Mkurugenzi
wa Mashtaka (DPP) Zanzibar, Ibrahim Mzee Ibrahim, ametupilia mbali
uchunguzi wa mauaji ya Padri Evarist Mushi uliofanywa na Jeshi la Polisi
kwa kushirikiana na Maafisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI)
na kusema mtuhumiwa hana kesi ya kujibu mahakamani.
Padri
Mushi ambaye alikuwa Paroko wa Kanisa Katoliki Minara Miwili aliuawa kwa
kupigwa risasi Febuari 17, mwaka huu katika eneo la Beitrasi mjini hapa
akiwa ndani ya gari alipokuwa akielekea kuongoza misa ya Jumapili
katika Kanisa la Mtakatifu Theresia, mjini Zanzibar.
Baada ya
mauaji hayo, Rais Jakaya Kikwete alitoa kibali cha kukaribisha maafisa
wa FBI kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa mauaji hayo
na Machi 17, mwaka huu Jeshi la Polisi lilimkamata Omar Mussa Makame kwa
tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Uchunguzi
wa NIPASHE umebaini kuwa DPP baada ya kulipitia jalada la uchunguzi wa
mauaji hayo, juzi alitoa mwongozo kwa Jeshi la Polisi kuendelea
kumtafuta muuaji wa Padri Mushi.
Kwa
mujibu wa uchunguzi huo, DPP aliliandikia barua Jeshi la Polisi na
kukabidhiwa juzi ikieleza sababu za ofisi yake kutofungua hati ya
mashtaka hadi sasa dhidi ya mtuhumiwa wa mauaji hayo.
Jeshi la
Polisi limethibitisha kuipokea barua ya DPP ambayo inaeleza kuwa
ushahidi uliokusanywa katika jalada la kesi hiyo hauna mashiko na kwamba
mtuhumiwa hahusiki na mauaji hayo.
Chanzo
cha habari kutoka Jeshi la Polisi kilieleza kuwa DPP hajaridhishwa na
uchunguzi wote uliokusanywa dhidi ya mtuhumiwa pamoja na watuhumiwa
watatu wanaotuhumiwa kwa mauaji ya askari polisi, Said Abdulrahman
aliyeuawa kwa kupigwa mapanga na watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa
Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar Oktoba 17, mwaka
jana.
Kamishna
wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alithibitisha hatua ya
DPP kutupa uchunguzi wote wa jalada la mauaji ya Padri Mushi na kuwataka
waandishi wa habari kumtafuta DPP azungumzie sababu za uamuzi wake wa
kutokubaliana na uchunguzi wa Polisi.
No comments:
Post a Comment