Elias John, mkazi wa Kigamboni jijini Dar, (28) baada ya kupofuka macho.
Na Imelda Mtema/ GPL
Katika hali ya kusikitisha sana, kijana mmoja Elias John, mkazi wa
Kigamboni jijini Dar, (28) amejikuta katika wakati mgumu wa kupofuka
baada ya kuchomwa sindano inayodaiwa kuwa na sumu kufuatia kujihusisha
kimapenzi na mwanamke anayedaiwa kuwa ni mke wa askari Polisi.
Alisema baada ya kuchomwa sindano hiyo, askari hao walimtaka aondoke na
akajitahidi kuwapa taarifa ndugu zake, ambao walimchukua na kumpeleka
Muhimbili ambako hata hivyo walishindwa kumsaidia na hata alipopelekwa
CCBRT, pia ilishindikana.
Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Elias alidai alikumbwa
na mkasa huo mwaka 2011 wakati akiwa na uhusiano wa kimapenzi na
mwanamke aliyemtaja kwa jina moja la Amina, ambaye pia alijihusisha na
polisi aliyemtaja kwa jina moja la James, aliyekuwa akifanya kazi katika
kituo cha Polisi cha Kilwa Road, jijini Dar es Salaam.
“Polisi huyo alikuwa akinifuata mara kwa mara na kuniambia kuwa niachane
na mwanamke huyo, lakini kwangu ilikuwa ngumu kwa sababu tulipendana
sana,” alisema kijana huyo.
Alisema siku ya tukio, akiwa kijiweni, polisi huyo akiambatana na
wenzake, walifika na kumkamata bila kosa lolote na kumpeleka katika
kituo kidogo cha polisi Mianzini, Temeke.
Wakiwa kituoni hapo, kijana huyo alisema kwa pamoja Polisi hao
walimshika mikono na miguu wakati James alichukua sindano na kumchoma.
Akiwa hajui hatima yake, Elias alisema mara tu baada ya kuchomwa sindano
hiyo, alisikia maumivu makali yaliyopanda hadi kichwani na ghafla
akapoteza uwezo wake wa kuona.
“Siwezi kuelezea zaidi maumivu niliyoyapata baada ya kuchomwa sindano
ile na hapo hapo macho yangu hayakuweza kuona tena licha ya kujitahidi
sana,” alisema.
Katika hali ya kusikitisha zaidi, ndugu zake walijaribu kufuatilia suala
hilo polisi, lakini walipofika waliambiwa kirahisi kwamba askari hao
wote walishafukuzwa kazi.
Alisema juhudi za ndugu zake kuhakikisha haki inatendeka zimegonga
mwamba licha ya suala lake kufikishwa kwa taasisi za haki za binadamu
ambako bado linashughulikiwa, ingawa hakuna matumaini ya kupatikana kwa
ufumbuzi.
“Maisha yangu yamekuwa magumu sana na sijui hatma ya kesi yangu,
nitaendelea kuishi hivi mpaka lini? Kwa vile kwa sasa naombaomba tu,”
alisema.
Alitumia fursa hiyo kumuomba Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuliangalia suala lake kwa undani ili lipatiwe ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment