Na Irene Mark
WATUMIAJI
wa simu wapatao milioni nane wapo hatarini kufungiwa simu zao ifikapo
mwishoni mwa mwezi huu, Tanzania Daima limebaini.
Tayari
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeziandikia kampuni za simu waraka wa
kuzitaka zianze kukata kodi mpya ya laini (simu card) mara moja kuanzia
Julai 30, 2013.(hd)
Kwa maana hiyo kila anayemiliki laini
moja ya simu atakatwa sh 3,000; anayemiliki laini mbili sh 6,000 na
anayemiliki laini tatu sh 12,000, lengo ni kuhakikisha serikali
inakusanya sh bilioni 178 zitakazopelekwa kwenye bajeti kuu ya serikali.
Watumiaji wa simu sasa watalazimika kulipia kodi hiyo ya miezi mitatu ya Julai, Agosti na Septemba kwa wakati mmoja.
Bunge
kupitia Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi,
Andrew Chenge (CCM) lilitaka kuwapo kwa kodi hiyo ili kusaidia shughuli
za bajeti ya Serikali Kuu.
Kupitishwa
kwa kodi hiyo kuliibua malalamiko ya wanasiasa dhidi ya Chenge
anayelazimisha kuwapo kwa kodi hiyo, huku akishindwa kuamini kwamba kuna
Mtanzania anayekosa sh 1,000 kwa mwezi kwa ajili ya laini ya simu.
Malalamiko
hayo yaliendelea hadi kwa wananchi na baadhi ya wabunge wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) waliotaka posho za wabunge zipunguzwe
ili kuziba pengo hilo badala ya kuwabebesha wananchi mzigo.
Inadaiwa
kwamba msimamo wa Chenge unaungwa mkono na Spika wa Bunge, Anne Makinda,
jambo lililosababisha kutojadiliwa kwa hoja binafsi ya Mbunge wa Kawe,
Halima Mdee (CHADEMA) iliyohusu kodi hiyo katika mkutano wa Bunge
lililopita kwa kisingizio cha kukosekana kwa muda wa kufanya hivyo.
Hata
hivyo, takwimu zilizotolewa na kampuni za simu zinaonyesha kuwa miongoni
mwa wamiliki wa laini za simu milioni 22; milioni nane wanatumia chini
ya sh 1,000 kwa mwezi.
Baada ya
malalamiko hayo, Rais Kikwete alikutana na wadau wa mawasiliano ambao ni
wamiliki wa kampuni za simu Tanzania (MOAT), Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Waziri wa Fedha,
William Mgimwa, kisha kuwaagiza waiondoe kodi hiyo.
"Rais
alisema lengo kuu la mkutano huo liwe kupendekeza jinsi ya kuziba pengo
la sh bilioni 178 zitakazopotea katika bajeti iwapo kodi hiyo itafutwa.
"Alisema
hawezi kuifuta moja kwa moja kodi hiyo, bila kutafuta njia nyingine za
kupata fedha kujazia pengo litakalotokeza huku tayari Bunge limezipangia
matumizi," alinukuliwa Makamba baada ya kikao hicho na rais.
Kwa
upande wake, rais alikaririwa akiwaambia wadau hao wa mawasiliano
kwamba: "Nakuombeni kaeni pamoja, wekeni bongo zenu pamoja, wekeni akili
yenu pamoja tutafute namna gani tutajaza pengo hili la sh bilioni 178
endapo tutakubaliana kuwa kodi hii inawabebesha wananchi mzigo mzito, na
kuwa pengine menejimenti ya kodi yenyewe ni ngumu."
Licha ya
agizo hilo la rais kutekelezwa kwa MOAT kutakiwa kuongeza kodi nyingine
iitwayo 'Excise duty' kutoka asilimia 14 hadi 17 bila kujali kwamba
katika Bunge la bajeti kodi hiyo iliongezwa kutoka asilimia 12 hadi
asilimia 14, tozo hiyo ya laini za simu haijaondolewa.
Wachambuzi
wa masuala ya siasa na mawasiliano walisema kutojadiliwa kwa mabadiliko
ya kodi hiyo ya simu ni dalili kwamba Waziri wa Fedha amezidiwa nguvu
na kiti cha spika kinachounga mkono hoja hiyo ya Chenge na kushindwa
kutekeleza agizo la rais.
Wataalamu
wa mawasiliano walilieleza gazeti hili kwamba kuongezeka kwa kodi hiyo
kutaifanya Tanzania kuwa na kiwango cha juu cha kodi kuliko nchi
nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ushauri
wa wataalamu hao ulibainisha kwamba kuongezeka kwa kodi hiyo kunaleta
nafuu kidogo kuliko ile ya laini za simu inayomuumiza zaidi mwananchi wa
kawaida:CHANZO TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment