MAHAKAMA
ya mwanzo Mjini Namanyere, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa imetoa amri ya
kumtaka Ndebile Kazuri kujenga nyumba ya aliyekuwa mke wake Maria Tarafa
iliyopo kijijini Isale ambayo aliibomoa akishinikiza mtalaka wake aondoke eneo ambalo alikuwa akikaa kabla ya kutengana.
Mwishoni
mwa mwaka jana (2013) Mahakama hiyo ilivunja ndoa ya wanandoa hao wenye
watoto wanne baada ya Kazuri kuwasilisha kesi mahakamani akitaka ndoa
yake na mkewe ivunjwe. Hata hivyo baada ya kuvunjwa kwa ndoa hiyo mke
amewasilisha kesi mahakamani hapo akitaka mali za ndoa hiyo zigawanywe
na mume awajibike kuwatunza watoto wake, jambo ambalo halikuzungumziwa
kwenye kesi ya awali.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi juzi, Bi. Tarafa alisema Mahakama ya mwazo
imetoa amri ya kumtaka mtalaka wake kujenga nyumba aliyomvunjia yeye na
watoto wake wanne akishinikiza aondoke nyumbani hapo, bila kupewa haki
ya mgao wa mali zilizochumwa wakati wa ndoa.
“…Juzi
tumetoka Mahakamani nilikwenda kufungua kesi nikiiomba mahakama igawe
mali ambazo tulichuma na mume wangu muda wote wa ndoa yetu lakini mume
wangu hataki zigawanywe, ila mahakama imemuamuru kwanza ajenge nyumba
ambayo amenivunjia pale nyumbani nikiwa na watoto akitaka niondoke
nyumbani, ameambiwa awe ameimaliza kabla ya Februari 14,” alisema Bi.
Tarafa akizungumza kwa njia ya simu.
Alisema
Kazuri alivunja nyumba ambayo mkewe alikuwa akiishi na watoto wake
wanne siku chache baada ya mahakama ya mwanzo wilayani Nkasi kuvunja
ndoa yao, jambo ambalo Bi. Tarafa hakukubaliana nalo kwani alitegemea
watagawana mali ya ndoa yao na yeye kupata nyumba ya kuishi.
“…Katika
muda wote wa ndoa yetu tumefanikiwa kupata mali kama nyumba tatu ambazo
zote zipo eneo moja la kijiji cha Isale, ng’ombe zaidi ya 127, mbuzi 30
pamoja na mashamba zaidi ya hekari 70 mali ambazo hazikuzungumziwa
kabisa na mahakama, lakini baada ya ndoa kuvunjwa nashangaa mwenzangu
ananibomolea hata nyumba ambayo nilikuwa naishi mimi na wanangu…sasa
naomba kila mmoja agawiwe haki yake,” alisema Bi. Tarafa.
Kazuri
alifungua kesi katika Mahakama ya Mwanzo, Namanyere Wilaya ya Nkasi
Oktoba 28, 2013, kesi namba 26/2013 iliyosikilizwa na Hakimu aliyetajwa
kwa jina la B. Stanley; na Novemba 18, 2013 hakimu huyo baada ya
kuisikiliza kesi aliamuru ndoa ivunjwe.
Mahakama
ilivunja ndoa hiyo na kuamuru Bi. Tarafa aondoke na watoto wawili kati
ya wanne waliozaa na mumewe kipindi wakiishi kama mke na mume bila
kueleza namna watoto hao watakavyo pata huduma toka kwa baba yao.
Mahakama
pia iliamuru watoto wa miaka 7 na 9 watabaki kwa baba yao na wenye
miaka chini ya saba kubaki na mama yao. Mahakama hiyo ya mwanzo pia
iliamuru mke apewe magunia 9 ya mahindi kati ya 10 ambayo walizalisha
wote na bati 7 zilizokuwa nyumbani.
Kwa
upande wake Kazuri akizungumzia juu ya mali ambazo mkewe
anazilalamikia, alisema mali hizo alipewa na babayake wakati anaanza
maisha hivyo bado ni mali ya babayake mzazi ambaye alidai yupo hai hadi
sasa. Hata hivyo tarifa zaidi zinasema baba yake na Kazuri (Kazuri
Moshi) alifariki mwezi Machi 2004 na mali zake kurithishwa kwa watoto
wake akiwemo Kazuri.
Katika
mgao huo mtalaka wa Kazuri alisema walipewa jumla ya ng’ombe 65 lakini
wamezizalisha hadi kufikia idadi kubwa hivi sasa, ambapo ni zaidi ya
ng’ombe 127 pamoja na mashamba.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na TAMWA
No comments:
Post a Comment