Rais wa Gambia Yahya Jammeh, amesitisha utekelezaji wa adhabu ya kifo kwa wafungwa waliohukumiwa dhabu hiyo.
Ofisi ya
rais huyo imesema hatua hiyo inafuatia wito wa kimataifa uliotaka adhabu
hiyo ikomeshwe lakini ameonya kuwa usitishaji huo ni wa muda.
''Hatua
itakayofuata itatategemeana na iwapo kiwango cha uhalifu kitapungua
ambako usitishaji huo utakuwa wa moja kwa moja, na iwapo uhalifu
utaongezeka basi hukumu hizo zitatekelezwa,'' taarifa ya rais huyo
imesema, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
Kiongozi huyo wa Gambia alikosolewa na jumuiya ya kimataifa mwezi uliopita alipotangaza kutekeleza adhabu ya kifo kwa wafungwa.
Wafungwa
tisa waliuawa kwa kupigwa risasi kufuatia uamuzi wa rais huyo huku
wengine 37 wakibakia katika orodha ya wafungwa waliohukumiwa adhabu ya
kifo.
Rais huyo
alisema kuwa wafungwa wote arobaini na saba waliohukumiwa adhabu ya
kifo wangekuwa wamekwishauawa kufikia katikati ya mwezi Septemba mwaka
huu.
Utekelezaji
huo wa hukumu ya kifo ulikuwa ni wa kwanza nchini Gambia iliyo maarufu
kwa watalii, katika kipindi cha miaka 27, huku wanaharakati wa haki za
binadamu wakisema kuwa wengi wa wafungwa hao ni wale wa kisiasa.
Umoja wa Afrika na mashirika ya kutetea haki za binadamu walipinga adhabu hiyo.
Benin
ambayo ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika ilimtuma waziri wake wa
mambo ya nje kwenda nchini Gambia kumuonya Bwana Jammeh kuacha
kutekeleza adhabu ya kifo kwa wafungwa hao.
Siku ya
Ijumaa kundi la Upinzani la Gambia lilisema kuwa lina mpango wa
kuanzisha serikali likiwa uhamishoni katika nchi jirani ya Senegal
katika kipindi cha siku chache zijazo.
Lengo la
kundi hilo la National Transitional Council of The Gambia (CNTG) ni
kuona linamaliza utawala wa ki-dikteta wa rais Yahya Jammeh.
Hukumu ya
kifo ilifutwa wakati wa utawala wa rais wa zamani wa nchi hiyo Dawda
Jawara lakini ikarejeshwa tena muda mfupi baada ya rais Jammeh kunyakua
madaraka mwaka 1994.
No comments:
Post a Comment