwekezaji katika mradi wa maegesho ya magari eneo Ubungo ikiwemo
katika eneo lililotengwa la ekari nne katika Chuo Cha Taifa cha
Usafirishaji ili wenye magari wanaokwenda Stesheni kuweza kuegesha
magari yao na kupunguza msongamano wa magari kuelekea katika ya Jiji.
Pia,
kwa kiwango cha fedha kiasi cha shilingi bilioni 4.75 zilizotengwa
kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013 zitolewe zote mapema ikiwa ni
sehemu ya matumizi vipaumbele na zielekezwe katika pamoja na mambo
mengine kuboresha hali na hadhi ya mabehewa pamoja kurekebisha mataruma
ya reli yakae pembe mraba na reli (squaring) ili kuongeza kasi ya treni
hiyo kuwezesha muda wa safari kati ya stesheni ya Dar es salaam na
Ubungo Maziwa kuweza kuwa dakika 35 tofauti na kasi ndogo iliyodhihirika
tarehe 10 Septemba 2012 wakati wa majaribio.
Ikumbukwe
kuwa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kati ya masuala ambayo
niliwaahidi wananchi kuwa nitayaunga mkono na kuisimamia Serikali
kuhakikisha yanatekelezwa kwa wakati ikiwa ni sehemu ya kuchangia katika
kupunguza msongamano wa magari ni pamoja na kuanzishwa kwa usafiri wa
treni kuelekea katika ya jiji.
Mara
baada ya kuchaguliwa wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Uchukuzi
mwaka 2011 niliitaka Serikali kuchukua kutoka katika fedha zilizotengwa
kwenye usafiri na uchukuzi wa reli kufanya tathmini na kuanza ukarabati
wa njia ya reli ya kutoka stesheni hadi Ubungo Maziwa.
Wizara
ya Uchukuzi ilijibu mwaka 2011 kuwa imekubaliana na mchango huo na
kuahidi kupitia Shirika la Reli (TRL), Kampuni ya Miliki ya Rasilimali
za Reli Nchini (RAHCO) na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA)
kuwa imefanya tathmini ya gharama za kuanzisha huduma za reli na kuanza
utekelezaji katika mwaka wa fedha 2011/2012.
Izingatiwe
kuwa bajeti ya utekelezaji imeongezwa zaidi katika mwaka wa fedha
2012/2013 ambayo inapaswa kufuatilia kwa karibu na mamlaka zote
zinazohusika pamoja na wadau wote muhimu ili kuhakikisha ubora na
ufanisi.
John Mnyika (Mb)
No comments:
Post a Comment