MBUNGE
wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amesema kuanzia sasa hataki
malumbano na mtu. Kauli ya Zitto, imekuja siku moja baada ya Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kupiga marufuku chombo chochote kujadili
uanachama wake. Akizungumza na MTANZANIA mjini Dar es Salaam jana, Zitto
alisema ameamua kukaa kimya ili kupata muda mzuri wa kutafakari
misukosuko ya kisiasa aliyokumbana nayo.
“Kuanzia
sasa naomba kukwambia sitaki malumbano na mtu, natafakari misukosuko ya
kisiasa niliyokumbana nayo kwanza,” alisema Zitto.
Alisema hayuko tayari kujibizana na mtu yeyote na kwamba anataendelea kufanya kazi ya kuwawakilisha wananchi wa jimbo lake.
Alisema
jukumu jingine lililo mbele yake ni kutunga sheria ndani ya Bunge na
kuisimamia Serikali kupitia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
“Kazi
kubwa iliyoko mbele yangu hivi sasa, ni kuwatumikia wapiga kura wa
jimbo langu, kutunga sheria za nchi kwa manufaa ya Watanzania na
kuisimamia Serikali kupitia kamati yangu,” alisema Zitto.
TUNAOMBA BOFYA HAPA NA ULIKE PAGE YETU KWA HABARI NYINGI ZA KILA SIKU,(USIPITWEEEEEEEE)
Zitto
alitoa kauli hiyo, baada ya kutakiwa na MTANZANIA kutoa msimamo wake,
baada ya CHADEMA kumtangaza kuwa yeye ni mbunge wa mahakama.
Alisema hivi sasa majukumu yaliyoko mbele yake ni makubwa, hivyo haoni kama kuna umuhimu wa kuendeleza malumbano.
Juzi
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, chini ya Jaji John Utamwa, ilitoa
uamuzi wa maombi yaliyowasilishwa na Zitto kupitia wakili wake, Albert
Msando, kwa hati ya dharura Januari 2, mwaka huu.
“Nakubaliana na hoja za Wakili Msando, pande mbili zinapopingana lazima shauri lao lisikilizwe mahakamani ili haki itendeke.
“Mdai
akivuliwa uanachama, akapoteza nafasi yake ya ubunge, Serikali
italazimika kufanya uchaguzi mdogo, kufanya uchaguzi mdogo ni hasara kwa
Serikali, kwani utahusisha hadi wapiga kura, hali itakayosababisha
fedha nyingi kutumika, itakuwa hasara kwa Zitto kupoteza nafasi mbili,
ya ubunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kabla
kesi yake ya msingi haijasikilizwa,” alisema Jaji Utamwa.
Alisema
kwa kuzingatia hoja zilizowasilishwa, mahakamani ilikubaliana na maombi
ya mdai, hivyo inatoa zuio kwa Chadema na chombo chochote kujadili
uanachama wa Zitto hadi kesi ya msingi itakapomalizika kusikilizwa.
Kabla
ya kutoa uamuzi huo, mahakama hiyo ilitupilia mbali hati kinzani
iliyoapwa na mawakili wa Chadema, Tundu Lissu na Peter Kibatala,
kutokana na makosa ya kisheria.
Pamoja
na hati hiyo, pia mahakama iliziondoa aya tatu katika hati ya kiapo
aliyoapa Wakili Kibatala kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini wa chama hicho
na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willbroad Slaa kwa sababu hakueleza
alichoandika alikipata wapi.
Maombi yaliyotolewa uamuzi juzi yalikuwa dhidi ya Baraza la Wadhamini la Chadema pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Slaa.
Katika
kesi ya msingi iliyopo mahakamani hapo, Zitto anaiomba mahakama izuie
kamati hiyo kujadili uanachama wake hadi rufaa yake itakaposikilizwa na
Baraza Kuu la chama hicho na anaomba mahakama imwamuru Dk. Slaa ampe
nakala za taarifa za vikao vilivyomvua uongozi ili akate rufaa.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment