Nahodha
wa klabu ya Simba Juma Kaseja akibubujikwa na machozi huku Daniel
Akuffo akimsihi aliendelee kulia baada ya klabu yake kutandikwa bao 2-0
na Mtibwa Suagar ya Manungu Turiani Morogoro katika mchezo wa Ligi kuu
ya Vodacom Tanzania bara juzi uwanja wa Jamhuri mkoani hapa.
MPASUKO,
mgawanyiko, msambaratiko hayo ni baadhi ya maneno unayoweza kuyatumia
katika kuelezea hali ya sasa iliyoizunguka klabu ya Simba.
Mabingwa
hao watetezi mwishoni mwa wiki iliyopita walipoteza uongozi wao wa Ligi
Kuu kwa watani zao Yanga baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka
kwa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Kabla
ya kipigo hicho cha Jumapili, Simba tayari ilishatoa sare mara tano
mfululizo dhidi ya Yanga 1-1, Coastal Union, Mgambo Shooting 0-0, Kagera
Sugar 2-2 na Polisi Moro 1-1 matokeo yaliyosababisha uongozi wake
kumsimamisha Haruna Moshi na kumpeleka timu ya vijana beki Juma Nyoso.
Katika
mechi ya Simba dhidi ya Mtibwa, wakati wa mapumziko kipa Juma Kaseja na
mshambuliaji Emmanuel Okwi walitaka kupigana kabla ya kuamuliwa, lakini
hiyo yote ilitokana na Mganda huyo kumlaumu Kaseja kuwa ndiyo chanzo
cha kusababisha Simba kufungwa na Mtibwa kwa kusababisha bao la kwanza.
Bao
lililozua tafrani hiyo lilikuwa ambalo Kaseja alipangua shuti la
Vincent Barbanas na mpira kumkuta mshambuliaji Mohamed Mkopi
aliyeukwamisha wavuni mpira huo kirahisi.
Hata
hivyo habari ambazo Mwananchi limezipata baada ya mechi hiyo ya Simba
dhidi ya Mtibwa zinadai sababu kubwa ya Simba kufanya vibaya ni kutokana
na ushindani uliopo kati ya Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange
'Kaburu' na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hanspope.
"Wachezaji
na viongozi wa Simba wamegawanyika kwenye makundi mawili kuna wale
waliokuwa upande wa Kaburu na wale ambao wapo kwa kundi la Friends of
Simba linaloongozwa na Hanspope," kilidai chanzo hicho.
Chanzo
hicho cha habari kilisema,"uhasama kati ya pande hizi mbili ulianza
baada ya Kaburu kukubali Kelvin Yondani auzwe Yanga pamoja na kufanya
usajili wa wachezaji wa kigeni ambao wengi walikuwa mzigo kwa Simba hali
iliyosababisha Kaburu kunyang'anywa mamlaka ya kusajili wachezaji na
Hanspope kuchukua jukumu hilo."
Chanzo
hicho cha habari kinadai kuwa baada ya Hanspope kuchukua jukumu la
kusajili wachezaji alisajili, ambapo anataka wachezaji wake wapangwe
kwenye mechi na Kaburu anataka wachezaji wake wapangwe hali inayofanya
hiongozi hao watofautiane na timu ifanye vibaya.
Akilizungumzia
sakata hilo, Hanspope ambaye pia ni Mwenyekiti wa ëFriends of
Simbaíaliyechaguliwa Agosti 24, alisema,"sina tofauti yoyote na Kaburu,
mimi ni mwenyekiti wa kamati ya usajili yeye ni makamu mwenyekiti,
hatuingiliani kabisa katika mgawanyo wa kazi zetu sasa tutofautine kwa
lipi?."
Alisema,"wanachosema
wanachama ni hisia tu hakuna tofauti yoyote na hata kama tuna tofauti
inahusiana nini na matokeo?, ninachowaomba watulie tumalize mzunguko wa
kwanza salama tuangalie wapi tulipokosea tujipange upya."
Hanspope
alisema, "matokeo mabovu ni suala la kiufundi zaidi na kocha ndiyo
anahusika kupanga wachezaji ambao hawana viwango, ukimshauri wachezaji
wa kupanga yeye hafuati ushauri anaamua anavyojua yeye matokeo yake
ndiyo haya.
Akimzungumzia
mshambuliaji Daniel Akuffo, Hanspope alisema,"Akuffo ukiniuliza
anafanya nini mimi sijui, hafungi magoli, ukimwambia mwalimu yupo Edward
Christopher mpange, yeye anamng'ang'ania Akuffo wake hilo ndiyo
tatizo."
Aidha
Hanspope alisema,ìFriends of Simba, tunachokifanya lazima kiendane na
tafsiri ya neno lenyewe na isije ikawa tofauti, kuwa ni maadui wa Simba,
naomba ushirikiano wa pamoja wa wanasimba kuhakikisha tunafanikisha
malengo yetu.î
Naye
Kaburu akilizungumzia sakata hilo alisema hana matatizo yoyote na
Hanspope na watu wanaosema hivyo hawajui lolote kwani wao ni viongozi
wawili wenye majukumu tofauti.
"Simba
haiongozwi na mtu mmoja ina mwenyekiti na mimi ni msaidizi wake, kuna
kamati ya usajili, mashindano, ufundi, kila mtu anatekeleza wajibu wake,
kutofanya vizuri kwenye timu kama viongozi tunasikitika, kufukuzana
siyo dawa na wala hatujengi, tunatakiwa kukaa chini na kuangalia ni
wapi tumekosea tujirekebishe,"alisema Kaburu.
Alisema,"ninachoona
ni tatizo la ufundi, mwalimu alitakiwa kubuni fomeshini ya kukabiliana
na viwanja vibovu, kushutumu wachezaji wamechukua rushwa au viongozi
wanahujumu timu siyo kitu kizuri ni kitu kibaya sana, kwani wachezaji
hawa hawa na mwalimu huyu huyu ndiyo waliochukua ubingwa mwaka jana, pia
mwaka huu wamechukua mataji manne tofauti tofauti."
WANACHAMA WAVAMIA KLABUNI
Baadhi
ya wanachama wa Simba jana walifanya maandamano makubwa makao makuu ya
klabu hiyo kwenye mtaa wa Msimbazi kushinikiza viongozi wao wajiuzulu
kwa madai kuwa wameshindwa kuongoza timu.
Wanachama
hao walikuwa na mabango yaliyobeba ujumbe tofauti tofauti ukiwashutumu
Rage, Kaburu na Kaseja waachie ngazi kwa kile walichodai kuwa wanahujumu
timu yao.
Baadhi
ya mabango hayo yalisomeka,"Mheshimiwa Rage una kazi nyingi tuachie
Simba yetu...."Wachezaji acheni kuidhalilisha Simba kwa pesa za mafisadi
...."Kocha wetu Milovan bado tunamuhitaji mchango wake
mkubwa...."Kaburu ulitaka kumuuza Okwi sasa unamtumia
kuhujumu...."Kaburu, Kaseja achieni ngazi.....".
Akizungumza
kwa hisia mwanachama Said Moscow kadi namba 250 alisema huku
akishangiliwa na kundi kubwa la wanachama,"viongozi ndiyo wanachangia
matokeo mabovu, wenyewe kwa wenyewe hawaelewani, wanaweka matabaka kwa
wachezaji, wameshindwa kuongoza timu, bora waachie ngazi."
"Kaburu
asikwepe lawama za matokeo mabovu yeye ni kiongozi amekuwa akiuza
wachezaji, Kaseja naye ana dhambi zake umri umeenda, kiwango kimeshuka
bado anang'ang'ania anang'ang'ania kitu gani?, Kaseja kachoka atafutwe
kipa mwingine, tutafanya mkutano wa wanachama kwa mujibu wa katiba yetu
wanachama 500 tunataka viongozi wajiuzulu,"alisema Moscow.
Naye
mwanachama Mgeni Ramadhani maarufu kwa jina la 'Macho' aliongea kwa
hasira akisema," Yondani kauzwa Yanga, Okwi naye alitaka kuuzwa Yanga,
Kaburu ndiyo tatizo, Hayati mwalimu Nyerere alisema kiongozi anayeingia
madarakani kwa fedha huyo hatufai."
Alisema,"tunampa
siku mbili atangaze kwa hiyari yake kujiuzulu la sivyo tutaandamana
mpaka nyumbani kwake Mbezi anapoishi tunapajua."
Akizungumzia
suala la mashabiki kuandamana hadi nyumbani kwake kushinikiza ajiuzulu,
Kaburu alisema,"ninachowaomba wanachama watulie katika kipindi hiki,
wasubiri tumalize mchezo wetu wa mwisho na Toto, kuna likizo ndefu
tutakaa na kuangalia cha kufanya, kuandamana hadi nyumbani kwangu siyo
dawa, atakayefanya hivyo nitamchukulia kama mhalifu na nitamchukulia
hatua, kufungwa mechi moja siyo tatizo, Yanga wamepoteza mechi mbili
mbona hawajaandamana?, kuna watu wana chokochoko walikuwa wanasubiri
timu ifanye vibaya wapate cha kusema."
No comments:
Post a Comment