Januari
26 na 27 ya kila mwaka chama cha upinzani cha wananchi CUF, huadhimisha
kumbukumbu ya maandamno ya kudai demokrasia zaidi katika visiwani
Zanzibar yaliyofanyika mwaka 2001. Wafuasi kadhaa wa chama hicho
waliuwaa na wengine kujeruhiwa katika maandamano ya kupinga matokeo ya
uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 katika mapambano na polisi.
Uchaguzi
mkuu wa mwaka 2000 katika visiwa vya zanzibar uligubikwa na utata
uliozusha vurugu kubwa na maandamano kutoka chama cha CUF kikidai
kuporwa ushindi wao katika uchaguzi uliomweka madarakani wakati huo,
Rais Aman Abeid Karume hivyo kutaka urudiwe.
Kamati
maalum iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania wakati huo
Benjamn Mkapa kuhusiana na uchunguzi wa vurugu hizo iliyoongozwa na
Brigedia Jenerali Hashim Mbita, ilibaini kwamba watu takribani 23
walipoteza maisha wakati wa maandamnao hayo ya wafuasi wa CUF ambapo pia
kwa mara ya kwanza Tanzania ilizalisha wakimbizi kwa baadhi ya watu
kukimbilia mjini Mombasa na kwingineko kukwepa vuruga hizo.
Akizungumza
na Sauti ya Amerika jijini Dar es salaam Jumatatu Mkurugenzi wa
Mipango, Uchaguzi na Bunge wa chama cha wananchi CUF, Shaweji Mketto,
alikumbusha kwanza madai ya chama hicho wakati huo ambayo amesema pia
bado wanaendelea kuyapigania hadi leo, nayo ni uchaguzi huru na wa
haki..
Aidha CUF
imewakumbusha watanzania umuhimu wa kumbukumbu hii ya kudai demokrasia
zaidi nchini hususan wakati huu ambapo Tanzania ipo katika mchakato wa
kudai katiba mpya itakayohakikisha kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi.
Serikali
ya umoja wa kitaifa visiwani Zanzibar iliyoundwa baina ya vyama vya CCM
na CUF baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ni moja ya matunda ya
maridhiano baina ya vyama hivyo kufuatia mlolongo wa migogoro ya kisiasa
iliyokuwa ikiibuka kila baada ya uchaguzi na ndipo vyama hivyo kupitia
rais wa wakati huo Aman Abeid Karume kufanya mazungumzo ya muafaka wa
kisiasa na katibu mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad.
Chanzo, voaswahili.com
No comments:
Post a Comment