Pamoja
na mambo mengine aelekeze kamati hiyo kupokea na kujadili Taarifa ya
Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge ya mwaka 2011 kuhusu Sekta Ndogo ya
Gesi Asili ikiwemo juu ya hatua iliyofikiwa katika kushughulikia tuhuma
za ufisadi, madai ya mapunjo ya fedha za mauzo ya Gesi asili na hatua
iliyofikiwa katika maandalizi ya sera, mpango mkakati na sheria ya gesi
asili.
Hatua
hii ni muhimu kufuatia ukimya wa Waziri wa Nishati na Madini Prof.
Sospeter Muhongo kuhusu kauli yangu ya tarehe 4 Oktoba 2012 ya kutaka
Taarifa ya ufafanuzi kuhusu utafutaji wa mafuta na gesi asili nchini
iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini tarehe 21 Septemba 2012
ifutwe kwa kuwa italinda ufisadi na kukwaza utetezi wa rasilimali za
taifa.
Taarifa
hiyo ya Wizara ya Nishati na Madini ilieleza kuwa maandalizi ya sera ya
gesi asili yapo katika hatua za mwisho wakati ambapo kamati mbalimbali
za kudumu za Bunge hazijahusishwa katika mchakato huo muhimu pamoja na
kuwa mamlaka ya kutunga sera kwa mfumo wetu wa sasa ni ya Baraza la
Mawaziri hata hivyo kwa unyeti na upekee wake sera ya gesi Spika wa
Bunge anapaswa kuwezesha Kamati za Kudumu za Bunge zihusishwe ili pawepo
mashauriano na maridhiano kwa mapana na marefu.
Taarifa
hiyo ya Wizara ya Nishati na Madini ilieleza kuwa mikataba 26 ya TPDC
ni sehemu ya nyaraka muhimu za kuboresha utayarishaji wa sera ya gesi
asili, hata hivyo mikataba hiyo imeendelea kuwa siri hivyo Spika
aingilie kati kuziwezesha Kamati za Kudumu za Bunge kuisimamia serikali
kurekebisha mikataba ya sasa na kuboresha mikataba ijayo kwa Serikali
kutekeleza mwito wangu wa toka mwaka 2011 wa kutaka mikataba hiyo
iwasilishwe bungeni na iwekwe wazi kwa umma.
Izingatiwe
kwamba katika Mkutano wa Nane wa Bunge Spika alitangaza kuwa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imevunjwa na kwamba majukumu
yaliyokuwa yakishughulikiwa na kamati hiyo yatashughulikiwa na kamati
nyingine kwa mujibu wa madaraka na mamlaka ya Spika.
Irejewe
kwamba kwa mujibu wa Kanuni ya 116 na Kanuni ya 114 fasili ya 14 Spika
ana mamlaka na madaraka ya kukabidhi mambo mengine yashughulikiwe na
Kamati ya Kudumu ya Bunge nyingine kama atakayoelekeza.
Ikumbukwe
kuwa Julai 2011 na Julai 2012 kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa
Nishati na Madini na kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani nilieleza
namna nchi yetu ilivyojaliwa utajiri wa gesi asilia katikati ya lindi la
umasikini wa wananchi na kwamba taifa letu lina fursa ya kuwa nchi
kiongozi katika gesi Afrika na kushindana kimataifa ikiwa tutaweka
mstari wa mbele upeo, umakini na uadilifu katika sekta ya nishati
kuepusha laana ya rasilimali.
Hata
hivyo, mapitio ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2011/2012 yanaonyesha
bado serikali haichukui hatua thabiti kushughulikia ufisadi na udhaifu
wa kiuongozi katika sekta ndogo ya gesi asili hivyo hatua za haraka
zisipochukuliwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 na kuendelea
rasilimali inaweza kuwa chanzo cha migogoro na kuhatarisha pia usalama
wa nchi.
Kwa
niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani nilieleza bungeni tarehe 15 Julai 2011
kuhusu tuhuma za ufisadi na ukiukwaji wa mikataba katika sekta ndogo ya
gesi inaoihusu pia Kampuni ya Pan African Energy Tanzania (PAT) na
kutaka kuundwa kwa kamati teule ya bunge kuchunguza suala hilo.
Badala
yake Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini uliunda kamati
ndogo ya iliyofanya uchunguzi uchunguzi wa masuala husika na taarifa
kuwasilishwa bungeni mwaka 2011 ; hata hivyo mpaka sasa maamizio ya
bunge kufuatia taarifa hiyo hayajatekelezwa kwa ukamilifu.
Tarehe
27 Julai 2012 kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani niliitaka Serikali
kueleza ni kwanini mpaka sasa kiasi cha dola milioni 20.1 zilizopunjwa
kifisadi hazijareshwa na kuitaka serikali iache kutumia kisingizio cha
kuundwa kwa Timu ya Majadiliano (GNT) kuchelewesha utekelezaji wa
maazimio, suala ambalo Wizara ya Nishati na Madini itapaswa kueleza
hatua iliyofikiwa iwapo Spika atazingatia mwito huu na kuchukua hatua za
haraka.
Ifahamike
pia kwamba mwaka 2011 kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na
Madini niliitaka serikali ambazo kuweka wazi bungeni na kwa umma
mikataba ya madini, mafuta na gesi asili katika nchini ili kuongeza
tija na uwajibikaji.
Aidha
nilitoa mwito mwito kwa wananchi na wabunge kuongoza marekebisho ya
kikatiba na kisheria ili kuweka vifungu vya kulazimisha uwazi katika
mikataba katika hizo muhimu kwa uchumi na usalama wa nchi.
Uwazi
katika mikataba utadhibiti pia mianya ya ufisadi miongoni mwa baadhi ya
watendaji wa serikali kwa kuwa mikataba hiyo itajadiliwa na umma na
hivyo kupunguza uwezekano wa viongozi kutanguliza maslahi binafsi na
kuwa na mikataba bora ya baadaye yenye kuzingatia maslahi ya umma.
Usiri
katika mikataba ni tatizo kwa sababu masharti kama ya kushughulikia
madhara ya kimazingira na kuchangia katika huduma za jamii pamoja na
kulipa kodi zinazokusudiwa yanaweza yasitekelezwe kwa ukamilifu kama
hayatafahamika kwa wabunge na umma. Aidha, ipo mikataba yenye vifungu
ambavyo vinakinzana na sheria nyingine ama vinalinda kupindukia
makampuni dhidi ya sheria nyingine za nchi zinazotungwa masuala ambayo
yanaingilia mamlaka ya bunge ya kutunga sheria na kuisimamia serikali.
Sheria
mpya ya madini Tanzania ya mwaka 2010 ina kifungu kinachotaka uwazi
hata hivyo kimejikita katika uwazi wa rekodi na ripoti hakijaweka bayana
mfumo wa uwazi katika mikataba ya madini, sheria ya mafuta nayo haina
kifungu cha uwazi katika mikataba na sheria ya gesi haipo kabisa; hali
ambayo inahitaji kurekebishwa.
Pamoja
na mapato uwazi katika mikataba utachangia katika kupata tija ya ziada
katika uchimbaji kwa kulinda maslahi ya wafanyakazi na kuweka mfumo
mzuri zaidi wa makampuni kununua bidhaa za ndani kwa majibu wa vifungu
vya mikataba hali ambacho itawezesha rasilimali kunufaisha wananchi
wengi zaidi.
Uwazi
katika mikataba utawezesha wabunge na wadau wengine kusimamia ipasavyo
taasisi za kiserikali kuhusu mifumo ya kifedha na kibenki ambayo
itaongeza mchango wa sekta za nishati na madini katika kuimarisha
uchumi kwa kudhibiti mfumuko wa bei na kuporomoka kwa sarafu wakati huu
ambapo thamani ya mauzo imeongezeka duniani lakini mzunguko umejitika
katika masoko na mabenki ya nje. Kwa ujumla, uwazi katika mikataba
utapanua pia uwajibikaji wa kuongeza umiliki wa nchi na wananchi wa
michakato ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asili.
Pamoja
na kuwa ibara ya nne ya katiba inasema kwamba rasilimali na mali asili
zote ziko chini ya usimamizi wa serikali; na ibara ya 63 inaeleza kwamba
bunge ndicho chombo kikuu cha kuisimamia serikali kwa kutunga sheria na
kupitisha mipango, katiba haijalazimisha mikataba ya madini, mafuta na
gesi kuridhiwa na bunge hivyo katika kipindi cha sasa mikataba hiyo
iwasilishwe kwa rejea na mapitio.
Katika
muktadha huo, tarehe 4 Oktoba 2012 nilimtaka Waziri wa Nishati na
Madini Prof. Sospeter Muhongo afute taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu
wa wizara hiyo kuwa lengo la agizo lake la kupitiwa kwa mikataba yote 26
ya utafutaji mafuta na gesi asili ni “kuhakikisha kwamba endapo kuna
mapungufu katika mikataba hiyo, mapungufu hayo yasijirudie tena katika
mikataba mipya ya baadaye” kwa kuwa ikiachwa ilivyo italinda ufisadi na
kukwaza utetezi wa rasilimali za taifa.
Nilieleza
kwamba ufafanuzi uliotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini unatoa mwanya kwa mikataba mibovu kulindwa wakati ambapo kuna
madai tuliyotoa toka mwaka 2011 kwamba baadhi ya mikataba hiyo imeingiwa
kifisadi na mwaka huu wa 2012 zimeibuka tuhuma za vigogo wa serikali
kuingiziwa fedha kifisadi katika akaunti zao za nchini Uswisi na
makampuni ya nje ya utafutaji mafuta na gesi asili.
Aidha,
pamoja Serikali kuwasilisha bungeni mikataba inapaswa pia kuwasilisha
mipango kabambe (master plan) ya mafuta na gesi asili yenye kuzingatia
mabadiliko ya kisera na kimfumo yenye kuwezesha nchi na wananchi
kunufaika na rasilimali husika.
Kauli
hii nimeitoa leo tarehe 14 Oktoba 2012 ikiwa ni Siku ya Kumbukumbu ya
Hayati Julius Nyerere ambaye alipinga ufisadi na kutaka rasilimali za
nchi zitumike kwa manufaa ya maisha ya wananchi:
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
No comments:
Post a Comment