Moja ya sifa ambazo Tanzania imejizolea katika medani za kimataifa katika miaka ya hivi karibuni, ni sifa ya kuwa moja ya vinara wa biashara ya dawa za kulevya duniani. Tofauti na sifa nyingine ilizonazo, ikiwamo sifa ya kuwa taifa lenye amani na utulivu, mara hii sifa ya kubobea katika biashara ya dawa za kulevya siyo sifa ya kujivunia hata kidogo.
Ni sifa inayochafua taswira ya nchi yetu, kwani
hivi sasa Watanzania wanaosafiri nje ya nchi wanaficha nyuso zao kwa
aibu kutokana na upekuzi wa aina yake wanaofanyiwa na mamlaka za forodha
na uhamiaji. Msafiri mwenye pasi ya kusafiria iliyotolewa na Serikali
ya Tanzania kila anapoingia katika nchi ya kigeni anapata msukosuko
mkubwa.
Matukio ya Watanzania kukamatwa ughaibuni wakiwa
na dawa hizo hakika ni matukio yanayotoa taswira ya taifa linaloanza
kupotea njia. Katika kipindi cha wiki mbili tu, Watanzania wanne
wamekamatwa katika nchi mbalimbali wakiwa na dawa hizo na wakiwa
wametokea Tanzania.
Mwezi uliopita, wasichana wawili Watanzania
walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo, Afrika
Kusini wakiwa na kilo 150 za dawa za kulevya aina ya Crystal
Methamphetamine zenye thamani ya Sh6.8 bilioni wakitokea Dar es Salaam.
Hata hivyo, kitendawili cha namna shehena hiyo kubwa ilivyoweza kupita
uwanja wa ndege Dar es Salaam bila kugunduliwa na mamlaka husika bado
hakijateguliwa. Hivi sasa wasichana hao wamefunguliwa mashtaka nchini
humo.
Katika tukio la aina hiyo, Watanzania wawili wiki
iliyopita walikamatwa Hong Kong, China wakiwa na dawa za kulevya aina ya
heroin zenye thamani ya Sh7.6 bilioni wakitokea Dar es Salaam kupitia
Dubai. Maofisa wa Uwanja wa Ndege wa Hong Kong (HKIA) wamesema kwamba
katika wiki hiyo, walimkamata kijana mwenye miaka 26 akitokea Tanzania
akiwa na dawa za kulevya kilo 1.6 aina ya heroin zenye thamani ya Sh1.5
bilioni na kwamba jioni ya siku hiyo, walimkamata Mtanzania mwingine
mwenye miaka 45 akiwa amemeza gramu 240 za dawa za kulevya aina ya
heroin.
Tatizo la biashara ya dawa za kulevya hapa nchini
limekuwa kubwa, kwani takwimu zinaonyesha kuwa, kuna orodha kubwa ya
Watanzania waliokamatwa ughaibuni wakiwa na dawa hizo na wengi wao
wanasubiri kunyongwa. Jambo la kusikitika ni kuwa, pamoja na kwamba kwa
muda mrefu Serikali imekuwa na orodha ya magwiji wa biashara ya dawa
hizo, imekuwa ikishikwa na kigugumizi cha kuwataja au kuwafungulia
mashtaka. Hata pale baadhi yao walipofunguliwa mashtaka, kesi zao
zimekuwa zikipotea hivihivi tu pasipo maelezo.
Sisi tunadhani katika hili Serikali inastahili
kubeba lawama kwa kuwalea na kuwakingia kifua magwiji wa biashara hiyo.
Lazima tutambue kwamba Watanzania wanaokamatwa na dawa hizo hapa nchini
na huko ughaibuni ni dagaa tu, kwani wenye biashara hiyo wamekaa kando
na Serikali inawafahamu.
Mwishoni mwa wiki, katika mhadhara wa kongamano la
kidini lililofanyika jijini Mbeya, vijana wawili waliokuwa wakitumiwa
kusafirisha dawa hizo, walisalimisha kilo tano za dawa aina ya heroin
baada ya kuguswa na mahubiri katika kongamano hilo, huku wakitaja majina
ya wamiliki wa dawa hizo, wakiwamo baadhi ya mawaziri na wabunge. Sasa
tumekuwa taifa la wauza unga.SOURCE GAZETI LA MWANAINCHI
No comments:
Post a Comment