Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo akiwaonesha waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, nakala ya gazeti la Mwanachi lililoandika habari kuhusu msimamo wa Kanisa juu ya suala la serikali tatu. Picha na Venance Nestory.
Dar es Salaam/Iringa. Siku mbili baada ya Tume ya Haki na Amani ya Baraza la MaaskofuTanzania (TEC) kutoa waraka wa kulitaka Bunge Maalumu la Katiba kutopuuza mapendekezo ya muundo wa serikali tatu, Askofu Mkuu wa Jimbo Mkuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameibuka na kusema msimamo huo siyo wa Kanisa Katoliki nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kardinali Pengo pamoja na kukiri kuwa tume ilitoa maoni hayo, alikanusha kuwa taarifa zilizotolewa na moja ya magazeti kuwa msimamo wa Kanisa Katoliki ni serikali tatu.
"Maoni ya Tume hayawezi kuwa ni msimamo wa kanisa. Kanisa Katoliki lina utaratibu wa kutoa misimamo yake na huwa inatolewa na Mwenyekiti wa TEC," alisema.
Hata hivyo, Rais wa TEC, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa kutoka Jimbo la Iringa, alisema jana kuwa alikuwa na shughuli nyingi, hivyo asingeweza kuzungumzia suala hilo, labda wiki ijayo.
Akizungumza katika makazi yake mjini Iringa, Askofu Ngalalekumtwa alisema: "Mniache, nina shughuli nyingi...labda mnitafute wiki ijayo," alisema.
Vilevile, Pengo ambaye alirejea msimamo wake binafsi wa kuunga mkono Muungano wa serikali mbili, alisema kwa namna Rasimu ya Katiba ilivyo, hakuna kigezo cha kulazimisha Kanisa Katoliki litoe msimamo.
Alisema Kanisa Katoliki lingeweza kutoa msimamo iwapo Rasimu ya Katiba ingekuwa na dosari zinazohusu imani au maadili.
"Kwa mfano, (Rasimu) ingekuwa inasema, hakuna Mungu lazima tungekuja juu kwa sababu inaingilia imani yetu," alisema Kardinali Pengo na kufafanua:
"Vilevile tungeweza kusema inakwenda kinyume na maadili iwapo inaruhusu kuua wazee au inaunga mkono ndoa za jinsi moja."
Tamko la Tume
Tamko la tume hiyo inayoongozwa na Askofu Mkuu wa Tabora, Paulo Ruzoka liliweka bayana kuwa muundo wa serikali mbili haukutatua matatizo ya msingi na badala yake ulilimbikiza kero zilizosababishaZanzibar kujiundia katiba yake mwaka 2010 bila kushauriana na Tanzania Bara.
Tamko hilo la kurasa 15 lililosambazwa kwa baadhi ya Wajumbe wa Bunge la Katiba, lilitolewa baada ya mkutano wa kitaifa wa Wajumbe wa Kamati za Majimbo za Haki na Amani za Kanisa hilo na Chama cha Wanataaluma Wakatoliki Tanzania (CPT), uliofanyika jijini Dar es Salaam Februari 5 na 6 mwaka huu.
Msimamo binafsi.
Kardinali Pengo alisema katika misimamo ya kisiasa ndani ya Kanisa Katoliki, waumini wanatofautiana bila kuzingatia ni kiongozi au muumini wa kawaida na hakuna sababu ya kulazimishwa kuwa na msimamo unaofanana.
Alisema yeye anaona serikali mbili zinaweza kusaidia zaidi katika usalama wa nchi na kujenga umoja hasa katika kuzuia watu wa nje wenye nia mbaya kupenya nchini ili kuanzisha chokochoko za uvunjifu wa amani.
Alisema ana wasiwasi mfumo wa Serikali tatu utatoa mwanya kwa maadui kupenya Zanzibarna hata kuingia Tanzania Bara.
Alitoa mfano wa nchi jirani ya Kenya, ambako matukio kadhaa makubwa ya kigaidi yametokea na kuonya kuwa kamwe asingependea kuona yanafanyika hapa nchini.
Kura ya siri
Akizungumzia mvutano wa mfumo wa upigani kura kwenye Bunge la Katiba, Pengo alisema: "Kura ya siri ndiyo njia pekee ya kutenda haki katika kupitisha vifungu kwenye Bunge linaloendelea mjini Dodoma."
Chanzo, mwananchi
No comments:
Post a Comment