Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, January 1, 2014

MAMBO KUMI(10) YALIYOTIKISA ANGA YA SIASA ZA TANZANIA MWAKA 2013


Leo tunaanza mwaka mpya, huku tukiwa na kumbukumbu ya mambo yaliyotikisa anga za siasa hapa nchini katika mwaka 2013 kama yafuatayo:
1. Rasimu mbili za Katiba
Miongoni mwa matukio makubwa kwa mwaka uliopita ni kuzinduliwa kwa Rasimu mbili za Katiba. Ya kwanza ikiwekwa hadharani Juni 3, 2013 na ya pili juzi Desemba 30, 2013.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alikabidhi rasimu hizo kwa Serikali kuamsha mjadala kuhusu mwelekeo wa nchi, baada ya rasimu hizo kubainisha uwezekano wa kutokea mabadiliko makubwa katika mfumo wa uongozi wa nchi.
Mambo makuu yaliyoibua mjadala mzito ni suala zima la kuwapo kwa serikali tatu – ya Muungano (shirikisho), Tanzania bara na Zanzibar.
2. Mawaziri wanne wang’olewa
Tukio kubwa la kufungia mwaka limetokea Desemba 20 baada ya mawaziri wanne kufutwa kazi baada ya ripoti ya madhila yaliyotokana na Operesheni Tokomeza Ujangili kuwasilishwa bungeni.
Mawaziri hao ni Balozi Khamis Kagasheki aliyekuwa Maliasili na Utalii, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
Kinachosubiriwa sasa ni Rais Kikwete kufanya mabadiliko kwenye baraza lake la mawaziri.

3. Kifo cha Nelson Mandela
Pengine tukio ambalo halijasahaulika vichwani ni kicho cha Nelson Mandela, aliyekuwa rais wa kwanza mzalengo wa Afrika Kusini hapo Desemba 5, 2013.
Kutokana na msiba huo wa dunia, viongozi zaidi ya 100 wakiwamo wakuu wa nchi na Serikali walishiriki hatua mbalimbali za safari ya mwisho ya mzee huyo maarufu kama Madiba.
Mandela alizikwa Jumapili, Desemba 15, 2013 katika Kijiji cha Qunu alikokulia, mazishi ambayo Rais Jakaya Kikwete alipata fursa ya kuhutubia na kueleza nafasi ya Tanzania ilivyoshiriki katika harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.
4. Kikwete ahutubia Bunge
Mwezi Novemba Rais Jakaya Kikwete alihutubia Bunge lengo kubwa likiwa ni kufafanua kuhusu kuzorota kwa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC). Pia aligusia ushindi wa majeshi ya Umoja wa Mataifa yakijumuisha askari kutoka Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), Katiba Mpya, na Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo baadaye imekuja kusababisha mawaziri wake wane wafukuzwe kazi.
5. Chadema uamuzi mgumu
Vilevile Novemba 22, Chadema kilimvua madaraka yote Zitto Kabwe aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mjumbe wa Kamati Kuu na Baraza Kuu kwa maelezo kuwa anakwenda kinyume na taratibu za chama hicho.
Pamoja na Zitto wengine waliovuliwa nyadhifa zao ni Samson Mwigamba aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha na Mjumbe wa Kamati Kuu na Baraza Kuu, Dk Kitila Mkumbo.
Viongozi hao wamepinga uamuzi huo wa Kamati Kuu na kukata rufaa kwenye vikao vya juu, uamuzi unayotarajiwa kutoka mapema mwezi huu.
6. Malumbano, matusi bungeni
Mwaka uliopita Bunge lilitawaliwa na matukio makubwa na mijadala mizito iliyoibua hisia kali, malumbano na wakati mwingine matusi yaliyowaacha wananchi midomo wazi.
Mojawapo ya mijadala hiyo ni ule wa Aprili 15, ambapo Ezekiel Wenje (Nyamagana) alitoa kauli za kukituhumu chama cha CUF kuwa na uhusiano na vyama vya kiliberali vinavyosapoti ushoga, hali iliyoibua majibu mazito kutoka kwa wabunge wa CUF kwamba Chadema “ni wehu, wahuni, wazushi na wameidhalilisha CUF”.
Katika hatua nyingine wabunge wakichangia hotuba ya Waziri Mkuu, Mbunge wa Kondoa Kusini (CCM), Juma Nkamia alijibizana na Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini-Chadema), alisema kuwa yeye “haongei na mbwa bali mwenye mbwa.” Naye Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde alitoa kauli ya iliyotafsiriwa kuwa ya kuudhi kuwa kuna “wabunge bungeni wenye mimba zisizitarajiwa.” Kauli nyingine iliyochoma masikio ya wabunge na wananchi ilikuwa ya Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini- Chadema) ya “akili ndogo kutawala akili kubwa” na wakati mwingine kutumia kifungu cha Biblia katika Kitabu cha Mithali 27:22, kinachosema kuwa; ‘Hata ukimtwanga mpumbavu kwenye kinu pamoja na ngano, upumbavu wake hautamtoka.
7. Makonde bungeni
Ukiacha zile kauli zilizolalamikiwa kuwa ni za kuudhi, mwaka 2013 ilifika wakati Bunge likawa kama sinema wakati maofisa usalama walipolazimika kumbeba mzobemzobe Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu).
Katika tukio hilo, ambalo maofisa usalama walitakiwa kumtoa nje Kiongozi wa Kambi Rasimu ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe huku wabunge wa kambi hiyo wakipinga kutolewa nje. Ilidaiwa kuwa Sugu alimrushia ngumi mmoja wa askari.
8. Lema ashinda rufaa ya ubunge
Mwezi Aprili 2013 Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema aliyekuwa nje ya Bunge baada ya ubunge wake kutenguliwa na Mahakama Kuu alishinda rufani baada ya Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali maombi ya marejeo na kuamua arudi bungeni.
Maombi ya marejeo yalikuwa yamewasilishwa mahakamani hapo na makada watatu wa CCM mkoani Arusha, kupitia kwa mawakili wao Alute Mughway na Modest Akida wakiiomba Mahakama ya Rufani ifanye marejeo ya hukumu yake hiyo kwa madai kuwa hukumu ya Mahakama ya Rufaa iliyomrejeshea ubunge wake haikuwa sahihi.
9. Kicheko Aeshi Hilary
Furaha ya kurudi bungeni haikuishia kwa Lema, Mei 6, kicheko kilihamia kwa Aeshy Hilary baada ya Mahakama ya Rufani, kumthibitisha kuwa ni mbunge halali wa Sumbawanga Mjini baada ya kushinda rufaa aliyokata kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga, iliyomvua ubunge.
Hilaly alivuliwa ubunge na aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Bethuel Mmila Aprili 30, 2012, kutokana na kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti hicho katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 kupitia Chadema, Nobert Yamsebo.
10. Dk Kafumu kidedea Igunga
Ilipotimu Mei 9, msimu wa furaha ukahamia Igunga pale Dk Dalali Kafumu wa CCM, ambaye ushindi wake uliokuwa umebatilishwa na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, alirejeshewa ubunge wake na Mahakama ya Rufaa.
Dk Kafumu katika uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi iliyoachwa na Rostam Aziz aliyejiuzulu, alimshinda Joseph Kashindye wa Chadema. Kashindye alipinga ushindi huo kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi na ubunge huo kutenguliwa.
Sakata la gesi Mtwara
Ingawa suala hili lilianza katika mwaka uliotangulia wa 2012, mwaka 2013 umeshuhudia maandamano makubwa, hasira za baadhi ya wananchi waliojichukulia hatua mkononi na kuchoma majengo na magari, pia hatua za Serikali katika kutuliza vurugu hizo za kupinga gesi kusafirishwa kwa bomba kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Hali hiyo ilitulizwa na sasa ujenzi wa bomba unaendelea na hivyo kuweka matumaini kuwa ugunduzi wa gesi nyingi hapa nchini unaweza sasa kuwa wa manufaa badala ya kuwa mkosi kama ambavyo ilikuwa imeanza kuonekana.


MWANANCH

No comments:

Post a Comment