Winnie
Madikizela-Mandela, (77) aliinama kumbusu Graca Machel (68), kabla ya
kukaa katika kiti cha tatu kutoka kile alichokalia mwanamke huyo. Graca
Machel alimwambia maneno machache ‘dada yake’ Winnie wakati akimbusu.
Wanawake
hao wote wakiwa wamevalia majaketi meusi na vilemba, walikumbatiana kwa
sekunde kadhaa huku Winnie akitabasamu na Graca akitazama mbele.
Wote
wawili wanaheshimika nchini Afrika Kusini kutokana na sababu
mbalimbali. Winnie anaheshimika kwa mchango wake mkubwa wa kupigania
ubaguzi wa rangi; Graca kwa moyo wake wa kujitolea kumtunza kiongozi wao
mpaka anafariki dunia.
Hata
hivyo Winnie amekuwa akikosolewa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo
ile ya kuruhusu wapinzani wake wauawe kwa kuchomwa moto wakitumia mafuta
ya petroli na matairi ya magari.
Mwaka
1988 alipatikana na hati ya kumuua kijana wa miaka 14 ambaye ilidaiwa
alimtuhumu kuwa kibaraka, hata hivyo hukumu yake ilipunguzwa kutoka kuwa
kifungo cha miaka sita jela na kuwa faini.
Winnie
pia anatuhumiwa kwa kutokuwa mwaminifu katika ndoa yake iliyodumu kwa
miaka 38 ingawa 27 kati ya hiyo hakuwa na mumewe ambaye alikuwa
akitumikia kifungo katika gereza la Robben.
Graca
Machel alifunga ndoa na Mandela wakati wa sherehe yake ya kutimiza
miaka 80. Pamoja na kuwa Winnie na Mandela walitengana, katika kipindi
cha ugonjwa wake kilichodumu kwa siku 181, alikuwa akimtembelea mara kwa
mara.
Mjane
wa Mandela, Graca,ambaye pia ni mjane wa Rais wa zamani wa Msumbiji,
Hayati Samora Machel, alitumia muda wote kuwa pembeni mwa kitanda cha
Mandela mpaka alipokata roho.
Ndugu
wa karibu wanasema, daktari aliposema hakuna kitu kinachoweza kufanyika
kuokoa uhai wa Mandela, Winnie alifika nyumbani hapo na alikuwepo muda
wote mpaka kiongozi huyo alipokata roho.
Tangu
Mandela afariki, Winnie amekuwa akionekana sana tofauti na Graca.
Jumapili ya wiki iliyopita, ikiwa ni siku tatu tangu Mandela afariki,
Winnie alikwenda kusali katika kanisa ambalo lilikuwa likifanya misa kuu
ya kitaifa kumuombea Mandela .
Winnie
alikaa pembeni ya Rais Jacob Zuma. Hata hivyo siku yake iliharibia na
Mchungaji, Mosa Sono aliyekuwa akiongoza ibada hiyo baada ya
kumtambulisha kwa jina la Graca. Kwa upande wake Graca alisali katika
kanisa dogo lililopo karibu na nyumba ya Mandela.
Graca ni mdogo wangu
Kwa
muda mrefu sasa Winnie amekuwa akisisitiza kuwa hakuna uhasama baina
yake na Graca na anamuona kama mdogo wake kwa kuwa kiumri pia amemzidi.
Winnie
aliwahi kunukuliwa akisema: “Namuita mdogo wangu, na yeye huwa ananiita
dada, hata tunapozungumza huwa maongezi yanamuhusu mume wetu,” anasema
Winnie.
Dunia yamuaga Mandela kwa heshima ya kipekee
Dunia
imeamua kumpa heshima ya kipekee Nelson Mandela kwa mkusanyiko wa aina
yake wa kumuaga kwenye kitongoji cha Soweto, ambapo zaidi ya viongozi
100 wa dunia wanahudhuria ibada hiyo.
Tangu
viongozi walioko madarakani mpaka waliostaafu, halijawahi kushuhudiwa
kuwa na watu wengi kiasi hiki; zaidi ya watu 95, 000 wamefurika uwanjani
tangu usiku wa manane kuhakikisha wanapata nafasi.
Kitongoji
hicho cha Jonnesburg ndiko alikokuwa akiishi Mandela kabla ya kukamatwa
na kuwekwa gerezani kwa miaka 27, kwa hivyo ni mahala pa kihistoria
kutoa heshima za mwisho kwa shujaa huyo wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa
rangi.
Kiasi
cha viongozi 100 wanahudhuria, wakiwamo wa mataifa na Serikali, wafalme
au warithi wao, achilia mbali watu wengineo mashuhuri duniani ikiwa ni
pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.
Wengine
ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini
Zuma, na wajumbe wa Baraza la Wazee la Kimataifa aliloliunda mwenyewe
Nelson Mandela, akiwamo Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter.
Marekani
inawakilishwa na Rais Barack Obama na mkewe pamoja na marais wa zamani,
George W. Bush na Bill Clinton na mkewe, waziri wa zamani wa mambo ya
nchi za nje, Hillary Clinton.
Viongozi
wengine ni pamoja na Rais Raul Castro wa Cuba, Hamid Karzai wa
Afghanistan, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, na Mwana wa mfalme
Charles, Rais Pranab Mukhrejee wa India, Rais Dilma Russels wa Brazil
na watangulizi wake wanne ikiwa ni pamoja na Lula da Silva,
Waziri
mkuu wa Italia Enrico Letta, Kiongozi wa Mamlaka ya Utawala wa Ndani wa
Palestina, Mahmoud Abbas na mawaziri wakuu wa Norway, Sweden na Canada,
kwa kuwataja wachache tu.
China
inawakilishwa na Makamu wa Rais, Li Yuanchao huku Japan ikiwakilishwa
na mrithi wa kiti cha mfalme, Mwanamfalme Naruhito. Ujerumani
inawakilishwa na Rais Joachim Gauck. Takriban viongozi wote wa bara la
Afrika wanahudhuria pia ibada hiyo.
Ibada kuendelea
Ibada kadhaa nyingine zinafanyika hadi siku ya mazishi ya Mandela katika kijiji walichotokea wazee wake, Qunu, Desemba 15.
Mbali
na ibada rasmi ya mazishi, maiti ya Nelson Mandela imewekwa katika
Ikulu kuanzia Jumatano hadi ijumaa itakaposafirishwa kwa ndege hadi
Mashariki ya Cape Town kwa mazishi.
Hatua za ulinzi zimeimarishwa. Afrika Kusini inauzoefu kutokana na maandalizi ya Kombe la Dunia la mwaka 2010.
Waziri wa Ulinzi, Nosiviwe Mapisa-Nqakula, amesema,”Kila kitu kiko tayari, tumejiandaa tangu miaka mitatu au minne iliyopita.”
Makala hii imeandikwa na Julieth Kulangwa kwa msaada wa vyombo vya habari.
MWANANCHI


No comments:
Post a Comment