NIMECHUKUA HATUA YA KUWASILISHA KWA TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA SUALA LA MATATIZO YA MAJI KATIKA KATA YA GOBA ILI HATUA ZA HARAKA NA ZA KUDUMU ZICHUKULIWE
Kazi
ya mbunge ni kuwakilisha wananchi, kushiriki katika kutunga sheria na
kuisimamia serikali ili kuwezesha maendeleo kwa pamoja na mambo mengine
kuhakikisha huduma za kijamii ikiwemo upatikanaji wa maji zinaboreshwa.
Tarehe
10 Oktoba 2012 ikiwa ni sehemu ya kufanya kazi hiyo nimekwenda kwa
niaba ya wananchi Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na
kuwasilisha malalamiko ya uvunjwaji wa haki za binadamu za kupata huduma
ya maji na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora katika uendeshaji wa
miradi ya maji kwenye kata ya Goba katika Manispaa ya Kinondoni.
Tatizo
la maji katika kata ya Goba limedumu sasa kwa kipindi cha miaka mingi
kabla ya mimi kuchaguliwa kuwa mbunge, pamoja na kwamba serikali
inaowajibu wa kuhakikisha inalinda haki ya kupata maji lakini
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imeshindwa kulinda haki hii kwa
wakazi wa Goba.
Ifahamike kuwa miongoni mwa haki za kijamii kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni (“The International Covenant on Economic, Social and Cultural Rights”, ICESCR ) wa 1966 ni pamoja na haki ya kupata maji safi na salama.
Hata
hivyo katika nchi yetu inaonekana haki ya kupata maji safi na salama
haitiliwi mkazo pamoja na Tanzania kutambua na kuridhia mkataba huo
hivyo malalamiko haya ya lengo la kuwezesha tume kusimamia haki za
msingi za binadamu na utawala bora katika sekta ya maji.
Ikumbukwe
kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, toleo la
mwaka 2005 Ibara ya 130 (b) na (c) inaeleza majukumu ya Tume ya Haki za
binadamu na utawala bora kuwa ni pamoja na kupokea malalamiko ya
uvunjaji wa haki za binadamu na kufanya uchunguzi juu ya mambo
yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa utawala bora;
Izingatiwe
kuwa Sheria ya Haki za binadamu na Utawala Bora namba 7 ya mwaka 2001
kifungu cha 22(1) kinaruhusu malalamiko kwa njia ya maandishi ;
Na
Irejewe kuwa kuwa kifungu cha 15(1) (b) (iii) cha Sheria ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora, sheria namba 7 ya mwaka 2001, kinaipa nguvu
Tume kuchunguza uvunjaji wa Haki za Binadamu ikiwa itapokea malalamiko
kutoka kwa mtu anayefanya hivyo kwa niaba ya kundi la watu.
Kwa
kutumia mamlaka na matakwa ya Ibara ya 130 ya Katiba ya Nchi na vifungu
vya 15 na 22 vya Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na utawala bora na
kwa kuzingatia mikataba ya haki za binadamu ambayo nchi yetu imeridhia
nimetaka tume ichukue hatua zifuatazo:
Mosi;
Ichunguze na kuchukua hatua dhidi ya waliohusika katika ukiukwaji wa
haki za binadamu za wananchi kupata huduma ya maji na ukiukwaji wa
misingi ya utawala bora kwa kushindwa kushughulikia matatizo ya kimfumo
kuhusu uendeshaji wa miradi ya maji, kutokutekelezwa kwa wakati kwa
vipaumbele vya maji kwa mujibu wa bajeti iliyopitishwa na tuhuma za
ufisadi, uzembe na udhaifu wa kiutendaji katika kamati za maji, ngazi ya
kata na kwenye idara ya maji ya Manispaa ya Kinondoni.
Pili;
Pamoja na kuchukua hatua kwa wahusika waliosababisha uvunjaji wa haki
ya msingi ya wananchi kupata huduma ya maji na ukiukwaji wa haki za
binadamu; Tume ya Haki za Binadamu ipendekeze hatua za haraka
zinazopaswa kuchukuliwa na Manispaa ya Kinondoni kuwezesha huduma ya
maji kurejea kwa wananchi, kupanua kwa dharura wigo wa upatikanaji wa
maji kwa wananchi wa Kata ya Goba pamoja na kuboresha mfumo mzima wa
upangaji, utekelezaji na usimamizi wa miradi ya maji katika Manispaa ya
Kinondoni.
Tatu;
Aidha, zaidi ya hatua za dharura Tume ya Haki za Binadamu ipendekeze
hatua za ziada ya kuchuliwa na Manispaa ya Kinondoni kuwezesha kata ya
Goba itoke katika kupatiwa huduma ya maji chini ya Manispaa ya Kinondoni
na badala yake ihudumiwe na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es
salaam (DAWASA) pamoja na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es
Salaam (DAWASCO) ili kuwezesha uboreshaji mpana wa miundombinu kwa ajili
ya ufumbuzi wa kudumu.
Nne,
Tume ichunguze na kupendekeza masuala mengine ya kushughulikiwa na
mamlaka zingine zinazohusika ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na
Maji (EWURA), Wizara ya Maji na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhusu
masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu na uvunjwaji wa misingi ya
utawala bora katika miradi ya maji kwenye kata ya Goba pamoja mfumo wa
upatikanaji wa maji kwa ujumla.
Wenu katika kuwakilisha wananchi,
John Mnyika (Mb)
12/10/2012
No comments:
Post a Comment