Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Sunday, October 27, 2013

Rais wa Bunge la Uswisi aelezea mabilioni, magazeti Dar kufungiwa



Rais wa Bunge la Uswisi, Maya Graf (wa nne kushoto) akizungumza na waandishi wa habari wa magazeti ya Mwananchi na The Citizen katika mahojiano maalumu, jijini Dar es Salaam. PICHA | EMMANUEL HERMAN 

Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd kupitia magazeti yake ya Mwananchi na The Citizen, yalipata fursa pekee ya kumuhoji Rais Maya Graf, kuhusiana na masuala mbalimbali ikiwamo madhumuni ya safari yake, mabilioni hayo, uwazi wa mishahara ya viongozi wa juu serikalini na uhuru wa vyombo vya habari. Mwandishi wetu, Noor Shija alikuwa mmoja wa walioshiriki kufanya mahojiano na kiongozi huyo wa kitaifa na yafuatayo ni mahojiano hayo:
Swali: Nini madhumuni ya safari yako na hii ni mara yako ya kwanza kutembelea Afrika na hasa Tanzania?
Jibu: Hii siyo mara yangu ya kwanza kutembelea Afrika, mara ya kwanza kuja Afrika ilikuwa mwaka 2011, nilitembelea nchi ya Senegal. Lakini kwa Tanzania ni mara yangu ya kwanza na kwa wadhifa wangu wa Rais naruhusiwa kusafiri nje ya nchi.
Na mimi nilichagua Tanzania kwa sababu ya uhusiano mzuri kati ya Uswisi na Tanzania uliodumu kwa miaka mingi. Kuna raia wengi wa Uswisi wanaoishi Tanzania, pia tunasaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile hospitali ya Ifakara (Morogoro), ambayo nimeitembelea.
Pia tunashiriki katika uendelezaji wa miradi mingine mbalimbali kama vile sekta ya kilimo, makazi na masuala mengine yanayohusiana na Serikali. Nikiwa Rais wa Bunge ni muhimu kwangu kuthibitisha fedha tunazosaidia Tanzania kama zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Swali: Ulikutana na Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda. Mazungumzo yenu yalilenga maeneo gani na nini matokeo ya mkutano wenu?
Jibu: Kwanza nilifurahi kuonana na Spika, kwa kuwa sote ni wanawake katika nafasi ya uongozi unaofanana, mazungumzo yetu yaliegemea sana kuhusu nafasi za wanawake katika uwakilishi wa uongozi wa kisiasa.
Tulizungumza kuhusu kanuni na taratibu za mabunge yetu, pia tulizungumza kuhusu changamoto tunazokabiliana nazo.
Pia tulizungumza kuhusu idadi ya wanawake ndani ya Bunge na umuhimu wa wanawake kushika nafasi za uongozi katika sekta ya elimu, sekta ya uchumi na katika ngazi za juu za uongozi. Hayo ndiyo tuliyozungumza.
Swali: Nchi yako imekuwa na uhusiano wa muda mrefu na Afrika, na hasa Tanzania katika masuala ya Bunge, diplomasia na misaada ya maendeleo. Kwa kifupi unaweza kuelezea uhusiano wa masuala ya Bunge na hasa katika kubadilishana uzoefu?
Jibu: Tuna uhusiano wa muda mrefu hasa katika ngazi ya kibunge, tumekuwa tukifanya kazi pamoja katika masuala ya umoja ya kibunge (Inter-Parliamentary Union-IPU), ambapo *fanyika Geneva, Uswisi, hivi karibuni Anne Makinda alihudhuria, lakini hatukubahatika kuonana.
Masuala mengine ni kama vile misaada ya kimaendeleo ambayo imeimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Uswisi, mfano miradi iliyopo Dodoma na Ifakara (Morogoro).CHANZO MWANANCHI

No comments:

Post a Comment