Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, April 4, 2013

Chadema wamtuhumu Mwakyembe kutoa zabuni kinyume cha sheria



Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemtuhumu Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe kwamba alitoa zabuni ya ujenzi wa bandari ya nchikavu kwa kampuni inayomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinyume cha sheria za ununuzi. Chadema walisema jana kwamba, kampuni hiyo ni Jitegemee Trading Company ambayo ilipewa zabuni ya ujenzi wa bandari katika Viwanja vya Sukita pasipokuwa na mchakato wa kushindanisha kampuni nyingine. 
Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila alisema: “Mwakyembe aseme alitoa zabuni hiyo kwa Jitegemee kwa kuzingatia vigezo gani? Kampuni ngapi zilishindanishwa katika mchakato huo na asipofanya hivyo hastahili kukaa wizarani hapo bali alipelekwa Segerea gerezani kwani ni kosa kubwa kutoa zabuni kinyemela.”
Hata hivyo, Dk Mwakyembe, ambaye yuko jimboni kwake Kyela mkoani Mbeya alipoulizwa kuhusu madai hayo alijibu na kukata simu; “Mimi nina kazi ya kuongoza wizara na wao Chadema wana kazi ya kuchonga mdomo, hivyo waache mimi niongoze Serikali.”
Kigaila alituhumu mradi huo ulitakiwa kujengwa ndani ya Halmashauri ya Temeke, lakini katika hali ya kushangaza CCM waliamua kuhamishia Bonde la Msimbazi.
“Kampuni hiyo tayari imetengewa Sh10 bilioni katika bajeti ya 2013/14 itakayosomwa bungeni, itakuaje Serikali inawafukuza watu kuishi mabondeni, lakini wao wanapeleka mradi huo bondeni?
“Hizo zote ni njama za CCM kujikusanyia fedha kwa ajili ya kampeni za uchaguzi wa 2015,” alisema Kigaila.

No comments:

Post a Comment