Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, November 20, 2012

WACHEZAJI 20 WALIOITEKA ULAYA KWA KUZISAIDIA TIMU ZAO





Kabla ya kuwataja wachezaji bora 20 ambao wameiteka Ulaya, napenda kuthamini mchango wa wachezaji hawa katika timu zao Yaya Toure, Xavi, Mario Gotze, Wayne Rooney, na Hazard. Hawa wamekuwa kwenye viwango bora kabisa msimu huu huku wakiziwezesha timu zao katika kupata matokeo bora.

Frank Ribery (20) 
Mfaransa huyu amekuwa akijitolea kila kitu kwa ajili ya klabu yake ya Bayern Munchen. Licha ya matatizo yake ya kugombana na winger mwenzake wa Bayern, Arjen Robben mara kwa mara, Ribbery amekuwa bora mara zote anapoingia ndani ya uwanja. Hivi karibuni Ribbery alikaririwa akisema kwamba anaipenda Bayern kuliko timu ya taifa ya nchi yake, Ufaransa. Ribbery anashika nafasi ya 20 katika viwango hivi.

Edin Dzeko (19) 
Amekuwa akitokea pale anapohitajika. Edin Dzeko amekuwa bora zaidi msimu huu hasa pale anapotokea benchi, watu kama Edin huitwa Super Sub. Yeye ndiye mtu ambaye amekuwa akiipa matokeo mazuri Manchester City mara kwa mara pale inapoonekana kushindwa. Huku akiwa na kiatu cha ufungaji bora cha ligi kuu ya Ujerumani pia mchezaji bora wa wachezaji wa ligi kuu ya Ujerumani, Dzeko ameendelea kumuonesha Roberto Mancini yeye ni mchezaji wa aina gani. Dzeko amekuwa wa 19.

Demba Ba (18) 
Huu ndio ulikuwa usajili bora wa msimu wa 2011/2012 kulingana na makocha wa timu za ligi kuu ya Uingereza. Baada ya Papiss Cisse kusajiliwa January, 2012, Ba alifunga goli moja tu, tangu msimu huu kuanza imekuwa kinyume chake, Cisse hafungi na Ba amerudi kuwa roho ya timu. Kama akiendelea na kiwango hiki Ba anaweza kuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya Uingereza. Ba anashika nafasi ya 18.

Marco Reus (17) 
Moja ya vipaji kutoka Ujerumani vinavyokuja kwa kasi ni huyu Marco Reus. Akisajiliwa kutoka Borussia Monchengladbach kuja kuziba pengo la Shinji Kagawa, Marco ameweza kushirikiana vyema na Mjerumani mwenzake, Mario Gotze pia mshambuliaji Lewamdowski katika kuiboresha timu ya Borussia Dortmund. Marco Reus ndiye mchezaji bora wa Ujerumani kwa mwaka huu, 2012. Reus anashika nafasi ya 17.

Thomas Muller (16) 
Mchezaji bora kijana wa kombe la dunia, 2010. Baada ya kuwa akitokea benchi msimu uliopita wakati Mario Gomez alipokuwa katika kiwango cha juu. Thomas Muller amekuwa akitengeneza chemistry nzuri na mshambuliaji mwingine wa Bayern Munich, Claudio Pizzaro. Mara nyingi Muller amekuwa hatajwi sana midomoni mwa wapenda kabumbu lakini yeye amaandelea kutunza kiwango chake vyema na sasa yupo kwenye kiwango cha hatari. Amekuwa wa 16.

Klaas-Jan Huntelaar (15) 
Wenyewe humwita Hunter, amekuwa akifananishwa na Ruud van Nistelrooy na Marco van Basten kutokana na jinsi anavyouchezea mpira. Kocha wa zamani wa Barcelona Louis van Gaal aliwahi kusema kwamba huyu ndiye mchezaji bora katika dimba la penalti. Tangu ajiunge na Schalke 04 akitokea Milan, Huntelaar amekuwa kwenye kiwango bora na ndiyo mhimili wa Schalke. Hivi sasa ana ushirika mzuri kabisa na Mholanzi mwenzake aitwaye, Ibrahim Affelay. Amekuwa wa 15.

Oscar (14) 
Kipaji cha ajabu kutoka Brazil. Uwezo wa kumiliki mpira, nguvu, pasi na jinsi anavyojitoa uwanjani haipingiki kwamba Oscar atakuja kuwa moja ya wachezaji hatari sana katika timu ya taifa ya Brazil. Oscar ndiye mchezaji wa Chelsea anayeng’ara zaidi katika ligi ya mabingwa Ulaya msimu huu kuliko mchezaji yeyote mwingine ndani ya klabu. Goli la pili aliloifunga Juventus katika mechi yake ya kwanza ya ligi ya mabingwa Ulaya halitafutika kirahisi katika vichwa vya wapenzi wengi wa soka. Alipoulizwa atoe maoni yake kuhusiana na goli lile, kipa wa Juventus, Gigi Buffon alisema hivi, “Siwezi kusema ni vizuri kufungwa goli lakini ni vizuri kuwa sehemu ya goli bora kama lile. Hongera kwake”. Oscar ni wa 14.

Maroune Fellaini (13) 
Mchezaji ghali zaidi wa klabu ya Everton. Huyu ndiye alikuwa gumzo zaidi wakati ligi ya Uingereza ilipokuwa katika wiki za mwanzo mpaka sasa. Akiwa ni mzaliwa Ubelgiji na asili ya Morocco, Maroune Abdellatif Fellaini amekuwa kiwango bora zaidi msimu huu kuliko msimu mwingine wowote katika maisha yake. Watu wengi wamekuwa wakiifuatilia Everton kwa sababu ya huyu mtu na yeye ndiye ubongo nyuma ya mafanikio ya Everton kwa msimu huu. Anazivutia klabu kubwa nyingi huku Chelsea ikiongoza mbio za kumnyakua, si ajabu kuona akihamia kwenye timu inayoendana na kiwango chake. Amekuwa wa 13.

Gonzalo Higuain (12) 
Mtambo wa magoli kutoka mzaliwa wa Ufaransa. Huyu ndiye patna wa Cristiano Ronaldo katika kupasia mipira nyavuni pale Real Madrid kwa sasa. Mafanikio ya Gonzalo msimu huu yamechangiwa zaidi na kuumia na kiwango cha Karim Benzema kushuka. Katika siku za hivi karibuni Higuain amekuwa akishirikiana vyema na Lionel Messi katika kutengeza nafasi za magoli katika timu ya taifa ya Argentina. Amekuwa wa 12.

Luis Suarez (11) 
Mchezaji ambaye amekuwa akiandamwa na mikasa ya kutosha tangu adake mpira uliokuwa ukiingia nyavuni katika mechi ya robo fainali ya kombe la Dunia pale Afrika Kusini dhidi ya timu ya Ghana. Pamoja na mikasa mingi kuwa upande wake Luis Suarez hajashuka kiwango na msimu huu tofauti na misimu mingine amekuwa akifunga magoli mengi ingawa timu yake ya Liverpool bado mambo hayajawa mazuri. Ndiye mchezaji anayeng’ara zaidi kwa majogoo wa jiji. Amekuwa wa 11.

Andrea Pirlo (10) 
Ule usemi wa ng’ombe hazeeki maini uhalisia wake huonekana hapa. Watumiaji wa mvinyo humfananisha Andrea Pirlo na kinywaji hicho, kadri kinywaji kinavyozidi kukaa ndivyo ubora wake unavyoongezeka. Kadri umri wa Pirlo unavyoongezeka ndivyo kiwango chake kinavyoongezeka. Huyu ndiye chachu hasa ya mafanikio ya Juventus katika kumaliza msimu uliopita bila kufungwa na Italia kufika kwenye fainali ya kombe la Ulaya. Amefunga 10 bora.

Juan Mata (9) 
Pamoja na kwamba Didier Drogba ndiye aliyeiwezesha Chelsea kushinda kombe la FA na lile la ligi ya mabingwa Ulaya kwa kiasi kikubwa katika mechi za fainali, Mata ndiye aliyekuwa mchezaji bora wa Chelsea kwa msimu uliopita. Msimu uliopita Mata alikuwa kwenye kiwango bora lakini sasa hivi amekuwa zaidi ya alivyokuwa msimu uliopita. Juan Manuel Mata Garcia anaendelea kuwa mchezaji bora wa Chelsea mpaka sasa. Huyu ndiye mchezaji bora wa ligi ya Uingereza kwa mwezi wa 10, mwaka 2012. Amekuwa wa 9.

Bastian Schweinsteiger (8)
Roho ya timu ya Bayern Munchen, akifunga magoli na kutoa pasi za mwisho za kutosha. Basti kama marafiki zake wanavyomwita ametengeneza chemistry katika timu ya Bayern hasa katika sehemu ya kiungo ya timu. Uwezo mkubwa wa kukota aliokuwa nao, pasi kali ‘zenye macho’ , uwezo mkubwa wa kukaba, uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, na mwisho wa yote ni uwezo wake mkubwa wa kupiga mipira iliyokufa unamfanya awe mchezaji wa kipekee. Schweinsteiger ana nafasi kubwa ya kuingia kwenye FIFA FIFPro World XI ya mwaka huu. Amekuwa wa 8.

Andres Iniesta (7) 
Mchezaji bora wa Ulaya kwa mwaka 2012, siku zote amekuwa kwenye kiwango bora. Iniesta kwa sasa yupo kwenye kiwango cha juu cha soka katika maisha yake. Yeye ndio mtu anayeng’aa zaidi kwenye timu yenye vipaji lukuki ya Spain. Sababu ya Iniesta kushika namba 7 katika listi hii ni kutokana na makali kupungua kidogo tangu mashindano ya Ulaya kuisha pia ni kutokana na watu waliopo juu yake viwango vyao kuongezeka kwa kiasi kikubwa. Kitu ninachoamini ni kuwa lazima Iniesta atajwe kugombania FIFA Ballon d’Or katika wale watu watatu wa mwisho.

Stephan El Shaarawy (6) 
Mashabiki wake humwita ‘The Pharaoh’ kwa sababu amezaliwa na wazazi wenye asili ya Misri pale Savona, Italia. Huyu ndio nguzo ya Milan kwa sasa katika upachikaji mabao baada ya Zlatan Ibrahimovic kuondoka. Akivaa jezi yenye namba ya mwaka aliozaliwa, # 92 (1992), na ikiwa ndio kwanza katimiza miaka 20 juzi tu mwezi October, Firauni huyu amekuwa tishio sana kwa mabeki wa timu pinzani zinazopambana aidha na Italia ama A.C Milan. Nimempa namba 6 kwa sababu anastahili.

Zlatan Ibrahimovic (5) 
Mtaalamu huyu mwenye mkanda mweusi wa mchezo wa karate amekuwa mkubwa kuliko ligi ambayo anacheza ndani yake. Tangu kuhama kutoka AC Milan na kutua PSG mambo yamekuwa rahisi sana kwa Ibracadabra. Kutokana na aina yake ya mchezo na kipaji chake watoto wa mjini wanakwambia, Ibra sio wa leo wala kesho wakimaanisha, Zlatan ataendelea kung’aa kwenye medani nzima ya soka kwa kipindi kirefu kidogo mpaka pale atakapoamua kustaafu. Huyu ndiye mfungaji anayeongoza katika ligi kuu ya Ufaransa kwa sasa. Tarehe 14 mwezi huu wa 11, 2012, goli la 4 aliloifunga Uingereza linasemekana kuwa goli la karne. Zlatan Sefik Ibrahimovic ni namba 5.

Radamel Falcao (4) 
Ukiwa ni msimu wake wa pili katika ligi kuu ya Spain, Radamel Falcao ameibuka ghafla na kuwa gumzo katika bara lote la Ulaya. Falcao ndio mpinzani mwenye nguvu wa Ronaldo na Messi ambaye alikuwa akinghojewa katika kugombania kiatu cha dhahabu cha ligi kuu ya Spain. Akiwa tayari ameshinda kombe La UEFA akiwa na Porto ya Ureno pamoja Athletico Madrid aliko sasa ambako pia majuzi alishinda UEFA Super Cup pale alipoichabanga Chelsea goli 3 peke yake katika ushindi wa 4-1, Falcao ameendelea kuwa mchezaji wa kutumainiwa katika kila timu anayoitumikia. Falcao anastahili nafasi ya 4.

Robin van Persie (3) 
Huyu ndiye mchezaji bora wa ligi kuu ya Uingereza kwa msimu uliopita, 2011/12, huku akiwa hana muda mrefu tangu ajiunge na mashetani wekundu akitokea kwa mahasimu wao wakubwa, Arsenal, RvP amekuwa ndio nguzo katika mashambulizi ya United msimu huu akiwa ameifungia goli 8 tayari na pasi za magoli 3 kwenye ligi kuu, van Persie ameendelea kuwa moja ya nembo za ligi kuu ya Uingereza kwa wakati huu. Hivi karibuni wakati Sir Alex Ferguson alipochaguliwa kuwa kocha bora wa mwezi October alimshukuru Robin kwa kutoa mchango mkubwa sana katika tuzo yake hiyo. Robin van Persie anakuwa wa 3 nyuma ya Ronaldo na Messi.

Cristiano Ronaldo (1) 
CR7 kama anavyopenda kujiita. Yeye kaiteka dunia ndani ya uwanja na nje ya uwanja. Cristiano Ronaldo ni moja ya wachezaji adimu sana katika kizazi hiki cha leo. Uwezo wake wa kupasia ‘kamba’ umekua ukiongezeka siku baada ya siku. Ronaldo ndiye mchezaji anayetawala vichwa vya habari vya magazeti kila kukicha pamoja na ‘fundi’ mwingine kutoka Italia aitwaye Super Mario Balotelli. Mtupia mabao huyu ambaye ndio anaongoza magoli katika ligi ya mabingwa Ulaya msimu huu akiwa na goli 5 katika mechi 4 alizocheza amekuwa akisifika kwa bidii yake ya kujituma mazoezini na kwenye mechi. Kutokana na yote haya Cristiano pia anashikilia namba moja pamoja na Leo Messi. Ronaldo ndiye mchezaji bora wa mwaka huu, 2012 wa Goal.com, mtandao wa soka wenye heshima kubwa zaidi.

LIONEL Messi (1) 
Ameendeelea kuiteka dunia kutokana na kipaji chake ambacho kinawashangaza wadau wengi wa soka. Huku akishikilia rekodi ya kufunga magoli mengi duniani katika msimu mmoja, magoli 73 katika msimu wa 2011/12 na magoli 76 mpaka sasa kwa mwaka huu akiwa nyuma ya Gerd Muller, urafiki wa Messi na nyavu umezidi kudumishwa siku baada ya siku ikumbukwe kwamba kila goli analofunga Messi kwa hivi sasa ni rekodi katika klabu ya Barcelona kwa sababu yeye ndiye mfungaji bora wa klabu kwa wakati huu. Kwa sasa mchezaji huyu bora wa dunia yuko katika kiwango sawa na mshindani wake wa karibu wa siku zote, Cristiano Ronaldo ndio maana wote wamekuwa vinara kwa kushikilia namba moja.

No comments:

Post a Comment