VITENDO vya uvunjaji wa sheria nchini,
vinavyofanywa na baadhi ya wananchi kwa kujichukulia sheria mkononi
kuwahukumu watuhumiwa, vimefikia hatua mbaya. Mkazi wa Mjimwema wilayani
Mufindi mkoani Iringa, Ezekiel Kaganga (29), amekamatwa na watu
wanaomtuhumu kwa kuiba pikipiki ya biashara maarufu bodaboda, na
kumbanika kwenye moto kama kitoweo.
Akisimulia unyama huo jana, Kaganga
ambaye amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mufindi mjini Mafinga,
alisema anafahamiana na watuhumiwa hao na kabla ya tukio hilo, Januari
7, mwaka huu walikuwa pamoja wakinywa bia katika moja ya maduka ya
kuuzia pombe mjini Mafinga.
Alisema kesho yake, Januari 8, mwaka huu
alipokea taarifa kuwa katika duka hilo la pombe lililopo katika eneo la
Mashine ya Mpunga, kuna pikipiki ilipotea katika mazingira ya
kutatanisha baada ya yeye kuondoka.
Kwa mujibu wa Kaganga, mmoja wa watu
waliokuwa wakimtuhumu kuhusika na wizi huo, alimfuata na kumtaka
arejeshe pikipiki hiyo, na yeye akamjibu kuwa hajui lolote kuhusu
kupotea kwa pikipiki hiyo.
“Jamaa hawakuridhishwa na majibu yangu
na Ijumaa ya Januari 12 nilikamatwa na polisi nikihusishwa na wizi huo
na baada ya kukosekana ushahidi, nilitolewa Januari 17,” alisema
Kaganga.
Siku tatu baada ya kutoka Polisi,
Kaganga alikamatwa na vijana hao na kupelekwa katika msitu wa Lumwago
nje kidogo ya Mji wa Mafinga. Katika msitu huo alifungwa kamba, kupigwa
viboko na baadaye alining’inizwa juu ya mti huku moto ukiwa umewashwa
chini yake.
“Nilibanikwa kama kuku, moto ukiwa chini mie nikiwa nimefungwa juu ya mti; niliachwa hapo kwa siku mbili,” alisema.
Alisema baada ya siku mbili alihamishwa
kutoka katika msitu huo na kupelekwa eneo la Machinjio mapya na
kumwagiwa mafuta ya taa ili achomwe na moto na kundi la watu
wanaokadiriwa kuwa saba.
Alidai akiwa mahututi kabla ya kuchomwa
moto, kulitokea mabishano kati ya watuhumiwa wengine wakishauri aachwe
bila kuchomwa moto, wakaamua kumuacha ambapo baadaye kidogo alichukuliwa
na wasamaria wakampeleka kituo cha Polisi.
Maeneo ambayo amejeruhiwa zaidi ni
mgongoni, makalioni, mikononi, ubavuni, miguuni na shingoni. Kaka yake
Kaganga, Isaac alisema; “mdogo wangu anaendelea kupata matibabu, na hali
yake sio mbaya sana japokuwa hawezi kutembea.”
Alisema alipata taarifa ya kupotea kwa
mdogo wake kulikokuwa kukihusishwa na wizi wa pikipiki, akawaomba
watuhumiwa wasimdhuru mdogo wake, badala yake wamsubiri arudi kutoka
safarini Arusha ili alipe pikipiki hiyo.
“Hata hivyo vijana hao hawakuwa na subira na badala yake wakamfanyia unyama waliofanya,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa,
Ramadhani Mungi amesema tayari watu wawili wanashikiliwa Polisi
wakihusishwa na tukio hilo la kinyama.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Alex Ludago (28) na Steven Michael (29) wote wakazi wa MET mjini Mafinga.CHANZ HABARI LEO
No comments:
Post a Comment