Mwaka 2013 ulimalizika vibaya kwa Chadema. Vivyo hivyo mwaka huu ulianza vibaya baada ya kuingiliwa na ‘bundi’ wa migogoro aliyepania kukipasua katika makundi mawili.
Hali hiyo iliendana na uamuzi mgumu wa Kamati Kuu
ya chama hicho kuwavua nyadhifa za juu viongozi watatu – Naibu Katibu
Mkuu, Zitto Kabwe, Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo na Mwenyekiti
wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Kamati Kuu haikuishia hapo, baadaye ikawavua
uanachama Dk Mkumbo na Mwigamba, huku Zitto akinusurika baada ya
kufungua kesi mahakamani.
Athari za uamuzi huo zilisababisha baadhi ya
viongozi wa ngazi mbalimbali ndani ya Chadema kutofautiana kimsimamo
huku wengine wakifikia hatua ya kujiuzulu nafasi zao.
Miongoni mwa waliojiuzulu ni pamoja na aliyekuwa
Makamu Mwenyekiti wa Taifa, Said Arfi na wenyeviti kadhaa wa mikoa,
walioeleza wazi kuwa wanapinga Zitto kuvuliwa nyadhifa zake.
Mbaya zaidi ni pale mvutano huo uliposambaa hadi
kwa mashabiki wa kawaida, nao wakaonekana kugawanyika katika makundi
mawili, moja likimuunga mkono Zitto na jingine likibakia upande wa
chama.
Hata hivyo, ingawa agenda hii haikuwekwa wazi,
uongozi wa chama hicho umeibuka na mbinu ya kukabiliana na ‘bundi’ huyo
wa mgawanyiko kwa kampeni maalumu iliyopewa jina la Operesheni Pamoja
Daima, itakayofanyika katika mikoa tisa.
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe anasema
lengo kuu la kuanzisha operesheni hiyo ni pamoja na kukiimarisha chama
na kuwafumbua macho Watanzania juu ya mchakato wa Katiba Mpya
unaoendelea. Operesheni hiyo ya siku 14 inayoendelea katika mikoa yote
isipokuwa Lindi na Mtwara, inaendeshwa na makundi sita ya viongozi
matatu yakitumia helkopta na wengine magari.
Swali la kujiuliza ni je, kufanyika kwa operesheni hii kutasaidia kumfukuza ‘bundi’ huyo aliyeanza kukipasua chama?
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema juhudi
hizo zinaweza kufanikiwa kwa kiwango kizuri kwa kutegemea mwamko wa
kisiasa wa mikoa wanayokwenda.
Ni njia sahihi
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kiraia ya kufuatilia
Utendaji wa Bunge (CPW), Marcossy Albanie anakubaliana na uamuzi wa
chama hicho akisema operesheni hiyo ndiyo njia sahihi inayoweza
kukiimarisha zaidi chama hicho. Albanie anasema harakati za kuanzisha
operesheni hiyo ni pamoja na kuongeza mwamko wa Watanzania kabla ya
Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015. Anasema mgogoro uliojitokeza ndani ya
chama hicho hauwezi kuwa sababu pekee ya kuanzisha operesheni hiyo.NA GAZETI LA MWANAINCHI
No comments:
Post a Comment