Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, August 20, 2013

KUKU NDIO CHANZO CHA SISTA WA KATOLIKI KUPIGWA NA KUVULIWA SHELA ZANZIBAR



Kanisa la Minara Miwili, Unguja ambako Sista huyo na wenzake wanafanyia kazi.
Watawa wa kike wa Shirika la Moyo Safi wa Maria, Mgolole, Morogoro, wanaofanya kazi katika Parokia ya Minara Miwili, Unguja, wameiomba Serikali kuongeza ulinzi kwenye maeneo ya kiimani.
Wametoa mwito huo,  baada ya jana kuvamiwa na kundi la watu kwenye makazi yao na kumpiga mmoja, Irene Mwenda na kumvua shela kichwani.
Tukio hilo japo lilihusisha majirani; nyumba ya watawa ya Bububu na majirani wa karibu na nyumba hiyo, waliodai kuku wao aling’atwa na mbwa wa watawa hao, watu wengine waliingilia ugomvi huo wakiwa na wenye kuku na kubishana na watawa hao, jambo lililosababisha ugomvi na hata baadhi yao kumpiga mtawa huyo na kumvua shela.
Mtawa Mkubwa wa Nyumba ya watawa hao visiwani, Sista Gaspara, alimwambia mwandishi jana kuwa tukio hilo halikuwa kubwa kiasi cha Polisi kuingilia kati.
Lakini, alisema ilibidi wapige simu Polisi baada ya kuona kundi la watu, wengi wakiwa vijana na silaha za jadi yakiwamo mawe, wakizungumza kwa jazba na matusi, wakidai kuku wao aling’atwa na mbwa wa watawa na bila kusubiri mazungumzo na namna ya kulipwa, walianza kumpiga mtawa mmoja.
“Ilikuwa saa 11 jioni  jana (juzi), tulikuwa tumerudi kutoka shughuli za ibada nje ya hapa nyumbani, tulipofika likaja kundi la vijana na watoto wakidai mbwa wetu amemng’ata kuku wao, wakati Sista Mwenda akiuliza imekuwaje mbwa ang’ate kuku kwa kuwa huwa tunawafungia ndani, mmoja alimpiga sista ngumi chini ya jicho na sehemu zingine za mwili,” alidai Sista Gaspara.
Alidai Sista Mwenda alitaka vijana wale wasiohusika na kuku waondoke, ili wasijae sana pale na abaki mmiliki wa kuku ili wazungumzie tukio hilo na namna ya kumfidia, maana nyumba ya watawa ina uzio na kuku huyo alirukia ndani kwa kuwa milango ilikuwa imefungwa.
Sista Gaspara alidai kuwa kinachosikitisha si kipigo dhidi ya mtawa, kwa kuwa hakuna damu iliyomwagika ila maumivu ya kawaida aliyopata na kutibiwa katika hospitali ya Jeshi ya Kibweni, lakini kibaya ni namna walivyopandisha jazba kuhusu tukio hilo na kitendo cha kumvua mtawa shela na kuitupa.
Katika utaratibu wa Kanisa Katoliki, shela anayovaa mtawa inabeba maana halisi ya kiimani ya utawa wake, hivyo kitendo cha kuvuliwa kitambaa ni sawa na kuvuliwa utawa. Hata hivyo, waliiomba Serikali kuongeza elimu ya maadili shuleni, wazazi kufunza nidhamu watoto wao na jamii nzima kuheshimu maadili na kuishi kwa amani na utulivu.
Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai wa Zanzibar, Yusuf Ilembo, alithibitisha kutokea tukio hilo lakini akasema ulikuwa ni ugomvi wa kawaida wa majirani kwa majirani, hivyo pamoja na kwamba Polisi ilishirikishwa, lakini uliisha kiujirani.
“Ni kweli suala limetokea, lakini ni ugomvi mdogo wa jirani na jirani, kuku aliingia nyumbani kwa watawa, pale wanafuga mbwa, akang’atwa, wenye kuku walikwenda kudai, ndipo ugomvi ukatokea mmoja akampiga mtawa ila hakuna damu iliyomwagika,” alisema Ilembo.

No comments:

Post a Comment