Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, August 13, 2013

AJALI YA BASI LA MERIDIAN LAUA WAWILI WENGINE 63 WAMEJERUHIWA


Abiria wawili wamefariki dunia na wengine 63 wamejeruhiwa na kulazwa katika vituo vya afya kadhaa, zahanati pamoja na Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani baada ya basi mali ya Kampuni ya Meridian kuacha njia na kupinduka jana katika Barabara Kuu ya Chalinze- Segera wilayani Bagamoyo mkoani Pwani. 
Abiria waliofariki ni miongoni mwa majeruhi 24 wa ajali hiyo ambao walipelekwa moja kwa moja kupata matibabu katika Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, Tumbi baada ya hali zao kuonekana ni mbaya zaidi ya wengine katika eneo la tukio. Wengi walikuwa wamevunjika sehemu mbalimbali za miili yao.
Kamanda wa Polisi Pwani Ulrich Matei alithibitisha kutokea ajali hiyo.
Akizungumza hospitali hapo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya hiyo, Dk Peter Dattan alithibitisha kupokea baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo na kusema kuwa kati ya 24 waliofikishwa hapo wawili walifariki na wote ni wanaume majina yao bado hayajajulikana.
Dk Dattan alisema majeruhi 22 wanaendelea kupatiwa matibabu na kati yao wanawake ni 12 na kwamba kwa jumla hali zao wote ni mbaya kutokana na majeraha makubwa waliyoyapata.
Naye Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Chalinze walikolazwa majeruhi wengine Dk ,Victor Bamba akizungumza kituoni hapo alisema majeruhi waliofikishwa hapo ni 12.
Alisema majeruhi watatu kati ya hao walikuwa wakifanyiwa mpango wa kupelekwa Tumbi baada ya hali zao kubadilika na kwamba wengi wao wameumia zaidi sehemu za kichwani, kuvunjika miguu, mikono na mbavu
Dk Bamba aliiomba Serikali na wadau wa afya kuhakikisha kuwa utoaji na usambazaji dawa na vifaa tiba unalenga kwenye maeneo yenye ajali nyingi za barabarani ili kuweza kupatikana dawa na vifaa tiba kwa wakati pindi inapotokea matukio ya ajali.
Kwa mujibu wa mashuhuda na wakazi wa Kijiji cha Kimange, Hamis Shaaban na Yusufu Mzee walisema ajali hiyo ilitokea saa 5.40 asubuhi jana.

No comments:

Post a Comment