Pichani ni waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakiwa katika maandamano ya amani (Picha na Maktaba).
---
Watu
wengi kwa sasa wameibuka na kutokea kuipenda fani ya uandishi wa habari
bila kujua misingi na miiko ya uandishi wa habari. Tatizo moja ambalo
limeonekana ni kubwa sana ni utandawazi ambao umekuwepo na kutokea ibuko
la kila kijana kufungua gazeti tando (blog).
Hatukatai
kuja kwa magazeti tando ila naomba tujiulize, yanatumika ipasavyo ama
ndiyo limekuwa ni wimbi vamizi lenye kutoa ama kusambaza habari hata
zile zisizokuwa na vyanzo kamili na visivyojitosheleza.Kwa sasa imezuka
tabia ya wanaojiita wamiliki wa magazeti tando,wengi wao kukopi na
kupaste vitu wanavyoviokota katika mitandao ya kijamii ikiwemo Twitter,
facebook na mingine mingi.
Sina
nia ya kumsema mtu bali napenda tuelimishane kama vijana wenzangu,ambao
wametokea kuipenda fani ya uandishi wa habari, wakumbuke kuwa fani ya
uandishi wa habari ina miiko na maadili yake, mfano. Katika kuandika
habari za mazingira, siasa, elimu, uchumi, michezo, burudani ukiangalia
habari hizi zote zina misingi na miiko yake. Leo hauwezi kumchukua
mwandishi wa habari za michezo ukamwambia aandike habari za uchumi kwa
vile hatakuwa na takwimu za uchumi na hata akiandika hiyo habari na
kuisoma utakuwa unajiuliza maswali mengi bila kupata majibu.
Vile
vile ni vizuri vijana wenzangu kutambua kuwa kila kazi ina mipaka na
misingi yake, juzi juzi nilisoma habari katika gazeti tando moja wapo
ikisema, 'ALIYEONGOZA MAANDAMANO YA IRINGA MHESHIMIWA MCHUNGAJI MSIGWA
ASWEKWA NDANI' nilijiuliza maswali mengi ambayo kiukweli nilikosa majibu
yake, kuona huyu aliyeandika hiki kichwa cha habari kweli amepitia fani
ya uandishi wa habari ama ndio ule upepo vamizi?
Maana
unapoandika habari za mahakamani, polisi kuna misemo yake, hauwezi
kumuhukumu mtu moja kwa moja kwa kusema fulani ni mwizi, hata hao polisi
ambao huwa wanakwenda kukamata watu eneo la tukio hawawezi kusema
fulani ni mwizi mpaka apelekwe mahakamani ndipo sheria ichukue mkondo
wake na kumbaini huyo aliyekamatwa ni mwizi.
Naomba
tufike mahali tuheshimu utu wa watu na kuepuka udhalilishaji wa bila
kujua naamini baadhi ya vijana wengi walioamua kufungua magazeti hayo
tando ambayo yanatoa habari, hawana taaluma ya uandishi wa habari.
Napenda
kuwapongeza wale walioamua kufungua magazeti tando katika milengo yao
tofauti ikiwemo kutoa habari kwa njia ya 'kufundisha masuala ya urembo,
mapishi, kuwasaidia kuwatangaza vijana katika muziki na hata wale
walioamua kuandika habari zao binafsi.
Nayasema
yote hayo kwa vile kumezuka wimbi la vijana wanaotaka kuichafua fani ya
uandishi wa habari na ionekane si fani ya watu walioenda shule bali ni
ya wahuni tu wasiojua mambo, naomba vijana tuelimike na tujifunze kwa
watu wanayoyajua mambo ili tuweze kufika mbele zaidi.
Namalizia kwa kusema tusipoziba ufa tutajenga ukuta.
Asanteni sana kwa kusoma.
Imeandikwa na Cathbert A. Kajuna
No comments:
Post a Comment