Mwanamke
mmoja raia wa Uingereza ametajwa na gazeti moja la nchi yake kuwa ndiye
aliyeongoza shambulizi la kigaidi lililofanywa katika eneo la maduka la
Westgate jijini Nairobi, Jumamosi iliyopita.
Gazeti la
Daily Mail la Uingereza lilikariri vyanzo vyake ndani ya duru za
usalama za Kenya ambavyo vilieleza kuwa magaidi hao wanaoaminika kuwa ni
wafuasi wa Kundi la kigaidi la Al-Shabaab la Somalia waliongozwa na
mwanamke anayeitwa Samantha Lewthwaite maarufu kwa jina la White Widow
(Mjane Mweupe)
Hata
hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Ole Lenku amesema
wanaamini kuwa magaidi waliovamia jengo hilo la Westgate wote ni
wanaume.
Ole Lenku
alisema baadhi ya watekaji hao walivalia nguo za kike ili kuwachanganya
watu na kwamba tayari wawili kati yao wameshauawa na vikosi vya
usalama.
Wakati
Ole Lenku akisema hayo, Mkuu wa Majeshi ya Kenya, Jenerali Julius
Karangi alisema kuwa wanajua magaidi hao wanatoka wapi lakini hakutaka
kueleza zaidi.
Lewthwaite
anayeaminika kuwa na umri wa miaka 29, alifiwa na mumewe, Jermaine
Lindsay baada ya kulipua bomu la kujitoa muhanga Julai 7, 2005 jijini
London, Uingereza.
Kundi la
Al-Shabaab ambalo limekiri kuhusika na shambulizi hilo, kupitia mtando
wa Twitter lilitoa taarifa jana likimsifia Lewthwaite, ambaye siku hizi
anatumia jina la Sherafiyah.
"Sherafiyah
Lewthwaite a.k.a Samantha ni mwanamke shujaa na tunajivunia kuwa naye.
Askari wetu wa Mujahideen wamejitolea kufa katika operesheni hii."
Milio ya silaha nzito na mabomu ilisikika kwenye eneo hilo la Westgate wakati wa mapambano kati ya polisi na magaidi hao.
Awali
askari wa Kenya walieleza kuwa mwanamke aliyevalia hijab ndiye
aliyeongoza kati ya watu 10-15 wenye silaha kuvamia jengo hilo.
Maofisa
wa usalama wa Kenya ambao hawakupenda kutajwa majina walikaririwa
wakisema kuwa watu wengi waliokuwa wameshikiliwa na magaidi hao walikuwa
wameachiliwa na bado jitihada zilikuwa zinafanyika kuwaokoa mateka
waliobakia.
Kwa
mujibu wa Daily Mail, mbali ya Lewthwaite, raia wengine wa Uingereza
wanaohusishwa na tukio hilo ni Liban Adam (23) na Ahmed Nasir Shirdoon
(24), ambao pia wametajwa kwenye taarifa ya Al-Shabaab.Kundi hilo
limesema kuwa limefanya shambulizi hilo kwa nia ya kuishinikiza Serikali
ya Kenya kuondoa vikosi vyake ndani ya Somalia.
Lewthwaite ni nani?
Lewthwaite, ambaye alikulia katika eneo la Buckinghamshire ni binti wa mwanajeshi wa zamani wa Uingereza.
Katika kipindi cha utoto wake Lewthwaite alipendelea zaidi kusomea muziki wa disco.
Anatokea katika familia ya Kikristo na aliamua kuingia kwenye Uislamu kabla ya kuolewa na Lindsay.
Mwanamke huyo anadaiwa kuwa amekuwa akiendesha mafunzo ya kigaidi kwa wanawake akiwa Somalia na Kundi la Al-Shabaab.
Lewthwaite alifahamiana na marehemu mumewe Jermaine Lindsay kupitia intaneti.
Wakati
Lindsay alipohusishwa na shambulizi la kigaidi mwaka 2005 jijini London,
Lewthwaite alimshutumu mumewe kwa kitendo kile.:CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment