Wanaotuhumiwa kwa ujambazi wa kutumia silaha
HAKIMU Mkazi wa Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya
Mbeya, Michael Mteite amewagiza wakili kuhakikisha anampeleka mtuhumiwa
mahakamani hata kwa machela.
Hakimu Mteite alilazimika kutoa kauli hiyo
wakati akisikiliza kesi inayowakabili Askari wawili wa jeshi la
Polisi na Magereza pamoja na watu watatu ambao ni
raia wa kawaida wanaotuhumiwa kwa ujambazi wa kutumia silaha.
Kauli ya Hakimu ilikuja kufuatia mmoja kati ya
washtakiwa wote watano kushindwa kuhudhuria mahakamani wakati kesi yao
ilipangwa kuendelea na ushahidi baada ya Wakili wa Serikali Archiles
Mulisa kuhoji Mhakamani kuwa Mshtakiwa namba mbili Elinanzi Mshana(22)Mkazi wa
Iyela Jijini Mbeya hajafika huku upande wa jamhuri ukiwa hauna taarifa.
Kutokana na hoja hiyo ndipo aliposimama Wakili wa
Utetezi ambaye anawasimamia watuhumiwa wote wato, Ladislaus Lwekaza na kuiambia
Mahakama kuwa Mshtakiwa namba mbili ameshindwa kuhudhuria kesi yake kutokana na
kuwa majeruhi yaliyotokana na kupigwa risasi sehemu ya paja hivyo kumfanya kuwa
na maumivu makali anayougulia akiwa gerezani.
Lwekaza alidai kuwa kutokana na mteja wake huyo
kuwa majeruhi aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi hapo mtuhumiwa huyo
hali yake itakapotengemaa na kuongeza kuwa pia hawataweza kuendelea na kesi
kutokana na washtakiwa wote kutopewa hati za mashtaka na maelezo ya mlalamikaji
ili wajiandae na utetezi.
Hata hivyo Wakili wa Serikali Mulisa alisimama na
kumuuliza Wakili wa utetezi kuwa anapaswa kuiambia mahakama kifungu alichotumia
kudai hati ya mashtaka pamoja na maelezo ya mlalamikaji sambamba na majeraha
aliyopata mtuhumiwa kuwa aliyapata wakati gani na lini.
Kwa upande wake Hakimu Mteite aliiambia Mahakama
kuwa kutokana na ubishani wa pande zote mbili ameona aingilie na kuwashauri
kuwa madai ya upande wa utetezi kuhusu hati ni haki ya kikatiba kupewa
mshtakiwa.
Mteite aliongeza kuwa madai ya majeruhi ya Mshtakiwa namba mbili ni
mbinu za kuchelewesha kesi ambazo mara nyingi hufanyika ili mahakama ishindwe
kuendelea na kesi na kuongeza kuwa yeye binafsi pamoja na mahakama hakubaliani
na suala hilo.
Alisema kama taarifa za ugonjwa huo zingikuwa za kweli Jeshi
la Magereza linajua taratibu ambapo mgonjwa hupelekwa Hospitali ambapo mahakama
ikitambua huhamishia kesi zake hospitali.
Alisema Wakili wa utetezi anapaswa kutambua kuwa mwenendo wa
Mahakama wa siku hizo tofauti na zamani ambapo kesi moja ilikuwa ikichukua hadi
zaidi ya miaka mitatu lakini sasa wamejipanga kumaliza kesi mapema kabisa.
Kutokana
na hali hiyo Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Januari
20 Mwaka huu na kumwagiza Wakili wa Utetezi Lwekaza kuhakikisha inampeleka
Mtuhumiwa siku ya kesi kwa njia yoyote hata kama ni mgonjwa namna gani ikiwa ni
pamoja na kumbeba kwa machela au gari la wagonjwa.
Pia alimwagiza mwendesha mashtaka wa
Serikali kuhakikisha anawapatia washtakiwa madai yao ambayo ni kupatiwa hati za
mashtaka, nakala ya maelezo ya mlalamikaji pamoja na mwenendo wa awali wa kesi.
Awali Mwendesha
mashtaka wa Serikali Archiles Mulisa akisaidiwa na Basilius Namkambe alisema
washtakiwa wote kwa pamoja wanatuhumiwa kwa kosa moja la unyang’anyi wa
kutumia Silaha kinyume cha Sheria kifungu cha 287 sura ya 16 kama ilivyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002.
Mulisa aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni
Mshitakiwa namba moja ambaye ni Askari Polisi PC James mwenye
namba
F8302 wa Wilaya ya Mbeya ambaye kabla ya kufikishwa mahakamani alivuliwa
Uaskari baada ya kuhukumiwa kijeshi.
Aliwataja wengine kuwa ni mshtakiwa namba mbili
kuwa ni Elinanzi Mshana(22)Mkazi wa Iyela Jijini Mbeya, Askari Magereza mwenye
namba B 500 Sajenti Juma Mussa(37) wa Gereza la Ruanda Mbeya,Mbaruku Hamis(29)
Mkazi wa Iyela na Amri Kihenya(38) Mkazi wa Iyela.
Akisoma mashtaka yao Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa
Mahakama hiyo, Michael Mteite, Mulisa alisema watuhumiwa hao walitenda kosa
hilo Januari 3, Mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika eneo la Mlima Kawetere
barabara ya Mbeya Chunya.
Alisema watuhumiwa
hao kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa kulizuia gari aina ya Pick Up lililokuwa
likiendeshwa na Ezekia Matatira (34) Mkazi wa Iyunga Jijini Mbeya
ambaye alikuwa na mtu aliyekuwa akifahamika kwa jina la Sreedhar
Pasupelet(38) mwenye asili ya Kiasia wakitumia magari madogo mawili ambayo ni
GX 100 Toyota Cresta T 782 BEU na Gari linguine ambalo lilikuwa na namba za
Chesesi GX 6011832 AINA YA Grand Mark II.
Na mbeya yetu
No comments:
Post a Comment