Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
SHIRIKISHO la
Soka Tanzania (TFF) limesitisha matumizi ya tiketi za kielektroniki
kwenye viwanja vinane mpaka itakapotolewa taarifa nyingine.
Habari zilizopatikana Dar es Salaam jana, zilisema TFF imeamua kufanya hivyo baada ya kubaini madudu mengi katika tiketi hizo.
Uwanja
wa Azam Complex uliopo Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam
ambao unatumika kwa tiketi hizo, haukutumia tiketi hizo katika mechi
yake ya juzi dhidi ya Kagera Sugar ya Kagera.
Hata
hivyo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Boniface Wambura alipotafutwa
kuzungumzia hilo, simu yake ya mkononi iliita bila majibu na hata
ujumbe ufupi wa maneno aliotumiwa, hakuujibu.
Lakini
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF Kanda ya Kaskazini (Tanga na
Kilimanjaro), Khalid Mohamed alisema mfumo huo sio tu unachanganya,
lakini pia mashine zimeharibika.
“Sisi
jana (juzi) hakukuwa na mechi kwenye Uwanja wa Mkwakwani, lakini katika
mechi zijazo, hatutatumia tena mfumo wa kielektroniki, maana sio kwamba
hatutaki, lakini hata hizo mashine zenyewe mbili zilizofungwa
zimeharibika,” alisema Mohamed.
Lakini
mtoa habari wetu alithibitisha jana kuwa licha ya kusimamishwa kwa
tiketi hizo, pia jana kulikuwa na kikao kuzungumzia suala hilo ambalo
limegonga vichwa tangu kuanza kutumika katika mzunguko wa pili wa Ligi
Kuu ya Tanzania Bara ulioanza Januari 25, mwaka huu.
Juzi,
Kamati ya Utendaji ya TFF ilikutana na kuiagiza Sekretarieti, Benki ya
CRDB na Bodi ya Ligi kufanya kikao cha dharura kwa ajili ya mapitio ya
tiketi hizo ambazo zimekuwa na malalamiko.
Viwanja
vilivyofungwa mfumo wa tiketi za kielektroniki ni Azam Complex, Kaitaba
Bukoba, Jamhuri Morogoro, Kumbukumbu ya Sokoine Mbeya, Shekhe Amri
Abeid Arusha, CCM Mkwakwani Tanga na CCM Kirumba Mwanza.
CHANZO HABARI LEO

No comments:
Post a Comment