Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, August 22, 2013

MBEZI LUIS NA BASIHAYA KUJENGWA VITUO VYA MABASI YAENDAYO MIKOANI

IMG_2579Msemaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bw. Gaston Makwembe KUSHOTO akiwaeleza waandishi wa habari Mpango wa Halmashauri kujenga vituo vya Mabasi yaendayo mikoani na nchi za jirani katika maeneo ya Mbezi Luis na Boko Basihaya katika mkutano na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam KULIA ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bi. Zamaradi Kawawa.
IMG_2592Meneja wa Kituo cha Mabasi Ubungo Bw. Juma Iddi KUSHOTO akifafanua jambo kwa waandishi wa habari juu ya ushiriki wao katika utoaji wa huduma ya usafiri wa Mabasi yaendayo haraka(Dar Rapid Transit-DART) katika mkutano na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam KULIA ni Msemaji wa Halmashauri hiyo Bw. Gaston Makwembe.
PICHA NA ELIPHACE MARWA.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam itajenga vituo vya mabasi yaendayo mikoani na nchi za jirani katika maeneo ya Mbezi Luis na Boko Basihaya. Ujenzi wa vituo hivyo ni utekelezaji wa mipango ya Jiji ya kuimarisha huduma za usafiri Dar es Salaam. Kituo cha Mbezi Luis kitahudumia wasafiri wa Kanda ya Kati na Nyanda za Juu wakati Kituo cha Boko Basihaya kitatoa huduma kwa wasafiri wa Kanda ya Kaskazini. Kwa Kanda ya Kusini Halmashauri ya Jiji itajenga Kituo cha Mabasi Kongowe.
Kituo kitakachoanza kujengwa ni Mbezi Luis ambacho kitajengwa sambamba na Boko Basihaya. Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo kimepangwa kutoa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka kwa wasafiri wote watakaokuwa wakitumia vituo hivyo vya mabasi yaendayo mikoani. Ujenzi wa vituo vya Mbezi Luis na Boko Basihaya, kutokana na upembezi yakinifu wa awali, unakadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 40 kwa kila kituo.
Ujenzi wa vituo hivyo unahitaji upembuzi yakinifu wa kina kwa lengo la kupata gharama halisi za utekelezaji wake, kubaini vyanzo vya fedha na kuangalia uwezekano wa kuzishirikisha taasisi mbalimbali za fedha na wawekezaji wanaoonyesha nia ya kushirikiana na Halmashauri ya Jiji katika ujenzi wa vituo hivyo ambavyo vitakapokamilika vitakuwa pia ni chanzo cha ajira kwa wananchi.
Katika kipindi hiki cha maandalizi ya ujenzi wa vituo hivyo, bado Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT) kitaendelea kutoa huduma kwa wasafiri waendao mikoani na nchi za jirani. Halmashauri ya Jiji inapenda wananchi wafahamu kwamba UBT, kama ilivyopangwa na Serikali, itakuwa ni kituo kitakachotoa huduma ya usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka(Dar Rapid Transit-DART) baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu yake. Pamoja na hilo Halmashauri ya Jiji pia itajenga “shopping malls” na hoteli katika kituo hicho cha UBT
Kukamilika kwa ujenzi wa vituo hivyo vya mabasi ni mafanikio makubwa katika jitihada za serikali za kuimarisha huduma za usafiri katika Jiji la Dar es Salaam. Wadau wa maendeleo katika sekta hii, wananchi na taasisi mbalimbali wanategemewa kuendelea kutoa mapendekezo yao ya kuimarisha huduma za usafiri Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment