Mkurugenzi wa zamani wa Utawala na Utumishi (DPA), Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), Amatus Liyumba, akitinga Mahakamani. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa zamani wa Utawala
na Utumishi (DPA), Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba
anayekabiliwa na kesi ya kukutwa na simu gerezani, ameiomba mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu imfutie shtaka hilo na kumuachia huru kwa madai kuwa
kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kumkomoa.
Liyumba aliyaeleza hayo jana wakati akijitete
mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando anayetarajia kutoa hukumu ya
kesi hiyo, Januari 15, mwaka na kuzitaka pande zote mbili kuwasilisha
majumuisho yao ya mwisho kama mshtakiwa ana hatia ama la, Desemba 30,
mwaka huu .
“Kesi hii imepangwa kwa ajili ya kunikomoa, wakati
natumikia kifungo sijawahi kuvunja sheria, kupewa adhabu wala kuonywa
kwa kosa lolote, simu yenye namba 0653004662 siijui nimeiona hapa na
kama imesajiliwa ni lazima mhusika atajulikana.” alieleza Liyumba.
Alidai kuwa, Julai 2011 alikuwa mfungwa akitumikia
kifungo cha miaka miwili na unapofikishwa huko ni lazima upekuliwe mara
tatu kwa kuvuliwa nguo zote.
Kutokana na utaratibu wa ulinzi gerezani, siyo rahisi kwa mfungwa ama mahabusu kuingia na simu
Julai 27, 2011 mchana nikiwa kwenye selo yangu na
mtu mmoja ambaye ni mahabusu, tukisoma magazeti ghafla askari wawili
akiwamo shahidi wa pili wa upande wa mashtaka, waliingia na kuniambia
kuwa hii simu umeipataje wakati wakiwa wameishika mkononi.
Aliongeza kuwa tukio hilo kwake lilikuwa ni
mshtuko na aliona ni kitu kilichopangwa na kwamba, wakati huo ilikuwa
bado mwezi mmoja na nusu amalize kutumikia kifungo chake.
“Naamini walikuwa wananingojea, nilitafakari
mlolongo wa matukio yanayonikuta, nilishtakiwa kwa kuambiwa
nimesababisha harasa ya Sh261 bilioni shtaka ambalo liliondolewa na
kupewa la kutumia madaraka vibaya, madaraka ambayo sina wala sijapewa
huu ni uonevu.” alisema Liyumba.
Alibainisha kuwa wakati akiwa gerezani muda mfupi
kabla ya kutoka watu wa Takukuru walimfuata na wakitaka kuandaa kesi
dhidi yake, lakini aliwapinga kwa madai ya kutaka kuwasiliana na
mwanasheria wake.
Alidai kuwa watu hao walimfuata tena na kwamba
baada ya dulu hilo, akaona tukio hili la Julai 27,2011 la kubambikiwa
kesi ya kukutwa na simu gerezani.
Alisisitiza kuwa simu na namba ya 0653004662
haifahamu, kama imesajiliwa mhusika atajulikana na iwapo atakuja
mtaalamu ataeleza angalau ilipigwa kwa nani.
Liyumba anadaiwa kukutwa na simu ya mkononi akiwa gerezani Ukonga, Dar es Salaam, wakati akitumikia kifungo cha miaka miwili.CHANZO MWANANCHI

No comments:
Post a Comment