Askari
kumi wa Misri wameripotiwa kuuawa na wengi kujeruhiwa kutokana na
kulipuliwa na bomu karibu na mji wa el-Arish kaskazini mwa Sinai nchini
Misri.
Gazeti la
Al-Masri al-Youm limesema msafara wa mabasi yakiwa yamebeba askari wa
miguu ulipigwa na bomu lililokuwa limetegwa kando ya barabara wakati
msafara huo ukielekea katika eneo la Kharouba.
Mashambulio
dhidi ya askari wa usalama katika eneo la Sinai, kaskazini mwa Misri
yameongezeka tangu Rais Mohammed Morsi ang'olewe madarakani mwezi Julai
mwaka huu.Idadi ya watu waliouawa katika shambulio hilo huenda
ikaongezeka, imesema taarifa ya vyombo vya usalama.
Hali ya
usalama katika eneo hilo imezidi kuzorota katika miaka ya karibuni,
ikichochewa na kuangushwa kwa Rais Hosni Mubarak. Kuondolewa kwake
madarakani mwezi Februari 2011 kulisababisha eneo la kaskazini mwa Sinai
kulengwa na vikundi vya wapiganaji, vikundi vingine vikihusishwa na
wapiganaji wa ukanda wa Gaza, huko Palestina.
Mwezi
Septemba, majeshi ya usalama yalianzisha mashambulio dhidi ya wapiganaji
wa Kiislam huko Sinai, lakini majeshi hayo yalikabiliwa na mashambulio
makali ya mabomu.
Shambulio
la Jumatano, ambalo lilitokea saa 01:45 asubuhi kwa saa za huko katika
barabara inayotoka Rafah kwenda el-Arish, linafikiriwa kuwa shambulio
baya kabisa kufanyika dhidi ya jeshi la Misri tangu Bwana Morsi
aondolewe madarakani.
Tovuti ya gazeti la al-Ahram imeripoti kuwa askari 26 wamejeruhiwa katika mlipuko huo.
Shambulio
hili limeripotiwa kulenga askari wa kikosi cha jeshi la Misri, ambao
wametumwa katika eneo la Sinai na wamehusika katika operesheni ya
kuharibu njia za chini ya ardhi zilizopo kati ya mpaka wa Misri na
ukanda wa Gaza.
Askari
walioshambuliwa walikuwa wakirejea Cairo kuanza likizo zao. Baadhi ya
askari waliojeruhiwa vibaya, walichukuliwa kwa ndege kupelekwa katika
hospitali, mjini Cairo.
No comments:
Post a Comment