






…………….
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema idadi kubwa ya mifugo katika bonde la mto
Mara ni mojawapo ya changamoto zinazokabili utunzaji endelevu wa bonde
na amewataka viongozi wa mkoa watoe elimu ya kutosha kwa wananchi ili
wafuge kisasa na kuepusha uharibifu wa mazingira.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Septemba 15, 2013) wakati akifunga
maadhimisho ya Siku ya Mara (Mara Day Celebrations) yaliyofanyika kwenye
uwanja wa Sokoine mjini Mugumu, wilayani Serengeti mkoani Mara.
Maadhimisho hayo yalianza Septemba 12, mwaka huu.
“Changamoto
iliyopo ni kuainisha, matumizi bora ya ardhi iliyopo kwa kuzingatia
uwiano baina ya ardhi na mifugo iliyopo. Tunawajibika kupima ardhi yetu
kuanzia ngazi ya vijiji ili kuepusha athari zinazotokana na kuzidisha
mifugo katika maeneo tuliyonayo ikiwemo eneo la Mto Mara.
“Kupima
ardhi kutasaidia kuepusha migogoro inayoweza kutokea baina ya wakulima
na wafugaji. Tutaendelea na mikakati ya kutoa elimu ya kutosha kwa
wananchi ili wafuge kisasa na kupunguza idadi ya mifugo ili kuepuka
uharibifu wa mazingira,” alisema.
Alisema
bonde la mto Mara ni rasilmali kwa wakazi wa Mara na kwamba kama bonde
hilo likitumiwa vizuri lina fursa kubwa ya kiuchumi na hasa kwenye
kilimo cha umwagiliaji maji.
Alisema
wastani wa pato la mwananchi wa Mara liko chini ikilinganishwa na mikoa
jirani ya Mwanza, Manyara na Shinyanga na kwamba kilimo cha umwagiliaji
kwa mazao kama mpunga na mbogamboga kitasaidia kuinua pato la wananchi
wa mkoa huo.
“Ili
kulitunza bonde hili ni lazima tuache kazi za kilimo umbali wa mita 60
kutoka kingo za mto huu kwa mujibu wa sheria. Tuache kuchoma misitu,
tuache kukata miti hovyo, na kama mnataka kufanikiwa, nawashauri mfuge
nyuki. Mkiwa na mizinga yenu kwenye misitu hamtachoma moto, ni lazima
mtajizuia kuchoma moto ili msiwadhuru nyuki wenu,” alisema.
Alisema
bonde la mto Mara ni fursa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi hivyo wakazi
wa bonde hilo wa pande zote mbili hawana budi kulitunza kwa faida ya
kizazi cha sasa na cha baadaye.
Aliwaomba viongozi wa Tanzania na Kenya kushirikiana kulitunza bonde hilo na kuhakikisha kwamba Mto Mara unadumu.
“Mto
Mara ni mto wenye historia, ni mto wa kumbukumbu, ni mto wa shughuli za
kiuchumi na shughuli za maendeleo. Lakini zaidi ya yote, mto Mara
unaunganisha jamii za pande zote mbili Kenya na Tanzania. Tutumie mto
Mara kama alama (Symbol) ya chanzo cha umoja wetu, mshikamano, udugu na
upendo kati ya wananchi wa Kenya na Tanzania na hata nchi zote za maziwa
makubwa zinazotumia Ziwa Victoria,” alisema.
Maadhimisho
hayo yalihudhuriwa na Naibu Mawaziri wa Maji, Maliasili na Utalii na
TAMISEMI pamoja na viongozi kadhaa kutoka Serikali ya Kenya. Pia wakuu
wa mikoa ya Arusha, na Manyara, na wakuu wa wilaya mbalimbali.
No comments:
Post a Comment