Jeshi
la Polisi limeendelea kupata kashfa, baada ya askari wake watatu mkoani
Morogoro na raia mmoja kushikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na fuvu la
kichwa cha binadamu ambalo walikuwa wanalitumia kubambikia watu kesi.
Askari hao wanaofanyakazi katika
wilaya ya Kilosa wanadaiwa kujaribu kukitumia kichwa hicho kutaka
kumbambikia kesi mfanyabiashara mmoja mkoani humo.
Fuvu hilo linadaiwa ni la mtu aliyeuawa hivi karibuni kati ya wilaya za Kilosa na Mvomero mkoani humo.
Tukio hilo limevuta hisia za
watu wengi ambao walikusanyika katika kituo cha polisi katika mji wa
Dumila ambako watuhumiwa hao wanashikiliwa.
Mmoja wa wananchi hao, Saleh
Omar, mkazi wa Dumila, aliwatuhumu askari hao kushirikiana na raia mmoja
kumbambikia kesi hiyo mfanyabiashara ya maduka katika mji wa Dumila,
Samson Mura.
Alisema Jumatatu wiki hii,
walifika askari watatu na raia mmoja ambaye naye alijitambulisha ni
askari wakiwa na mfuko usiojulikana ndani yake kuna nini na kwenda
nyumbani kwa mfanyabiashara huyo wakitaka kumfanyia upekuzi nyumbani
kwake kwa madai kuna vitu vya wizi amevihifadhi.
Baadaye
askari hao walimtaka mfanyabishara kutoka nje na kufungua gari lake
ndogo milango ya mbele, lakini nako hawakukuta kitu na baadaye mlango wa
nyuma na ndipo walipokiweka kichwa hicho kwa siri na kumtuhumu kuwa
alikuwa amefanya mauaji.
Naye Musa Magisa alisema kuwa
wakati tukio hilo linatokea kulikuwa na baadhi ya wananchi ambao
walishuhudia kitendo hicho na kutokukubaliano nacho na hasa baada ya
askari hao kutaka wapewa Sh. milioni 25 ili waachane na kesi hiyo.
“Sisi tuliwakatalia askari hao
kwa kuwa tuliona wazi kuwa walimbambikia mzigo ule ulikuwa ndani na fuvu
la kichwa cha binadamu na tukataka suala hilo lipelekwe katika Kituo
cha Polisi cha Dumila,” alisema Magisa.
Kwa upande wake, Mura alisema
alifuatwa na askari hao watatu pamoja na mtu mwingine aliyejitambulisha
ni askari na kumtaka kumfanyia upekuzi katika nyumba yake na yeye hakuwa
na shaka na kuwaruhusu kufanya hivyo.
“Sikuwa na shaka, niliwaruhusu
kuingia ndani kwa kuwa walijitambulisha kuwa ni maaskari, walingia na
hawakukuta kitu chochote, walipotoka nje wakaniambia fungua gari
wakaangalia mbele wakakosa baadaye katika milango ya nyuma ndiyo wakadai
wamekuta mfuko wenye fuvu la kichwa cha mtu, nikawambia sikuwa na mzigo
kama huo kumbe wananchi walikuwa wakifuatilia, waliona walivyoweka,” alisema Mura.
Hata hivyo, alidai kuwa kabla ya
kuelekea katika kituo cha polisi, askari hao walimwambia awapatie Sh.
milioni 25 ili kumaliza suala hilo, kitu ambacho alikipinga na kuwataka
kulifikisha Polisi.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa
Mgodeni ambako tukio hilo lilipotekea, Zaituni Kifutu, alisema alifuatwa
na askari hao wa kituo cha Dumila ambao anawafahamu na mwingine ambaye
hakumfahamu na alipomuhoji alisema ni askari mgeni kutoka wilayani
Mvomero.
Kifutu alisema baada ya kufanya
upekuzi huo katika nyumba ya mfanyabiashara Mura, hawakukuta kitu ndipo
walihamia katika gari lake.
Aliongeza kuwa baada ya kuona
askari hao wakibishana na mfanyabiashara huyo, yeye na wananchi waliamua
kulifikisha suala hilo katika kituo cha Polisi Dumila.
Hata hivyo, Kifutu alisema baada ya mahojiano, askari huyo aliyejitambulisha kutoka wilayani Mvomero alikiri
kuwa si askari bali ni raia mkata mkaa na kwamba alipigiwa simu na
askari hao kushirikiana naye kumtishia mfanyabiashara huyo ili kujipatia
fedha.
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya
Jinai Mkoani Morogoro, Asifiwe Ulime, alithibitisha kutokea kwa tukio
hilo, lakini hakuwa tayari kutaja majina ya askari hao.
Hata
hivyo, Ulime alieleza kuwa Jeshi la Polisi linawashikilia askari hao
pamoja na raia mmoja kwa ajili ya uchunguzi na utakapokamilika,
watafikishwa mahakamani.SOURCE AUDIFACEJACKSON BLOG
No comments:
Post a Comment