Dar/Zanzibar. Mauaji,
mashambulizi ya kudhuru mwili na uporaji vimeendelea kuchafua taswira ya
Tanzania baada ya juzi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), kuuawa kwa kupigwa risasi na watu ambao hawajafahamika, raia
wawili wa Uingereza kumwagiwa tindikali na mfanyabiashara kuporwa zaidi
ya Sh40 milioni.
Jana, Rais Jakaya Kikwete alikwenda Hospitali ya
Aga Khan kuwajulia hali raia hao wawili wa Uingereza waliomwagiwa
tindikali huko Zanzibar, Kate Gee (18) na Kirstie Trup (18) akisema
tukio hilo limetia aibu kwa mataifa ya nje na kuliamuru Jeshi la Polisi
kuhakikisha linawakamata na kuwafungulia mashtaka wote waliohusika.
Mauaji
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni,
Camillius Wambura alisema jana kuwa mauaji ya Mhadhiri huyo Msaidizi
katika Idara ya Uhandisi na Teknolojia, Patrick Rweyongeza (32)
yalitokea juzi saa saba mchana maeneo ya Magomeni Tanesco, Dar es
Salaam, wakati marehemu alipokuwa ndani ya gari lake akielekea katikati
ya jiji.
“Alipofika maeneo hayo alivamiwa na watu waliokuwa
kwenye pikipiki aina ya Boxer ambao walimpiga risasi ya kifua upande wa
kulia kisha kutokomea.”
“Baada ya kupigwa risasi alipelekwa Muhimbili
lakini kabla ya kuanza kupatiwa matibabu alifariki dunia,” alisema
Kamanda Wambura.
Alisema hakuna mtu yoyote aliyekamatwa kuhusiana
na tukio hilo. “...Tunaendelea na upelelezi kufahamu tukio hilo
lililofanywa na watu hao kama ni la ujambazi au kisasi.”
Akizungumza nyumbani kwa mjomba wa marehemu
Mbweni, Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Uhandisi, Dk John Mahunza
alisema Rweyongeza alikutwa na mkasa huo baada ya kutoka benki kuchukua
fedha kwa ajili ya shughuli za ofisi.
“Baada ya kuchukua fedha hizo Ubungo, alipanda
gari kuelekea Magomeni na kufika maeneo ya Tanesco, walimzingira na
kumlazimisha kufungua mlango, lakini aligoma na wakampiga risasi,”
alisema.
“Baada ya kumpiga risasi mkononi, walimpora
bahasha iliyokuwa na fedha... nadhani wale walikuwa wanamfuatilia tangu
alipokuwa benki hadi anatoka.CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment