Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, October 9, 2013

MRATIBU MISS UTALII 2013 ADAIWA KUDHALILISHA WASHIRIKI.



Miss utalii Tanzania 2013, Hadija Mswaga (kushoto) akiingia kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana, kuelekea Equatorial Guinea kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Dunia ya Miss Tourisim World 2013, pembeni ni mshindi wa tatu, Teresia Kimolo. aliyemsindikiza (Picha na Hosea Joseph)
BARAZA la Sanaa la Taifa (Basata), limempa karipio kali Mwenyekiti wa shindano la Miss Utalii, Gideon Chipungahelo kwa kosa la kudhalilisha baadhi ya washiriki na malalamiko kufanyiwa kazi na Baraza hilo.
Karipio hilo lilitolewa baada ya Basata kupitia tathmini iliyohusisha vipande vya matukio yaliyorekodiwa (clips) na kujionea namna wasichana wanavyofanyiwa vitendo vya udhalilishaji na Chipungahelo kwa kipindi cha kambi ya miezi mitatu.
Katika hafla ya upitiaji wa clips hizo uliofanyika mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Basata, Ilala, jijini Dar es Salaam mbele ya Chipungahelo, ilionekana wazi wasichana kukosa uangalizi walipokuwa kambini, hivyo kuwepo kwa matukio mbalimbali yasiyofaa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa kitengo cha Sanaa wa Basata, Nsao Shaluwa alisema baada ya kupata malalamiko kuwa wasichana wanafanyiwa mambo yasiyofaa wakiwa kambini, waliamua kuutafuta ukweli na kujiridhisha shindano hilo lina ukakasi mwingi.
Alisema baada ya kukusanya baadhi ya matukio katika kuthibitisha hali halisi iliyopo kwenye shindanohilo, watapeleka vielelezo kwa Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana Michezo na Utamaduni ili Chipungahelo ajadiliwe kwa kosa la kudhalilisha warembo wa shindano hilo.
Alisema kwa kukosa matroni, yaelezwa warembo walikuwa wakizurula kutwa nzima hadi usiku kwenye gari huku kukiwa hakuna ratiba ya chakula ya kueleweka huku wakifanyishwa mazoezi muda mrefu.
Mbali ya muda mrefu kuanzia saa 2 usiku hadi 9, pia walikuwa wakivaa viatu virefu, hivyo miguu kuvimba na wakati mwingine walikuwa wakichapwa makofi na kulazimishwa mapenzi.
Aidha, Chipungahelo anakabiliwa na shutuma ya kuwaweka mabini washiriki kwa muda wa miezi mitatu tofauti na alivyoeleza Basata kuwa kambi ni ya wiki tatu.
Zaidi ya hapo, Chipungahelo alishindwa kutoa zawadi kwa washindi wala kifuta jasho kwa washiriki wengine huku mshindi wa mwaka 2013, akidaiwa kubebwa kwa hila.
Shaluwa alisema baada ya malalamiko hayo kufikishwa kwao, waliamua kunyatia katika kambi yake iliyokuwa na warembo saba ambayo pia Chipungahelo aliwaficha.
Baada ya kuwahoji washiriki, walikiri kwamba walikuwa wakilala warembo saba, wengine watano katika chumba kimoja na wengine wakilala chini huku wakila mlo mmoja tena katika muda usiofaa.

“Warembo wengi wamekiri walikuwa wakifanyishwa mazoezi kwa muda mrefu huku wakiwa wamevaa viatu virefu,
“Tulikuwa tukifanyishwa mazoezi kuanzia saa mbili usiku hadi saa tisa, tuna njaa na tulipolalamika, baba alitutukana matuzi ya nguoni na kukashifu tupu zetu” mmoja wsa warembo alisema katika CD ya Basata.
Shaluwa anasema walipofika Ikondolelo ambako kulikuwa na kambi ya awali, walizungumza na warembo hao, lakini wakishindwa kusema ukweli mbele ya Chipungahelo.
Alisema walipowapa karatasi kuandika kero zao, kila mtu aliandika jina na kusaini ambapo walieleza mengi yaliyorekodiwa na wadau kuoneshwa mwishoni mwa wiki mbele ya mwanasheria Ashura Mzava kutoka TAWLA.
Mzava alisema wazi kwa madudu yaliyopo kwenye shindano hilo, Chipungahelo anapaswa kushtakiwa kwa udhalilishaji.
Kashfa nyingine ni kitendo cha Chipungahelo kutumia kiasi cha sh 200,000 ambazo zilitolewa na Mkuu wa Wilaya Tanga Mjini, Halima Dendego ili washiriki waende saloon kabla ya fainali.
“Baba ametunyanyasa sana hadi, ametumia pesa tuliyopewa na mama Halima Dendego, lakini hapohapo amekuwa akimpendelea mshiriki mwenzetu (jina tunalo), kwa vile alikuwa na uhusiano naye wa kimapenzi,” alisema mmoja wa washiriki na kuongeza:
“Hata siku ile ya fainali, alipokuja mpambaji kutoka Sofia Record, alimuita na kumvalisha nguo nzuri pamoja na kumpamba tofauti na alivyovalisha washiriki wengine” wamesema washiriki hao.
Wakati huohuo Mkurugenzi Msaidizi wa Sanaa kutoka Wizarani, Leah Kihimbi alisema atalifikisha kwa usahihi suala hilo katika ngazi ya juu akimtaka Chipungahelo ajitayarishe kwa maamuzi yoyote.
Mshiriki pekee wa Miss Utalii 2013 aliyefika kwenye tahmini hiyo, ni Glory John aliyesema wazi shutuma zote zilizoelezwa na wenzake dhidi ya Cipungahelo ni kweli.
“Tulipokuwa tunakwenda Mikumi , tulilala Morogoro, Baba (Chipungahelo) aliniita akaniambia nipande juu katika chumba kimojawapo, nilipokwenda na kufungua mlango, nikakutana na moshi wa ajabu nikashindwa kuvumilia nikatoka.
Akanifuata akinitaka nirudi chmbani mle, nikagoma, nilipowaeleza wenzangu, walinieleza nilielekea kunaswa kwenye mtego wake,” alisema Glory.
Naye Katibu Mtendaji BASATA Godfrey Mngereza alisema, hilo ni suala nyeti linalogusa jinsia ya kike, hivyo ni hatari kwa ustawi wa jamii.
Kupitia tathmini hiyo ya aina yake, Basata itachunguza mazingira ya ushindi wa Miss Utalii mwaka 2013, ikibainika hakustahili, atavuliwa taji hilo ili iwe fundisho.
“Tabia hizi chafu zinatuchafua hata sisi BASATA tunaonekana hatufanyi kazi sasa ndio tutaanza na Miss Utalii na ikibidi kusiwe na shindano la aina yeyote kama mambo yenyewe ni kudhalilishana,” alisema Mngereza.
Wadau wengine waliohudhuria tathmini hiyo ni kutoka TAMWA, TAWLA,TGNP,THAWE, Polisi Jamii, Polisi kutoka kituo cha Pangani Ilala, Dar es Salaam, Shirikisho la Sanaa na Ufundi, Binti Leo na wengineo.

Shaluwa alisema suala hilo litapelekwa ngazi za juu na vielelezo kuonesha wasichana wakieleza yanayotokea kambini pamoja na maoni ya wadau yaliyorekodiwa.
Akizungumnzia tuhuma dhidi yake, Chipungahelo alisema ni majungu yaliyopikwa na maadui zake ambao walimpandikizia makahaba kwa lengo la kuchafua taswira ya shindano
hilo ili kummaliza, lakini aliomba radhi kwa dosari na mapungufu yaliyojitokeza na kuahidi kuwa hazitajirudia tena.

No comments:

Post a Comment