Ndugai, amesema hatua hiyo inatokana na
jinsi umma na taasisi zake vikiwamo vyombo vya habari, ‘vinavyokibeba’
chama pasipo hicho kutafakari kuhusu udhaifu wa Chadema.
Naibu Spika alisema, Chadema ni chama
kinachoungwa mkono, lakini hakina mfumo thabiti wa kiuongozi
unaoshawishi ama kukipa hadhi ya kuunda serikali.
“Lakini sasa watu wanakiona kama ndio
mbadala kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitu ambacho si kweli…ninatamani
sana kuiona Chadema inaingia Ikulu ili watu wauone udhaifu huo na
waandishi wataiandika vipi itakapokuwa madarakani,” alisema.
Ndugai alisema pamoja na azma hiyo
inayolenga kuiaminisha jamii kwamba Chadema haina mfumo bora wa uongozi,
CCM inabaki kuwa chama imara, lakini kikikabiliwa na changamoto
mbalimbali.
Alisema, miongoni mwa changamoto hizo
ni dalili za kuporomoka kwa umoja miongoni mwao, huku miongoni mwao
wakielekea katika kuzitukuza pande za Muungano wanazotoka.
“Hata ndani ya Bunge wakati mwingine
unaweza kuona mgawanyiko kwa wabunge wa CCM, lakini sasa bado
kinaendelea kubaki kuwa chama tawala,” alisema.
Mbunge mmoja wa Chadema ambaye hata
hivyo hakutaka jina lake kutajwa gazetini, aliungana na Ndugai, kwa
nyakati tofauti, akisema chama hicho bado kina upungufu katika safu yake
ya uongozi.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo, uongozi wa
Chadema bado unakabiliwa na changamoto nyingi kuanzia maadili binafsi,
stadi na uwezo wa ki-uongozi katika kuchukua madaraka ya nchi.
“Tunakabiliwa na changamoto nyingi
ambazo kwa Bahati mbaya, viongozi wetu hawapo tayari kutusikiliza sisi
tulio ndani, matokeo yake ni kupunguza kasi ya ukuaji wake,” alisema.
Hata hivyo, Mbunge huyo alisema
Chadema inahitaji kupata wabunge wengi katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na
viongozi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji mwakani, ili
kukifanya kitime wajibu wa kujiimarisha katika ngazi za msingi.
Alisema uwepo wa wabunge wengi wa
Chadema, kutasaidia kuchagiza kasi ya mabadiliko hasa ya kimfumo ikiwa
ni njia ya kukifanya chama hicho kikidhi hitaji la kuunda serikali kwa
miaka ijayo.
VITA DHIDI YA UFISADI
Mbunge huyo aliikosoa Chadema kwa
namna inavyoshiriki vita dhidi ya ufisadi, na kusema inawakwaza baadhi
ya watu wenye uwezo mkubwa kujiunga.
Alisema ni kweli kwamba ufisadi
hautakiwi kwa vile unakwamisha azma ya kufikia maendeleo endelevu na
ustawi wa jamii, lakini nadharia inayoelekezwa kwa baadhi ya viongozi,
pasipo kujali uadilifu wao na uwezo wa kiuongozi, unakifanya chama hicho
kuwakosa ‘watu makini’ zaidi.
“Kuna watu wengi ambao wakijiunga
Chadema, CCM itapasuka na kuwa mwanzo wa kuondoka madarakani, lakini
wanashindwa kuja kwa sababu wameshatajwa na wengine wanaogopa kuhusishwa
na ufisadi,” alisema.
CHADEMA YAMJIBU
Hata hivyo, Chadema imemkosoa Ndugai na kusema kiongozi huyo ameonyesha udhaifu katika kuliongoza Bunge.
“Ndugai ameonesha udhaifu kuliongoza
Bunge na mara zote, udhaifu huo uliibuliwa na kuwekwa wazi na wabunge wa
CHADEMA, hawezi kusema chama kina uwezo duni wa kiuongozi,” alisema
Afisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene.
Makene, alisema kwa takribani miaka
10 sasa, Chadema kupitia viongozi na wabunge wake, imekuwa ikiilekeza
serikali ya CCM (kwa niaba ya Umma), namna bora ya kuutumikia umma,
ingawa (serikali hiyo) sio sikivu.
Alisema umma unakiunga mkono chama
hicho kutokana na wanaona ubunifu, matumaini, haki, uwezo, ufahamu,
umakini, uwajibikaji, utayari, maadili, misimamo na mawazo mbadala kwa
ajili ya maslahi ya watanzania.
“Watanzania si wajinga kuamua
kuchagua kwenda na Chadema, wameuona uongozi bora, sera endelevu,
mikakati thabiti na oganaizesheni imara,” alisema.
Kuhusu ‘kubebwa’ na vyombo vya habari, Makene alisema hiyo ni hoja iliyokufa na kwamba ni dharau kwa wanahabari.
No comments:
Post a Comment