Rais Jakaya Kikwete
---
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za
Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Lt(Mst) Chiku Galawa kufuatia vifo
vya watu 12 na wengine 71 kujeruhiwa baada ya basi Na. T610 ATR la Kampuni ya
Burudani lililokuwa likitokea Korogwe kwenda Dar es Salaam kupinduka katika
Kijiji cha Taula mapema asubuhi ya tarehe 12 Desemba, 2013.
“Nimepokea kwa mshtuko
na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu 12 vilivyotokea tarehe 12
Desemba, 2013 huku wengine 71 wakijeruhiwa, baada ya basi la Kampuni ya
Burudani walilokuwa wakisafiria kutoka Korogwe kuelekea Dar es Salaam kupinduka
katika Kijiji cha Taula”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake.
Rais Kikwete amesema
vifo vya watu hao ni pigo kubwa siyo tu kwa familia za watu waliopoteza ndugu
zao katika ajali hiyo, bali pia Taifa letu kwa ujumla ambalo limepoteza nguvu
kazi muhimu iliyokuwa bado inahitajika kwa ujenzi wa Taifa.
“Kutokana na msiba huo
mkubwa uliotokea katika eneo la Mkoa wako, ninakutumia Salamu za Rambirambi
kutoka dhati ya moyo wangu wewe Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Lt. (Mst)
Chiku Galawa kwa kupoteza watu wengi kwa mara moja katika ajali hiyo.
Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Mahala Pema
Peponi Roho za Marehemu wote, Amina”.
Rais Kikwete amemuomba
Mkuu wa Mkoa wa Tanga kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na pole nyingi kwa
familia, ndugu na jamaa waliopotelewa na wapendwa wao katika ajali hiyo, lakini
amewahakikishia kwamba yuko pamoja nao katika kipindi hiki cha
maombolezo. Amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu, ujasiri na subira katika
kipindi hiki kigumu wanachopitia wakiomboleza vifo vya ndugu zao.
Aidha Rais Kikwete
amesema anawaombea kwa Mwenyezi Mungu majeruhi wote wa ajali hiyo waweze kupona
haraka na kurejea katika hali zao za kawaida, ili waungane tena na ndugu na
jamaa zao na kuendelea na maisha yao kama ilivyokuwa kabla ya kutokea kwa
ajali.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
12 Desemba, 2013
No comments:
Post a Comment