KAMATI ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa,
imewaidhinisha Mbuyu Twite na Kevin Yondan kuchezea Yanga katika
msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, unaoanza mwishoni
mwa wiki.
Habari
kutoka ndani ya kikao cha Kamati hiyo, kilichomalizika hivi karibuni,
zimesema kwamba pamoja na maamuzi hayo, Yanga imepewa siku 21 kulipa
dola 32,000 ambazo Simba SC ilimlipa Twite ili ajiunge nao, lakini baadaye akaghairi na kusaini na kuhamia Yanga.
Uamuzi huu, unafuatia kikao cha pamoja baina ya Simba na Yanga
Jumatatu iliyopita kuvunjika bila kufikia makubaliano kuhusu
mustakabali wa wachezaji hao.
Katika kikao hicho kilichoanza majira ya saa 7:00 mchana, hoja ya
kwanza kuwasilishwa mezani ilikuwa ni suala la beki Twite na upande
wa Yanga uliwakilishwa na Sanga na Katibu, Celestine Mwesigwa wakati
kwa Simba walikuwepo Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’
na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Kapteni wa zamani wa Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ), Zacharia Hans Poppe.
Ikumbukwe,
Simba iliwasilisha malalamiko ya kufanyiwa mchezo usio wa kiungwana na
Yanga kwa Twite. Ilidai Twite alisaini mkataba na klabu yao
Agosti 1, mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la Soka Rwanda
(FERWAFA) na APR na kulipwa dola za Kimarekani 30,000 na nyingine
2,000 za nauli ya kuja Dar es Salaam kujiunga na klabu hiyo. Hata hivyo,
mchezaji huyo akahamia Yanga.
Katika mjadala huo, Simba ilikubali kurudishiwa fedha zao, lakini
viongozi wa Yanga wakasema hawawezi kutoa hadi waombwe radhi na
Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage, ambaye alisema viongozi
wa klabu hiyo yenye maskani yake makutano ya mitaa ya Twiga na
Jangwani wana ‘fedha chafu za EPA’.
Simba wakasema kauli yake ya Rage ilikuwa sehemu ya utani wa jadi,
kama ambavyo Yanga walimvalisha jezi Twite yenye jina la Rage.
Kufikia hapo, Simba wakasema hawawezi hata kujadili suala la Kevin
Yondan na Kamati ya Mgongolwa ikasema itapitia maelezo ya pande zote,
watatoa majibu kwa mujibu wa kanuni na sheria Septemba 10, mwaka
huu, yaani leo.
Katika kesi ya Yondan, walalamikaji ni Simba, ambao wanadai beki huyo
alisaini Yanga akiwa bado ana mkataba na klabu yao.
Awali, Kamati ya Mgongolwa ilikutana Jumapili iliyopita asubuhi hadi
usiku, bila kupata suluhisho la pingamizi hizo na kuamua kutumia
busara ya kuzikutanisha pande zinazopingana kujaribu kupata suluhu
siku iliyofuata.
source bin zubeiry
No comments:
Post a Comment