Katika
hali isiyokuwa ya kawaida wilayani hapa, Mkoa wa Geita, watu
wasiojulikana wamefukua kaburi la mtu aliyekufa na kuzikwa katika
makaburli ya mtaa wa Elimu Nyantorotoro, kisha kukata kichwa chake na
kuondoka nacho kusikojulikana.
Tukio
hilo limekuja siku chache wakati wakazi wa Wilaya ya Geita wakiwa na
hofu baada ya kutokea tukio la mtoto Shaabani Maulidi (16) aliyefariki
miaka zaidi ya miwili iliyopita na kuonekana akiwa hai jirani na mtaa
huo.
Katika tukio
hilo ambalo limekusanya umati mkubwa wa wakazi wa mji wa Geita,
lilitokea jana baada ya watu kukuta jeneza la maiti likiwa limefukuliwa
na kupasuliwa na baadae kutoa kichwa cha maiti hiyo ya mwanaume (jina
halijafahamika), kisha kuondoka nacho na kuliacha kaburi likiwa wazi.
Akizungumza na NIPASHE jana, Mwenyekiti wa Mtaa wa Elimu Nyankumbu,
Hassan Malima, alisema tukio hilo liligunduliwa saa tatu asubuhi na watu
walioenda eneo hilo kuchimba kaburi baada ya kutokea msiba kwa
mchungaji Mtafuteni Mihana, wa kanisa la Pefa, aliyefiwa na mtoto wake.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, maiti hiyo ilizikwa takribani miezi mitatu iliyopita.
Hata hivyo, ndugu na jamaa wa karibu wa marehemu huyo hawakupatikana haraka kuzungumzia tukio hilo.
Malima alisema baada ya kupata taarifa za tukio hilo linalohusishwa
na imani za kishirikina, walitoa taarifa polisi ambao walifika haraka
katika eneo hilo wakiongozwa na mkuu wa polisi wilaya ya Geita, OCD
Bwire.
Baada ya kufanyika uchunguzi wa kitabibu uliofanywa na Dk. Alex Makonda, alibainisha kuwa marehemu huyo alikuwa ni mwanaume.
Naye mchungaji wa kanisa la Pefa, katika mtaa huo, Mchungaji
Mtafuteni alisema tukio hilo limetokana na imani za kishirikina na
kwamba imesababishwa na watu kukosa hofu ya Mungu.
No comments:
Post a Comment