WAZIRI
Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa (pichani) amesema hana fedha wala si
tajiri bali ushawishi mkubwa alionao na wafuasi wengi wanaomuunga mkono
katika shughuli za kimaendeleo ndivyo vinavyomng’arisha.
Kauli
hiyo aliitoa jana wakati wa uzinduzi wa Jumuiya ya Akiba, Mikopo na
Maendeleo Dodoma (Jamimado) katika viwanja vya Kumbukumbu ya Mwalimu
Nyerere.
Lowassa
anayetajwa kuwa miongoni mwa wagombea urais mwaka 2015 kupitia CCM,
ambaye amekuwa akiandamwa kwa kufanya siasa kwenye makanisa, alisema
amekuwa akifanya kazi kubwa ya kuchangia masuala ya maendeleo katika
vikundi mbalimbali kwa lengo la kuwakwamua katika umasikini.
“Najua
mmenipa heshima ya kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Jumuiya ya
Jumimado kwa kuwa mnajua ninachokifanya kwingine. Sina fedha, lakini
nina ushawishi mkubwa kwa watu na wengi wananiunga mkono,” alisema.
Aliwataka
wanajumuiya hiyo kujipanga ili wafanye harambee waweze kupata fedha
zaidi ya sh milioni 500 na kwamba hilo linawezekana.
“Nataka
tukifanya harambee iwe babu kubwa ili kila mtu ajue tumefanya nini, na
nilitamani tufanye harambee hiyo kabla ya mwisho wa mwaka huu. Unajua
ukiwawezesha akina mama umeliwezesha taifa na utakuwa umeondoa
umasikini,” alisema.
Lowassa
alisema ameamua kutoa sh milioni 10 kwa ajili ya maandalizi ya harambee
itakayokuwa na tija pamoja na kuutunisha mfuko wa jumuiya hiyo.
Mwenyekiti
wa Jumuiya hiyo, Aksa Lemwayi katika risala yake alimmwagia sifa lukuki
Lowassa kuwa wanamtambua ni baba wa kupinga umasikini katika maeno
mbalimbali hapa nchini.
“Tunatambua
jinsi anavyosimamia na kutekeleza maamuzi yake katika shughuli za
kimaendeleo, amekuwa ni kiongozi wa aina yake katika kutambua na
kuthamini shughuli za maendeleo katika jamii,” alisema.
Aliongeza kuwa Lowassa amekuwa ni kiongozi anayepigana kufa au kupona kuhakikisha jamii inaondoka kwenye lindi la umasikini.
Lemwayi alisema wanajisikia furaha na ufahari kumualika Lowassa kwenye uzinduzi wa jumuiya hiyo.
Alisema
kuwa jumuiya hiyo kwa sasa inakabiliwa na changamoto za kukosekana kwa
usafiri kwa wanachama wanaotoka maeneo mbalimbali nje ya mji.
Alibainisha
kukosekana kwa usafiri kunafanya shughuli za jumuiya hiyo ikiwemo vikao
vya mara kwa mara kushindwa kutofanyika au kufanyika kwa wakati
usiostahili.
Lemwanyi
aliziomba taasisi za kifedha zipanue mitandao katika kutoa mikopo yenye
riba nafuu ili kuwawezesha Watanzania wengi kujikwamua katika dimbwi la
umasikini ambao kwa sasa ni kilio kikubwa kwa wananchi wengi.
na Danson Kaijage, Dodoma - TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment