Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, January 20, 2014

WAZIRI MKUU AAGIZA HALMASHAURI ZITUMIE VIJANA

pm1..Waziri Mkuu Mhe. Mizonge Pinda akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa Nehemia Mchechu mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi ambapo alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufungaji wa mafunzo kwa Vijana waliowezesha kupata taaluma ya utengenezaji wa matofali kwa teknolojia ya kisasa. leo jijini Dar es Salaam.
………………………………………………………………………………………………..
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amezitaka Halmashauri zote 160 za Miji na Wilaya zilizoko nchini kuhakikisha zinaunda vikundi vya vijana vya ujenzi wa nyumba nafuu (building brigades) ili viwe sehemu ya miradi ya kila Halmashauri.
Ametoa agizo leo (Jumatatu, Januari 20, 2014) wakati akizungumza na wahitimu wa mafunzo ya wataalam wa mashine za kutengeneza matofali kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kwenye hafla fupi iliyofanyika Mwenge jijini Dar es Salaam.
Mafunzo hayo yaliyoanza Januari 6 – 17, mwaka huu yaliendeshwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kushirikiana na Wakala wa Utafiti wa Vifaa Bora vya Ujenzi (NHBRA) iliyo chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.  
Mafunzo hayo ambayo yanahusu namna ya kutumia mashine za Hydraform ni pamoja na kutambua udongo unaofaa kutengenezea matofali na namna ya kujenga kwa kutumia matofali hayo.
Waziri Mkuu alisema alimshawishi Mkurugenzi Mtendaji wa NHC, Bw. Kyando Mchechu atafute mbinu za kutumia teknolojia rafiki wa mazingira ili kuepuka janga la uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi makubwa ya kuni mbichi ili kuchoma matofali.
“Licha ya kuwa utengenezaji wa matofali ya kuchoma unatekeleza azma ya Serikali ya kutaka wananchi wake wawe na nyumba bora, kwa kweli roho huwa inaniuma hasa ukizingatia kiasi kikubwa cha miti inayokatwa kuyachoma hayo matofali hadi yawe imara, tena ikiwa mibichi,” alisema.
Aliipongeza Wakala wa Utafiti wa Vifaa Bora vya Ujenzi (NHBRA) kwa kubuni mashine hizo ambazo alisema zinauzwa kwa bei ambayo Halmashauri inaweza kuzimudu. “Mkurugenzi Mkuu ameniambia kila mashine inauza kwa sh. 450,000/- na inaweza kutengeneza matofali 700 kwa siku moja… hayo matofali yanatumia mifuko saba tu ya saruji. Hili ni jambo linalowezekana!” alisisitiza.
“Wakurugenzi wapangeni vijana wenu katika building brigades  ili wanufaike na mapando huu. Na Wakurugenzi wa Dodoma itabidi tuwapigie kelele ili wawasimamie wananchi waweze kupata nyumba kupitia mpango huu,” aliongeza.
Alisema anataka wachangamkie haraka hizo mashine kwa sababu  zinasaidia uhifadhi wa mazingira, zinachochea ufanisi wa teknolojia, zinapunguza gharama za ujenzi na zinasaidia kutoa ajira kwa vijana.
“Kila Halmashauri itapewa mashine nne, na kila mashine inahudumiwa na vijana 10 kwa hiyo itachangia ajira ya moja kwa moja kwa vija 6,400. Hata hivyo aliwasihi watakaoendesha miradi hiyo wasitoze bei kubwa kwa matofali watakayotengeneza ili wananchi wengi waweze kumudu bei na wabadili hadhi za makazi yao,” alisema.
Alimtaka Bw. Mchechu aweke mpango wa kuendeleza kampeni hiyo kwa miaka mitano mfululizo ili uweze matokeo chanya kwa jamii badala kuanzisha mwaka na kuachia katikati.
Mapema, Mkurugenzi Mtendaji wa NHC, Bw. Kyando Mchechu alisema chini ya mpango wa kusaidia miradi ya maendeleo inayofanywa na jamii (CSR), Shirika lake limekuwa linachangia sekta za afya na elimu na hivi sasa wamelenga vijana hasa kutoa ajira katika sekta ya ujenzi.
“Shirika limegawa mashine 640 za kufyatulia matofali na kila Halmashauri itapatiwa mashine nne, …kwa kuanzia NHBRA wameahidi kutoa mashine 320 kwa mkupuo mara zitakapokamilika,” alisema.
Aliwasihi wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri watoe ushirikiano kwa shirika hilo ili mpango huo wa kutoa jaira kwa Vijana uweze kufanikiwa.
Mafunzo hayo yalihusisha wataalamu 50 waili kutoka kila mkoa ambapo kati yao 34 walikuwa ni walimu wa VETA na 16 ni wahitimu wa VETA.
NHC na Tumeelezwa na VETA zimekubaliana ya kuwatumia vijana waliohitimu VETA kutengeneza matofali katika Kanda Tano zenye miradi ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu wakitumia mashine za kisasa za Hydraform.

No comments:

Post a Comment