Msikiti mkongwe wa Chake Chake, Pemba. |
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema Rasimu ya Mahakama ya Kadhi imekamilika
na inatazamiwa kuwasilishwa katika ngazi za makatibu wakuu kabla ya
kufikishwa kwenye Baraza la Mapinduzi.
Waziri wa
Sheria na Katiba, Abubakar Khamis Bakary, alisema jana kuwa Rasimu hiyo
ambayo inasubiriwa kwa hamu na makundi ya watu wakiwamo wanaharakati
baada ya kupata baraka za Baraza la Mapinduzi itawasilishwa kwenye
Baraza la Wawakilishi mwakani.
Alisema
Rasimu hiyo imeandaliwa kwa ajili ya kuboresha mfumo wa kuendesha
Mahakama za Kadhi ili uwe na ufanisi na kutatua migogoro ikiwamo ya ndoa
kwa Waislamu.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mdungi Ussi, alisema Rasimu
hiyo ina lengo la kuimarisha na kuweka mfumo mzuri wa kuendesha mahakama
za kadhi nchini.
Alisema
kwa muda mrefu yapo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu muundo
wa Mahakama ya Kadhi na utaratibu wa kuendesha kesi na kutoa uamuzi.
"Rasimu
ya Mahakama ya Kadhi kwa kiasi kikubwa itaondoa malalamiko yaliyokuwapo
awali ikiwamo wanaume kutelekeza wake na matunzo ya watoto," alisema.
Miongoni
mwa mambo ambayo yalijadiliwa kwa kina likiwamo suala la wanawake kupata
mgawo wa mali wanapoachwa na waume zao na suala la matunzo ya watoto,
ambapo kwa kawaida mwanamke anapopewa talaka huachiwa malezi ya watoto.
Kwa mujibu wa utafiti lipo wimbi kubwa la talaka na tatizo la wanawake kutelekezwa na waume zao na watoto.
Katika
mkoa wa Kaskazini Unguja mwaka 2012/13 talaka 53 zilitolewa huku
wanawake wakitelekezwa na waume zao na watoto kwa mujibu wa karani ya
Mahakama ya Kadhi Mkokotoni, Asma Francis.
Aidha,
kesi 10 za wanawake kutelekezwa na kudai matunzo ya watoto zilifikishwa
katika Mahakama ya Kadhi ili kupata ufumbuzi huku wanaume wawili
wakikubali kutoa fedha za matunzo ya watoto.
No comments:
Post a Comment