skip to main |
skip to sidebar
Picha hii imezua mjadala na CHADEMA kulazimika kuitolea ufafanuzi...
- Yadai Ofisa wa Polisi anayeonekana kwenye picha, alikuwa akiwaelekeza
watu wasogee pembeni kwanza, akimwambia Slaa asubiri kidogo watengeneze
njia 'vizuri' apite!
Ndugu wana JF
Tangu mapema sana asubuhi, tumepokea simu kutoka maeneo mbalimbali ya
nchi, watu tofauti, wakionesha concerns zao juu ya taarifa kuwa ofisa
mmoja wa Jeshi la Polisi ameonekana kwenye picha 'akimdhibiti' Katibu
Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willbroad Slaa.
Picha na maelezo yake (caption) yameonekana kuwasononesha na kuwatisha watu wengi.
Ili kusaidia jamii na kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea, iwapo
usahihi wa tukio hilo hautaelezwa, tumeona ni vyema kwa nafasi yetu
kuweka kumbukumbu sawa.
USAHIHI; Kama ilivyo ada ya misafara ya CHADEMA, hasa inapohusisha
viongozi wakuu, viongozi (watendaji waandamizi) wengine wa kitaifa,
wabunge na viongozi wengine wa chama katika maeneo husika, huwa ina
hamasa, shamrashamra na mapokezi makubwa kila mahali kunapofanyika
mikutano au shughuli ya kichama.
Katibu Mkuu, Dkt. Slaa na timu yake walipotua Mpwapwa kwa helkopta siku
ya Agosti 18, mwaka huu, alilakiwa na umati mkubwa wa watu, wakitaka
kumsalimia na kumkumbatia. Wakifurahia ujio wa mmoja wa viongozi wakuu
wa chama katika eneo lao, kwa ajili ya kuendesha Mabaraza Huru ya Rasimu
ya Katiba Mpya, katike eneo hilo.
Katika hali kama hiyo, walinzi, wakiwemo askari polisi, walikuwa
'concerned' na hali ya usalama, maana 'lolote' laweza kutokea. Ofisa wa
Polisi anayeonekana kwenye picha, alikuwa akiwaelekeza watu wasogee
pembeni kwanza, akimwambia Daktari asubiri kidogo watengeneze njia
'vizuri' apite, maana watu wote wale kumfuata na kumkumbatia ingeweza
kuwa hatari.
Kama anavyoonekana, Dkt. Slaa naye alikuwa akijaribu kumwambia yule
askari kuwa awasaidie wale watu bila kuharibu utaratibu wa yeye
kusalimiana na wananchi wake, ambao hujaa kumlaki kwa nia njema, bila
kukodiwa wala kusombwa.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa. Hakukuwa na 'kudhibitiana', bali kulikuwa na kuongozana.
Timu ya Katibu Mkuu, kama ilivyo kwa Mwenyekiti Freeman Mbowe, kwa
kutumia usafiri wa chopa, inaendelea na ratiba ya kuendesha Mabaraza
Huru ya Rasimu ya Katiba Mpya, ambapo muda huu timu ya Mwenyekiti
imeshaingia Mkoa wa Katavi, kutokea Tabora na timu ya Dkt. Slaa iko
Morogoro!
Maelfu ya Watanzania wanaendelea kupata fursa ya kushiriki moja kwa
moja, kutoa maoni yao kwenye mabaraza hayo, yanayoendeshwa kwa njia ya
wazi kwenye mikutano ya hadhara.
Nawe unaweza kuendelea kutoa maoni yako ya katiba, kwenye Mabaraza Huru
ya Rasimu ya Katiba Mpya, kupitia ujumbe mfupi kwenye namba 0789 248224
au email; chademamaoni@gmail.com
Asanteni.
Makene
0752 691569
No comments:
Post a Comment