Raia
watatu wa Syria wamekamatwa walipokuwa wakijiandaa kusafiri kupitia
uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA) kuelekea Rome
Italy kwa kutumia ndege ya Italy yenye nambari 193253 tarehe
29/01/2014.
Raia
hao ni Mamdoh ALasfar Yousuf aliezaliwa tarehe 01/08/1975 katika mji wa
Hama Syria, Mohd Akram Adnan aliyezaliwa tarehe 14/01/1995 Damascus na
Bibi Razan Adnan Alkurdi aliezaliwa Damascus tarehe 01/01/1994.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Uhamiaji Zanzibar kwa vyombo
vya habari, Mamdoh Alasfar Yousuf alikuwa na pasi ya kusafiria nambari
006011215 iliyotolewa tarehe 24/02/2011 Hama Syria na aliingia nchini
kwa mara ya kwanza tarehe 21/12/2013 kupitia AAKIA na kuondoka tarehe
29/12/2013 kwa kupitia AAKIA akiwa na pasi yake halali ya kusafiria.
Mamdoh
alikamatwa AAKIA akitumia pasi ya kusafiria ya Taifa la Bulgaria yenye
nambari 308991470 iliyotolewa tarehe 28/05/2010 kwa kutumia jina la
kughushi ambalo ni Anastas Dimitrov Karabobov.
Mohd
Akram Adnan alikuwa na pasi ya kusafiria nambari 0073573492 iliyotolewa
tarehe 22/10/2012 aliingia nchini kwa mara kwanza tarehe 15/01/2014
kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambare Nyerere (JKNIA)
akiwa na pasi yake halali ya kusafiria.
Mohd
alikamatwa AAKIA akitumia pasi ya kusafiria ya kughushi ya Taifa la
Luxembourg yenye nambari G 76CB80 iliyotolewa tarehe 14/07/2009 yenye
jina la kughushi Hosam Jaber.
Taarifa
hiyo imeongeza kuwa Bibi Razan Adnan Alkurdi alikuwa na pasi ya
kusafiria nambari 006425707 iliyotolewa tarehe 27/08/2011 na aliingia
nchini tarehe 15/012014 kupitia JKNIA.
Razan
alikamatwa AAKIA akitumia pasi ya kusafiria ya kughushi ya Taifa la
Sweden yenye nambari 0966629944 iliyotolewa mwezi Disemba 2004 kwa
kutumia jina la Laila Mohd.
Raia
hao walizuiliwa kuondoka nchini kwa vile waligundulika kutumia pasi za
kusafiria za kughushi ambalo ni kosa kwa mujibu wa sheria za Uhamiaji
pamoja na sheria za kimataifa za kusafiria kifungu 31(1)(e)(g)(o).
Baada
ya kuhojiwa na kufanyiwa uchunguzi wa kina na Maafisa Uhamiaji
ilibainika pamoja na kuwa na hati za kusafiria za kughushi walikuwa na
pasi zao halali za kusafiria pamoja na tiketi rejea walipoondokea.
Baada
ya kuhojiwa raia hao walipelekwa Polisi Madema ambako walikaa kwa muda
wa siku mbili na baadae wakakaa Hoteli ya Tembo siku moja na
wakasafirishwa na Afisa Uhamiaji husika kupitia AAKIA.
Taarifa
hiyo imebainisha kwamba kwa mujibu wa taratibu za kimataifa za usafiri
zinazoongozwa na Shirika la Kimataifa la usafiri (ICAO) zinaelekeza
msafiri aliegundulika kufanya makosa ya kiuhamiaji anatakiwa kurejeshwa
kituo cha mwisho alichoondokea, hivyo Idara ya Uhamiaji Zanzibar
iliwarejesha raia hao wa Syria Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa JKNIA
tarehe 31/01/2014 ambacho ni kituo walichoingilia nchini. Kunataarifa
kuwa JKNIA wameshawarejesha raia hao wa Syria kituo walichotoka.
Uchunguzi
wa awali wa tukio hilo inaonekana raia wa kigeni hasa kutoka mataifa
yenye mizozo wanakimbilia nchi mbali mbali za Ulaya kwa kupitia baadhi
ya nchi ikiwemo Tanzania na mara nyingi kusaidiwa na wenyeji wenye nia
mbaya kama ilivyojitokeaza katika tukio hilo.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR


No comments:
Post a Comment