CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Bunda
kimepata pigo la kuondokewa na Diwani wake wa Kata ya Nyasura, Zamberi
Mwisarya (68).
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Kaimu Katibu wa
CHADEMA wilayani hapa, Samweli Alfred, alisema kuwa diwani huyo
alifariki dunia juzi saa mbili usiku katika Hospitali ya Bugando jijini
Mwanza alikokuwa amelazwa.
Alisema kuwa wamepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo na kwamba
wameondokewa na kiongozi shupavu ambaye alikuwa akitetea wananchi wa
Kata ya Nyasura na kwamba chama kimeondokewa na mpiganaji wa kweli.
Naye Katibu Mwenezi wa kata hiyo, Benjamin Kasonde, alisema kuwa
wananchi wa kata hiyo walikuwa wakimtegemea sana diwani wao katika mambo
mbalimbali na kwamba alikuwa ni mtetezi wao katika masuala mbalimbali
ya maendeleo.
Mtoto wa marehemu, Mgendi Ngabayi, alisema kuwa baba yake alikuwa
akisumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi tangu mwaka jana na kupelekwa
Bugando kwa matibabu kisha alipata nafuu lakini baadaye mwaka huu hali
yake ilirudia kuwa mbaya, hivyo waliamua kumrudisha huko tena kwa
matibabu hadi juzi alipokutwa na mauti.
Alisema kuwa mazishi yalitarajiwa kufanyika jana katika makaburi ya Nyasura saa kumi jioni.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Joseph Marimbe, alisema kuwa
ameshutushwa na msiba huo kwani diwani huyo alikuwa ni mmoja wa madiwani
mashuhuri na kwamba halmashauri imepoteza mmoja wa madiwani wake.
No comments:
Post a Comment