RAILA
ODINGA NA UHURU KENYATTA, WAGOMBEA WA KITI CHA URAIS WANAPEWA NAFASI
KUBWA YA KUINGIA IKULU YA KENYE KATIKA UCHAGUZI MKUU UNAOFANYIKA LEO
NCHINI HUMO.
WANANCHI wa Kenya leo wanapiga kura
kuwachagua viongozi wao katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza baada ya kupata
Katiba Mpya, ambao unawapambanisha vikali watoto wa waasisi wa taifa
hilo ambao sasa ni marehemu.
Uchaguzi
wa leo unaelezwa kuwa na kinyang’anyiro kikali ambacho hakijawahi
kushuhudiwa baina ya wagombea wawili wa urais, Uhuru Kenyatta wa
Muungano wa Jubilee na Raila Odinga wa Cord.
Uhuru ni
mtoto wa Rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta wakati Raila ni
mtoto wa aliyekuwa makamu wa Kenyatta, Jaramog Oginga Odinga.
Mbali na
wagombea hao wenye matumaini ya kuingia Ikulu kila mmoja, wapo wengine
sita – Musalia Mudavadi (UDF), Peter Kenneth (Eagle Alliance), Martha
Karua (Narc), Mohammed Abduba Dida (ARK), Prof James ole Kiyiapi (RBK)
na Paul Muite wa Safina.
Wapiga kura wameombwa kudumisha amani
Wagombea
wote walihitimisha kampeni zao Jumamosi na jana hakukuwa na kampeni kwa
mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Kenya. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka
ya Kenya (IEBC), imesema maandalizi yote yamekamilika na vifaa vyote vya
kupigia kura vimeshafika katika maeneo husika.
Mwenyekiti
wa IEBC, Ahmed Hassan alisema katika taarifa yake jana kuwa vituo
vitafunguliwa saa 12:00 asubuhi na kufungwa saa 1:00 jioni, lakini kama
kutakuwa na wapigakura kwenye foleni wataendelea hadi watakapokuwa
wamemaliza kupiga kura.
Kwa mujibu wa Hassan, kura zote zitahesabiwa vituoni na matokeo kutumwa kwa njia ya simu.
Kwenye kampeni zao za lala salama wagombea
wenye nguvu, Odinga na Kenyatta, wamewahamasisha wapigakura kujitokeza
kwa wingi na kuwachagua, ili waweze kushinda katika raundi ya kwanza.
Waangalizi wa kimataifa nchini humo wameridhika na maandalizi ya shughuli hiyo.
Msukumo
huo unatokana na uwezekano wa kura kupigwa kwa raundi ya pili Aprili 10,
kutokana na uwezekano wa wagombea wote wanane kushindwa kufikisha nusu
ya kura zote, kwa mujibu wa kura za maoni zilizofanyika awali.
Wakati
uchaguzi wa leo umeigharimu Serikali Sh24.9 bilioni (Sh473.1 bilioni za
Tanzania), ule wa marudio unakadiriwa kugharimu Sh11.2 bilioni (sawa na
Sh212.8 bilioni).
Asemavyo Uhuru
Mosi, nina matumaini kuwa kazi niliyofanya
mimi na washirika wangu katika Muungano wa Jubilee, wafanyakazi makini
wa chama changu cha TNA na maelfu ya wafuasi wangu, italipa.
Pili,
ninatamani uchaguzi wa amani na matumaini haya yanazidi hata furaha ya
ushindi wa Jubilee. Sitaki tena Kenya irejee katika matukio ya 2007/8.
No comments:
Post a Comment