Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, October 16, 2012

Wanaswa na kompyuta, meza za kanisa Mbagala



Pamela Chilongola
WATU wanne zaidi wamekamatwa na polisi wakiwa na kompyuta na meza zilizoporwa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mbagala, Dar es Salaam.Kukamatwa kwa watu hao kunafanya idadi ya waliokamatwa kutokana na vurugu zilizotokea Ijumaa wiki iliyopita kufikia 126.
Vurugu hizo zilisababishwa na watu wanaodaiwa kuwa waumini wa dini ya Kiislamu kuvamia Kituo cha Polisi Maturubai wakitaka wapewe mtoto aliyedaiwa kudhalilisha kitabu kitakatifu cha Quran kwa kukojolea.
Mtoto huyo wa miaka 14, anadaiwa kukojolea Msahafu alipokuwa akibishana na mwenzake kuwa endapo angefanya kitendo hicho, angegeuka nyoka.
Vurugu hizo zilisambaa kwa baadhi ya watu kuharibu mali, kupora na kuchoma moto baadhi ya makanisa na kuharibu magari.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, David Misime alisema jana kwamba watu hao wanne wamekamatwa wakiwa na seti ya kompyuta na meza za kanisani zilizoibwa katika Kanisa hilo la KKKT... “Wamefikishwa katika Kituo kidogo cha Polisi Maturubai.”
Kamanda Misime alisema watu hao wameunganishwa na wengine 122 waliokamatwa awali wakihusishwa na vurugu hizo kati yao, 36 wakituhumiwa kuchoma makanisa wakati 86 walikamatwa kwa kosa la kufanya fujo.
Alipotembelea makanisa yaliyoharibiwa na juzi akizungumza katika kilele cha kumbukumbu ya miaka 13 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rais Jakaya Kikwete aliagiza hatua kali zichukuliwe kwa wote waliohusika na uharibifu huo.
Rais pia alionya tabia ya wananchi kuchukua hatua kwa jazba na kwamba hali hiyo ikiachwa amani inaweza kutoweka.
Aliwataka Watanzania kutafakari kabla ya kuchukua uamuzi wa kufanya ghasia au uharibifu.
Viongozi wa Taasisi za kidini, wanasiasa na watu wa kada mbalimbali walilaani vurugu hizo wakisema hazikuwa na tija.
Katika vurugu hizo, makanisa yaliyoharibiwa ni la Katoliki la Kristo Mfalme la Mbagala Rangi Tatu, Anglikana ambalo lipo Mbagala Kizuiani, Agape lililopo Kibonde Maji, Wasabato la Kizuiani, KKKT Ushirika wa Mbagala na TAG Shimo la Mchanga.
Kamanda Misime alisema kuwa ofisi yake ilikuwa ikiandaa hati za mashtaka na kuanzia leo wahusika wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.
“Tulikuwa katika mkutano wa kuwaandalia kila mmoja hati yake ya mashtaka na wakati wowote kuanzia kesho (leo) tutawafikisha mahakamani kujibu mashtaka yao,” alisema Kamanda Misime.

No comments:

Post a Comment