skip to main |
skip to sidebar
ASKARI FFU ZANZIBAR APIGWA RISASI.
KWA UFUPI
Alikuwa akijaribu kumsaidia mwenzake aliyekuwa amevamiwa na majambazi eneo la hoteli.
Zanzibar.Askari wa Kikosi cha FFU, Mohamed Mjombo (Namba E 5607)
ameuawa kwa kupigwa risas, huku mwingine akijeruhiwa baada ya majambazi
kuvamia hoteli ya kitalii ya Pongwe Bay iliyo Pongwe mkoani Kusini
Unguja.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kamishna wa Polisi
Zanzibar, Hamdan Omar Makame alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 3:00
usiku wakati wageni wakiwa wamepumzika na askari hao wa FFU kutoka Kituo
cha Polisi Machui wakiwa katika lindo kwenye hoteli hiyo.
Kamishna Hamdan alisema muda huo lilifika gari moja na baada ya
kuegeshwa watu watatu waliteremka na kumvamia askari mweye Namba F 6198,
Ibrahim Juma Mohamed na kujaribu kumnyang’anya silaha aina ya SMG na
katika purukushani hiyo walimpiga risasi ya begani.
Alisema askari huyo anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.
“Majambazi walifanikiwa kumpora bunduki aina ya SMG na kisha kumpiga
risasi na kumjeruhi begani. Tuko katika msako mkubwa hivi sasa,” alisema
Kamishna huyo wa Polisi Zanzibar.
Hata hivyo, alisema wakati
Mjombo akisonga mbele kujaribu kumsaidia mwenzake, alifyatua risasi
lakini ikakwama katika chemba na majambazi hao kufanikiwa kumpiga risasi
sehemu ya ubavu na kutoroka.
Alisema askari huyo wa FFU
alifariki majira ya saa 7:00 usiku katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na
kuzikwa jana huko Bambi Mkoa wa Kaskaszini Unguja. Watu wawili
wanashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo na wengine wanaendelea
kusakwa.
“Tayari tumepeleka kikosi cha askari maalumu kutoka
Mkoa wa Mjini Magharibi na Mkoa wa Kusini Unguja, ili kuhakikisha
usalama unaimarishwa katika maeneo ya ukanda wa utalii,” alieleza
Kamishna Hamdan.
Daktari bingwa wa Hospitali ya Mnazi Mmoja,
Msafiri Marijani ambaye ndiye aliyemfanyia uchunguzi Mjombo, alisema
askari huyo alipoteza damu nyingi baada ya kupigwa risasi ubavu wa
kushoto na kutokea paja la kulia na ndio maana alipoteza maisha.
“Uti wa mgongo pia ulivunjika,” alisema Dk. Marijani. “Amepoteza damu
nyingi iliyokuwa ikivuja ndani ya tumbo na nje. Risasi bado
haijapatikana mahali ilipo mwilini.”
Akizungumzia tukio hilo,
mwenyekiti wa Jumuiya ya Uwekezaji Katika Sekta ya Utalii Zanzibar
(ZAT), Abdulswamad Said alisema wakati umefika kwa SMZ kuimarisha ulinzi
katika Ukanda wa Utalii kwa vikosi vya SMZ na Polisi kufanya kazi
pamoja ili kulinda wawekezaji, watalii na wananchi.
Abdulswamad
alisema uongozi wa ZAT uliwahi kukutana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali
Mohamed Shein na kuomba vikosi vya SMZ viongezewe nguvu za ulinzi ili
kukabiliana na matukio ya uhalifu na kusema jambo la kushangaza pamoja
na Rais kutoa agizo hilo, hakujawa na utekelezaji wa wazi.
“Matukio ya watu kumwagiwa tindikali, milipuko ya mabomu na uhalifu wa
kutumia silaha hayatoi sura nzuri kwa maendeleo ya utalii Zanzibar.
Juhudi zaidi zinahitajika kukabiliana na vitendo hivyo hatari,” alisema
mwenyekiti huyo wa ZAT.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza
kuwa majambazi hao walikuwa wamebeba silaha za kivita na kuaminika
huenda walikuwa na silaha aina ya AK 47, lakini hawakufanikiwa kupora
mali hotelini hapo.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment